Monday, April 11, 2011
Mkuchika: Ufisadi ndio umetumaliza
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bara, Kapteni George Mkuchika, amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaonekana machoni mwa umma kuwa kinakabiliwa na tuhuma za ufisadi. Mkuchika aliwaambia waandishi wa habari mjini Dodoma jana kuwa kutokana na hali hiyo, imeonekana kuwa na umuhimu wa kubadili timu ya uongozi yaani Sekretarieti na Kamati Kuu (CC). Alisema CCM kina wapenzi wengi ambao wanaendelea kukiamini kwa kuwa si viongozi wote wanakabiliwa na tuhuma za rushwa. Aliongeza kuwa hata tathmini iliyofanywa na mikoa haikueleza kama ni wanachama wote na viongozi wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi. Mkuchika alisema kuwa anaamini watu wapya wa watakaochaguliwa na wajumbe wa NEC watafanya vizuri kazi za chama. Mkuchika alisema sekretarieti mpya itaundwa na watu watakaokuwa kazini wakati wote kwa lengo la kushiriki vizuri katika mapambano ya kisiasa. Kwa mujibu wa Mkuchika, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), mpambano wa kisiasa umekuwa mkubwa kuliko ilivyokuwa wakati wa chama kimoja. Juzi saa 5:30 usiku aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi, John Chiligati, alizungumza na waandishi wa habari na kuthibitisha kujiuzulu kwa sekretarieti na CC, hatua ambayo aliieleza kuwa ni mwanzo wa mageuzi ndani ya CCM kwa lengo la kujijenga upya na kukiimarisha katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Akizungumza baada ya kumalizika kwa kikao cha CC, Chiligati alisema imeonekana kuwa kuna haja ya kukifanyia chama mageuzi. “Aidha, kamati Kuu imejadili kwa kina ajenda kuhusu hoja na haja ya mageuzi ndani ya Chama na imefanya uamuzi wa wajumbe wote kujiuzulu ili kumpa nafasi Mwenyekiti wa Chama kuunda upya Kamati Kuu na sekretarieti ya chama,” alisema. Chiligati alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa falsafa ya kujivua gamba aliyoitangaza Rais Kikwete wakati wa sherehe za miaka 34 ya CCM mjini Dodoma. Kikao cha NEC kilianza jana saa 6:00 mchana huku miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni uteuzi wa wabunge na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walioomba kuwa wajumbe wa chombo hicho. Pia kikao hicho kitafanya uteuzi wa Katibu wa Kamati ya wabunge wa CCM na Katibu wa Wawakilishi wa CCM; tathmini ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na taarifa kuhusu muswada wa Sheria ya Marejeo ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ameomba ushirikiano wa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili kukivusha chama hicho. Rais Kikwete alisema hayo jana mchana mjini Dodoma wakati akifungua kikao cha NEC. Alisema kuwa CCM inapoingia katika mazogo, watu wengi wanapata tabu na kwamba wajumbe hao wana wajibu wa kujipanga upya ili kurejesha matumaini kwa wananchi. Rais Kikwete ambaye alikuwa akifungua kikao hicho ambacho ni cha kwanza tangu baada ya kukamilika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, alisema ni mkutano wa historia na kwamba baada ya majadiliano ya kikao cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika Ijumaa na juzi ni lazima wajipange ili kusogeza chama hicho mbele. Katika kikao cha CC Sekretarieti nzima ya NEC chini ya mwenyekiti wake ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, ilitangaza kujiuzulu pamoja na Kamati Kuu isipokuwa Rais Kikwete; Makamu wa Mwenyekiti Bara, Pius Msekwa; Makamu Mweyekiti Zanzibar, Amani Abeid Karume na wajumbe wanaoingia kwa nyadhifa zao kama, Marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa; Spika wa Bunge, Anne Makinda na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Ameir Pandu Kificho; Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Bilal; Waziri Mkuu, Mizengo Pinda; Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seid Ali Iddi; na mjumbe wa kudumu wa CC, John Malecela. “Ninategemea ushirikiano tusome mazingira tuliyonayo tujipange ili kusogeza mbele chama chetu,” alisema Rais Kikwete na kuongeza kuwa anategemea ushirikiano kutoka kwa wajumbe wa NEC.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment