-Mbowe asema hana mahusiano na watuhumiwa
WAKATI watuhumiwa wa ufisadi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wakielezwa kuwa wanajipanga kupinga uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa kuwataka wajiuzulu au watimuliwe, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimekana kutumika kuwabeba watuhumiwa hao.
Watuhumiwa ambao sasa wanaelezwa kujipanga kupinga hadharani maamuzi hayo ya NEC kwa maelezo kwamba hicho si kikao kilichowachagua, ni Andrew Chenge na Rostam Aziz, ambao tayari wameenguliwa katika Kamati Kuu lakini wakabaki na nafasi nyinginezo ikiwamo ujumbe wa NEC; na Edward Lowassa ambaye pia ni Mjumbe wa NEC.
Taarifa zinasema ukiacha mkakati wao binafsi, kuna uwezekano kuwa watatumia ‘vinywa’ vya baadhi ya taasisi zenye mafungamano na dini, baadhi ya waandishi wa habari na viongozi kadhaa vyama vya siasa ndani na nje ya CCM.
Habari zinaeleza kwamba sikukuu ya Pasaka inayoanza wiki hii inatarajiwa kutumika kufanya vikao maalumu mkoani Arusha, ambako watu kadhaa wamealikwa kushiriki.
“Sasa mstari wa mapambano umechorwa, ni mpambano upande wa wanaotakiwa kung’oka dhidi ya wale wanaoshinikiza uamuzi wa NEC wa kuwang’oa utekelezwe,” kinaeleza chanzo chetu cha habari.
Taarifa zinasema katika moja ya sura za mkakati huo, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dk. Wilbroad Slaa, anatajwa kutumiwa bila kujua na baadhi ya viongozi wenzake ndani ya CHADEMA, walio karibu na Lowassa, kutekeleza malengo ya watuhumiwa hao wa CCM.
Tuhuma za kutumiwa kwa Dk. Slaa na CHADEMA zimekwishakuanza kuwekwa hadharani na viongozi wapya wa CCM, akiwamo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa NEC ya chama hicho, Nape Nnauye, ambaye katika mkutano uliofanyika viwanja vya Mwembe-Kisonge Zanzibar, mwanzoni mwa wiki, alisema mkakati huo wa watuhumiwa unahusisha baadhi ya vyama vya siasa, magazeti na asasi za dini kujibu mapigo.
“Tumewapa miezi mitatu watuhumiwa wote wa ufisadi katika chama chetu wajiondoe wenyewe. Baadhi wanajaribu kupinga na kujibu mapigo kwa kutumia magazeti, vyama vya siasa na taasisi za dini...tunajua tutashinda na wao lazima waondoke.
“Tumeandaa mkakati wa kusafisha chama kutoka ngazi za chini mpaka katika ngazi ya Taifa. Tumechunguza na tunajua wanaotakiwa kuondoka ndani ya chama chetu. Lakini baadhi ya watu wamejitokeza kutaja majina ya watuhumiwa ndani ya chama chetu; hiyo si kazi yao,”alisema Nape.
Hayo yakiendelea, taarifa zaidi zinaeleza kuwa watuhumiwa hao wanatarajia kuitisha mkutano na waandishi wa habari kueleza sababu za kutokukubaliana na uamuzi wa NEC.
Akizungumzia tuhuma hizo, Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe, alisema chama chake hakina uhusiano wowote na mafisadi na hakina mpango wa kushirikiana nao.
“Huo ni umbea wenye lengo na dhamira chafu ya kuvuruga CHADEMA. Ni wajibu wetu kuibua mafisadi kwa kadiri tunavyopata ushahidi. Tulianza 2007 na tutaendelea kwa awamu,” alisema na kuendelea:
“Binafsi sijawahi kuwa na uhusiano na mtuhumiwa yeyote wa ufisadi zaidi ya uhusiano wa shughuli za Bunge.”
Taarifa hizo zinabainisha kuwa mkutano huo na wanahabari ni sehemu ya mkakati ambao umetanguliwa na mikutano ya baadhi ya vyama vya siasa kuwataja viongozi wengine wa CCM kuwa ni mafisadi ili kuongeza wigo wa watuhumiwa.
“Kutokana na kazi ya utangulizi ya baadhi ya vyama vya siasa, hasa kimojawapo kilichojizolea umaarufu siku za karibuni kwa kuwataja mafisadi wapya, watuhumiwa hao sasa watafanya press conference kueleza kuwa si wao pekee wanaotajwa kuwa mafisadi, kwa hiyo ama wabaki ndani ya chama au kama wanaondoka waondoke na wengine wanaotajwa,” anaeleza mwananchi mmoja anayejitambulisha kwa jina la Fareed akiwasilisha mawazo yake katika mtandao.
Kwa mujibu wa mwananchi huyo, mbali na CHADEMA, vyama vingine vinavyotajwa kuhusishwa kwenye mkakati huo ni CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, TLP na DP.
“Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, ameingizwa mkenge na wanasiasa wenzake kuitoa orodha mpya ya mafisadi, bila kujua kuwa mpango huo umepikwa.
“Wafuasi wa watuhumiwa hao kwa kutumia watu wa CHADEMA ambao wako nao karibu wamemuingiza mkenge Dk. Slaa aitoe list of shame (orodha ya fedheha) mpya ili kuleta mvurugano ndani ya CCM.
“Siyo coincidence hata kidogo kuwa CHADEMA waliibuka na orodha yenye majina mapya siku chache tu baada ya CCM kuwataka kina Rostam, Lowassa na Chenge wajiuzulu.
“Inaeleweka wazi kuwa Rostam na Lowassa wako karibu sana na baadhi ya viongozi wakuu wa vyama vya upinzani na wamekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara nao.
"Wanachotaka kufanya ni kuibua tuhuma mpya za uongo dhidi ya Kikwete, Magufuli, Malecela, Sitta, Mwakyembe, Sumaye na viongozi wengine wa CCM wajitetee kwenye vikao vya NEC vijavyo kwa kusema kuwa mbona kuna viongozi wengine CCM wenye tuhuma, lakini wanatakiwa wajiuzulu wao tu," anasema mwananchi huyo akinukuu wapambe wa watuhumiwa.
Katika hatua nyingine, inaelezwa kuwa Sekretariati ya CCM imekwisha kuandaa barua kuwataarifu watuhumiwa hao kujiuzulu kama ambavyo uamuzi wa NEC unavyotaka.
Kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, katika barua watakazoandikiwa hawatapewa nafasi ya kuzijibu isipokuwa kutaarifiwa rasmi kuhusu uamuzi wa NEC.
Nape anasema viongozi waliotajwa ni sehemu ya wajumbe wa NEC ambao walikuwamo katika kikao kilichofikia uamuzi huo na kwa hiyo walikubaliana na uamuzi wa kikao.
Katika mikutano kadhaa iliyokwisha kufanyika mara baada ya hatua ya wiki iliyopita ya kile kilichoitwa “kujivua gamba” mjini Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa, amekwisha kuweka bayana kuwa chama hicho kilifanya makosa katika kujisimamia na kuonekana ni chama cha wafanyabiashara na hivyo kupoteza sifa ya kuwa chama cha wanyonge.
Akizungumza wiki hii mjini Zanzibar, Nape kwa upande wake alisema uamuzi wa chama hicho kuwapa miezi mitatu wajumbe wa NEC wanaotuhumiwa kwa ufisadi, hauna maana ya kuwaogopa bali ni utaratibu uliowekwa.
“Msiwe na wasiwasi; ni kama kumvua pweza baharini, akifika nchi kavu unamtandika mikwaju kisha mnampika baada ya kulainika na ndivyo tafsiri ya muda waliopewa,” alisema Nape.
Nape alikilinganisha na kitendo cha kujivua gamba kwa CCM na kuwasha mwenge unaomulika kwenye chuki, pasipo na matumaini, pasipokuwa na nidhamu na kupaweka sawa na kwamba mwenge huo hautazimika.
Lakini akizungumzia jinsi watuhumiwa hao wanavyojihami Nape alisema:
“Tunazo taarifa kwamba baadhi ya watu waliotoswa katika chama chetu wameanza kutumia magazeti. Tunawaambia hawatashinda vita hiyo; CCM ni chama kikubwa na makini.”
Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati, amewataka wanachama wanaojiona wamechafuka ama kwa tuhuma za ufisadi kuanzia ngazi ya matawi, majimbo, wilaya, mikoa na kwenye NEC wajiondoe kwenye nyadhifa zao.
Chiligati alisema anawashangaa wanaobeza uamuzi wa NEC kujiuzulu kuwa wajaribu katika vyama vyao, kama havikusambaratika, kwani ni uamuzi mgumu ambao CCM iliuchukua na imevuka salama.
“Kuachia ngazi ni jambo gumu sana na si la kubeza hata kidogo; tumelazimika kujiuzulu kukinusuru chama, ingelikuwa vile vyama vingine mngevisikia vimesambaratika … wajaribu waone,” alisema Chiligati.
Kwa upande wake Msekwa, mbali ya kuelezea historia ya “kujivua gamba” kwa chama hicho, alielezea mpango mkakati wa CCM katika kujenga chama kipya chenye matumaini kwa Watanzania.
No comments:
Post a Comment