Wednesday, April 6, 2011

Dk. Migiro ashauri Ukimwi uwe ajenda ya kisiasa

NAIBU Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro amesema suala la kupambana na maambukizi ya Ukimwi linatakiwa liwe ajenda ya kisiasa ili kuwa na msukumo mpya wa kupunguza maambukizi hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Dk. Migiro alisema, kwa miongo mitatu sasa, kumekuwa na jitihada nyingi zinazofanywa duniani katika kupambana na maambukizi ya Ukimwi, lakini idadi ya wagonjwa katika kipindi hicho ilifikia milioni 60 huku milioni 25 kati ya hao walipoteza maisha.

Alisema jana kuwa, maambukizi mapya yalipungua kwa asilimia 20 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita na akaeleza kuwa licha ya kuwa hiyo ni hatua nzuri, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya.

“Kwa kila mtu anayeanza tiba ya maambukizi ya Ukimwi, wawili zaidi wanapata maambukizi mapya, hivyo rasilimali zinatumika zaidi na hivyo fedha zinazotengwa kutotosheleza kugharimia wagonjwa wote kupata tiba,” alisema Dk. Migiro aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania.

Alisema, ndiyo maana anaona suala hilo la kupambana na Ukimwi liwe sehemu ya ajenda za kisiasa na liwekwe zaidi katika mipango ya maendeleo ya kiafya. Pia alisema kunatakiwa juhudi zinazofanywa sasa za kupambana na Ukimwi ziwe endelevu na za muda mrefu.

Alisema, katika hali hiyo, UN imekuja na malengo ya kuwa na maambukizi sifuri, unyanyapaa sifuri na vifo sifuri ambavyo lengo lake ni kupunguza nusu ya maambukizi, vifo na unyanyapaa ifikapo mwaka 2015. “Sifuri tatu hizi zitakuwa na manufaa kwa walioambukizwa mtu mmoja mmoja na dunia nzima,” alisema.

Mkurugenzi wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Kupambana na Ukimwi (UNAIDS), Michel Sidibe alisema licha ya kuwapo juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau kwa kuwapatia dawa za kupunguza makali wagonjwa, lakini sio wagonjwa wote wanaopata dawa hizo.

Alitoa mfano kuwa ni asilimia 70 tu ya wajawazito ambao wameambukizwa Virusi vya Ukimwi nchini ndio wanapata ARV’s na ni asilimia 52 ya wagonjwa wa Ukimwi ndio wanaopata dawa hizo kuanzia mwaka 2004.

“Tumepiga hatua, lakini bado kuna kazi kubwa ya kufanya ya kuzuia, kutibu na kuwajali hawa ambao tayari wameambukiziwa,” alieleza Sidibe.

No comments: