Thursday, April 21, 2011

Atunukiwa tuzo ya kimataifa ya Mwanamke Jasiri

UBALOZI wa Marekani nchini, umemtunuku Mkurugenzi Mtendaji na mwanzilishi wa taasisi ya kutetea haki za mwanamke ya Kivulini Women’s Rights Organization ya Mwanza, Maimuna Kanyamala Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri ya mwaka 2011.

Akizungumza kabla ya kumkabidhi tuzo hiyo Dar es Salaam jana, Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt alisema ubalozi wake umemtunukia Kanyamala kutokana na kujielekeza katika kutetea haki za wanawake hususani katika kusisitiza kuweka mazingira ya mazuri ya kuishi wanawake katika jamii ni kuondokana na vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Katika kutimiza majukumu yake, alikutana na changamoto nyingi sana kutoka kwa jamii, wakipinga kampeni za kuhamasisha jamii kupata uelewa, Kanyamala amekumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa wapinzani wake katika ukanda wake walikuwa wanamtuhumu kuwa ni chanzo cha ‘kuwavimbisha vichwa wanawake’ na ni ‘mpinzani wa wanaume,” alisema Balozi Lenhardt.

Aidha, Balozi Lenhardt alisema tatizo la unyanyasaji wa kijinsia ni tatizo kubwa ulimwenguni na kuwa nchi yake imejikita kusaidia zaidi ya Dola za Marekani milioni saba kwa ajili ya kupunguza ubaguzi wa kijinsia na vitendo vya kikatili kwa Tanzania.

Kanyamala anakuwa ni mwanamke wa nne kutunukiwa tuzo hiyo iliyoanzishwa kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa mwanamke aliyeonesha ujasiri wa kiwango cha juu na uongozi mzuri katika kutetea masuala ya haki za wanawake.

Wengine ni Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya kwa mwaka 2010, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (2009) kutokana na ujasiri aliouonesha katika kukosoa na kuupa changamoto uongozi wa chama chake ili ushughulikie kikamilifu rushwa na Helen Kijo-Bisimba (2008) wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kusaidia na kuimarisha haki za wanawake.

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, pamoja na Ubalozi wa Marekani kutambua mchango wa watu walio chini kabisa, Kanyamala alisema pamoja na kukumbana na changamoto nyingi, kamwe hatarudi nyuma kutetea na kukomesha vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

“Tangu kuanzishwa kwa taasisi yetu zaidi miaka ya 10 iliyopita, tumekutana na changamoto nyingi, watu walifikia hata kunihoji kama vile nimeolewa na kuonekana napingana na mila na desturi na pia imani za dini za watu, lakini hayo yote hayakunifanya nirudi nyuma,” alisema mama huyo ambaye ameshawasaidia wanawake zaidi ya 2,000 katika kanda hiyo.

Naye Kilango alisema akiwa mbunge na mwanamke, atapaza sauti bungeni ili kumzungumzia kazi ya Kanyamala ambayo inatakiwa kufanywa na viongozi na pia kutoa changamoto kwa wanawake wengine kupambana na vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake.

No comments: