Thursday, April 14, 2011

CAG alalamika kupuuzwa na Serikali

SERIKALI haikutekeleza mapendekezo yote 15 yaliyotolewa na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) mwaka 2010, hali aliyoieleza kuwa inakwamisha ufanisi serikalini na katika mashirika ya umma.

CAG amelalamikia hatua hiyo ya Serikali katika ripoti yake ya mwaka 2010, iliyotolewa wiki hii na kuorodhesha mapendekezo yote aliyotoa huku akionya kuwa kudharauliwa kwake, kutasababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo.

Baadhi ya mapendekezo aliyosema hayakufanyiwa kazi ni pamoja na ushauri wa kuitaka Serikali ipunguze ununuzi wa magari ya kifahari na kupunguza gharama za warsha, ili mapato yanayokusanywa yatumike kwenye shughuli za maendeleo.

Pia alilalamikia kutotekelezwa kwa mapendekezo ya kuondoa wabunge kuwa wajumbe wa bodi za wakurugenzi wa mashirika ya umma, ili kuepuka mgongano wa maslahi kwa kuwa ni wabunge hao hao wanaosimamia utendaji kazi za mashirika hayo kupitia Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC).

Mapendekezo mengine aliyolalamikia kutotekelezwa na Serikali ni kuboresha ukusanyaji mapato kutoka vyanzo mbalimbali, kuziba mianya ya ukwepaji kodi hususani kwenye mafuta ya magari na mitambo, kupunguza misamaha ya kodi na kupanua wigo wa kodi.

CAG alisema katika ripoti hiyo, kuwa hata alipoomba maelezo ya kina kuhusu uhalali wa malipo ya dola milioni 4.8 za Marekani kwa kampuni ya M/s Dowans kwa ajili ya kukodisha ndege maalumu, Serikali haikumpa majibu yoyote sasa yapata mwaka.

Mbali na maombi ya kupata taarifa za Dowans ambayo hayajatekelezwa, CAG alilalamikia pia ushauri wake wa Serikali kuligawa mara mbili Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania (TPDC); shirika moja lishughulikie biashara na lingine litoe leseni, ukaguzi na kufanya kazi za udhibiti, ili kuleta ufanisi katika biashara ya mafuta, haukutekelezwa.

Mapendekezo mengine aliyosema yalipuuzwa ni kuruhusu Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC), kusimamia hesabu za mashirika na kampuni zote ambazo Serikali ina hisa.

Mkaguzi huyo pia alipendekeza bodi za wakurugenzi za mashirika ya umma kuhakikisha watendaji wakuu wa mashirika hayo wanawajibika zaidi kwa matokeo ya utendaji kazi wao, lakini alieleza kuwa ushauri huo haujatekelezwa.

No comments: