Thursday, April 21, 2011

Serikali kuvua gamba kama CCM

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, amesema, baada ya Operesheni Vua Gamba kukamilika ndani ya chama hicho, mkakati huo utahamishiwa kwa watendaji wote wa Serikali wanaoshindwa kutekeleza Ilani ya Chama hicho.

Alisema hayo juzi wakati yeye na Naibu Katibu Mkuu CCM, Bara, John Chilligati waliposalimia wananchi wa Iringa Mjini katika mkutano wa hadhara uliofanyika nje ya ofisi kuu ya CCM ya mkoa mjini hapa.

Nnauye alisema, katika kukisafisha chama hicho baada ya Sekretarieti mpya kuundwa, viongozi wote ndani ya chama wanaotajwa kwenye kashfa kubwa zikiwamo za Richmond, Kagoda, Dowans na Rada, wanatakiwa ndani ya siku 90 walizopewa wawe wamejiuzulu nyadhifa zao.

"Tumewaambia wenzetu mnaotajwatajwa kwenye kashfa hizo, jipimeni wenyewe na kisha mwajibike, vinginevyo tutawakamata na kuwatosa kwa aibu," alisema na kuongeza, kwamba baadhi yao wamekwishaandikiwa barua za kuombwa wajiuzulu.

Hata hivyo, alisema kipimo cha nani anatakiwa kuachia ngazi ndani ya chama hicho wanacho wao wenyewe na kamwe hawatatumia kelele za chuki kutoka kwa baadhi ya wapinzani.

Nnauye alisema, Operesheni hiyo inayotarajiwa kwenda hadi ngazi ya mashina na matawi, itaingia serikalini kwa sababu wanawafahamu baadhi ya watendaji wasiotekeleza Ilani ya chama hicho zaidi ya kujaza matumbo yao.

Alisema, kufanikiwa kwa Operesheni hiyo kutakiwezesha chama hicho kuingia katika uchaguzi wake mkuu ujao na wa Serikali wa mwaka 2015 kikiwa na sura za viongozi waadilifu na kurudisha imani kwa wananchi.

Chilligati aliwataka viongozi waliosababisha chama hicho kupoteza umaarufu hata kukifanya kipoteze baadhi ya majimbo, kuacha kusubiri uamuzi wa kujiuzulu nyadhifa zao, ili kuwapisha wanachama wengine waadilifu na wenye uwezo kuongoza chama hicho.

"Wanaokitesa chama mpaka kinasemwa vibaya si tu kwamba wako kule kwenye NEC hata huku kwenu wapo na mnawafahamu na ndiyo maana katika uchaguzi mkuu mwaka jana tulipoteza jimbo hili la Iringa Mjini kwa Chadema," alisema.

Chilligati alisema, kwa kuwa mageuzi ya sasa ndani ya chama hicho yanataka kukirudisha kwa wanachama wenyewe, viongozi watakaochaguliwa watapatiwa mafunzo yatakayowawezesha kufanya kazi za siasa kwa wanachama wanaowachagua.

"Pamoja na mkutano huu, kubwa lililotuleta hapa Iringa ni kumkabidhi Nnauye Chuo chetu cha Siasa cha Ihemi ili akijenge upya," alisema.

Alisema chuo hicho kilichopo nje kidogo ya mji wa Iringa, kitatumika kutoa mafunzo kwa viongozi wa ngazi zote watakaochaguliwa katika uchaguzi mkuu wa chama hicho, mwakani.

Shughuli za kumkabidhi Nnauye chuo hicho zilifanyika jana chuoni hapo.

No comments: