Tuesday, April 5, 2011

Bunge kusikiliza maoni ya wakazi wa Dar, Dodoma kuhusu Katiba

Wakati Mkutano wa Tatu wa Bunge unanza leo, wananchi wa mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma, watapata nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi kuanzia Alhamisi hadi Jumamosi wiki hii. Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Mawasiliano ya Umma wa Bunge, Jossey Mwakasyuka, alisema jana mjini hapa na kuwataka wananchi wa mikoa hiyo kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao. “Huu ni muswada muhimu sana, wananchi wanatakiwa kutoa maoni yao kwa kadiri watakavyoweza kuijitokeza…tunatoa nafasi kwa watu wengi zaidi kutoa maoni yao,” alisema. Alisema kwa kuwa Alhamisi ni ya mapumziko, yaani ni Siku ya kumbukumbuku ya kifo cha Karume, imeamuliwa iwe ni siku ya kupokea maoni ya wananchi kuhusu muswada huo. Alisema kama wananchi wengi watakuwa bado kutoa maoni yao kwa siku hiyo ya Alhamisi, wataendelea tena kwa siku ya Ijumaa na Jumamosi. Alisema wajumbe wa Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala ya Bunge watagawanyika makundi mawili ili kupokea maoni hayo kwa mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma. Mwakasyuka alisema Muswada huo wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Nchi unatarajiwa kuwasilishwa bungeni Aprili 18 na kujadiliwa hadi kesho yake. Katika hatua nyingine alisema Muswada wa Sheria ya Manunuzi ya Umma wa Mwaka 2011 unatarajiwa kuwasilishwa bungeni Aprili 15, mwaka huu baada ya kipindi cha maswali na majibu. Katika mkutano huu wa tatu, jumla ya maswali 145 yanatarajiwa kuulizwa na kupatiwa majibu.

No comments: