CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetoa miezi mitatu kwa wanachama wa chama hicho wanaotuhumiwa kwa rushwa na ufisadi wajiuzulu, wakikaidi watawajibishwa.
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, amesema, wanaCCM hao wakiwemo vigogo wanapoteza haiba ya CCM katika macho ya Watanzania.
Kwa muda mrefu, wanachama kadhaa wa CCM wamekuwa wakitajwa kuhusika katika vitendo vya rushwa na wakahusishwa kwenye kashfa kadhaa ikiwemo ya uzalishaji wa umeme wa dharura ya kampuni hewa ya Richmond, kashfa ya Dowans, kashfa ya ununuzi wa rada, na kashfa ya ulipaji wa madeni ya nje kupitia akaunti ya EPA Benki kuu Tanzania (BOT) kupitia kampuni ya Kagoda.
Kwa mujibu wa Kikwete, Halmashauri Kuu ya CCM imezungumza na watuhumiwa hao wakati wa mkutano uliomalizika jana usiku mjini Dodoma, na wameelewana.
“Tusionekane kuwa ni chama ambacho vitendo vya rushwa hatuchukizwi navyo” amesema Kikwete wakati anafunga mkutano huo wa Halmashauri Kuu ya Taifa CCM ulioanza juzi asubuhi.
Amesema, CCM imeanza kuchukua hatua, wanaotajwa kuhusika kwenye ufisadi na rushwa wanafahamika, hivyo wasionewe haya, wao wenyewe wawajibike, wasipofanya hivyo ‘wataoneshwa ulipo mlango’.
Katibu mpya wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amesema, chama hicho kimeamua kuwashughulikia WanaCCM wala rushwa na mafisadi.
“Haogopwi mtu, na Mwenyekiti alisema, tumekusudia, tunakwenda kujivua gamba” alisema Nnauye jana usiku wakati anazungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Halmashauri Kuu kwenye jengo la White House mjini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, John Chiligati amesema, watuhumiwa hao wanapaswa kujiuzulu kwa kuwa wanatajwa vibaya kwenye jamii, hivyo wawajibike hata kama hakuna ushahidi.
“Tumewaambia wao wenyewe wapime, wachukue hatua za kuwajibika” amesema na kubainisha kuwa wasipotekeleza waliyokubaliana, CCM itawawajibisha hivyo wasisubiri kuoneshwa ulipo mlango.
Chiligati amewaambia waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa, kuanzia sasa, CCM ipo makini kupambana na vitendo vinavyoleta sura mbaya katika chama hicho na amewaambia watuhumiwa kuwa “ usiulize ushahidi upo wapi”
Kikwete ameishukuru iliyokuwa Kamati Kuu ya CCM kwa kukubali kujiuzulu kwa maslahi ya chama hicho kwa kuwa wameonesha wanajali maslahi ya wanachama.
Ameishukuru Kamati Kuu mpya yenye wazee na vijana wasiozidi umri wa miaka 35, na ameishukuru pia iliyokuwa Sekretarieti ya CCM iliyojiuzulu kwa ujasiri wao na kujali maslahi ya chama chao.
Kikwete amesema, anaamini kwamba, Kamati Kuu mpya itakidhi matarajio ya kuijenga upya CCM, na amesema, kuwa miongoni mwa wajumbe ni wakongwe, wawe kama panga la zamani, makali yale yale.
“Tumekubaliana, mwenzetu anayelegalega tunamwambia, mwenzetu unalegalega” amesema Kikwete akimaanisha kuwa, kuanzia sasa hakuna kuoneana haya CCM.
No comments:
Post a Comment