Wednesday, April 6, 2011
John Mnyika aihoji serikali kuhusu Kagoda
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika,(Chedema) amehoji uchunguzi dhidi ya kampuni ya Kagoda inayodaiwa kuchota mabilioni ya fedha za Malipo ya Madeni ya Akaunti ya Nje (EPA), umefikia hatua gani. Katika swali lake la nyongeza kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, (Utawala Bora), Mathias Chikawe, Mnyika alitaka kujua serikali imechukua hatua gani katika uchunguzi wa suala hilo. Lakini katika majibu yake, Waziri Chikawe alisema kwa kifupi kuwa uchunguzi dhidi ya kampuni hiyo bado unaendelea. “Serikali tunasema bado tunaendelea na uchunguzi na ukikamilika tutachukua hatua,” alisema. Hata hivyo, katika swali lake la nyongeza, Hamad Rashid (CUF Wawi) alisema kesi za uchunguzi zipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), na akaitaka serikali kuwasilisha bungeni taarifa za kesi zilizofanyiwa uchunguzi ambazo zipo kwa DPP. Akijibu Chikawe alikubaliana na mbunge na akasema serikali itawasilisha taarifa za kesi hizo bungeni. Katika swali lake la msingi, Pudenciana Kikwembe (Viti Maalum), alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba lengo la taifa katika kupambana na rushwa linafikiwa. Chikawe alisema katika kuhakikisha lengo hilo, linafikiwa. Serikali ilipitisha sheria mbalimbali ambazo hasa ndiyo msingi wa mapambano dhidi ya rushwa. Pia alisema kupitia mkakati wa taifa dhidi ya rushwa na utaratibu wa Public Expenditure Tracking System (PETS), serikali imeanzisha mafunzo dhidi ya rushwa na miundombinu ya maadili kwa watumishi wa serikali na taasisi zisizo za kiserikali, ili kuhakikisha kuwa watumishi wanazingatia maadili katika kutoa huduma kwa wananchi. Aliwaomba viongozi wote wa serikali, wa siasa, wa dini na wa jamii kwa ujumla, kukemea rushwa kila wanapopata nafasi ya kufanya hivyo kwani rushwa ni adui wa haki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment