Tuesday, April 19, 2011

Waliohojiwa Baraza la Maadili kutimuliwa

BARAZA la Maadili ya Viongozi wa Umma, limesema viongozi wa umma takribani 23 waliosimamishwa mbele yake kuhojiwa juu ya kutowasilisha matamko yao kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, baada ya kuamua na kumshauri Rais, huenda wakakosa sifa ya kuwa viongozi.

Pia Baraza hilo limesisitiza kuwa kazi yake si tu kufuatilia ujazaji wa matamko ya mali na madeni ya viongozi wa umma bali kusimamia maadili ya viongozi hao na kuhakikisha kila kiongozi anazingatia maadili hayo.

Pamoja na hayo, Baraza hilo jana lilihoji na kusikiliza maelezo ya viongozi wawili wa umma ambao ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala na Msaidizi wa Masuala ya Siasa wa Rais, Rajab Luhwavi, ambaye wiki iliyopita alifikishwa mbele ya Baraza hilo chini ya ulinzi wa Polisi.

Akitoa majumuisho ya kazi ya Baraza hilo ya kuhoji viongozi wa umma 23, ambao wanalalamikiwa na Sekretarieti ya Maadili kwa kutowasilisha matamko yao, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema Baraza hilo limekamilisha awamu ya kwanza ya kusikiliza maelezo ya viongozi wa umma wasiowasilisha matamko yao kwa Sekretarieti ya Maadili ambao wasipoangalia wanaweza kupoteza uongozi.

“Napenda ifahamike kuwa Baraza hili kazi yake si kushughulikia kutojaza fomu za matamko ya mali na madeni ya viongozi, tunazo kazi nyingi za kushughulikia za uvunjifu wa maadili na hawa tunawahoji, inawezekana wakakosa sifa za kuwa viongozi lakini kwa sasa tutazingatia utetezi wao na kumshauri aliyetutuma kwa hatua zaidi,” alisema Lubuva.

Aidha, alisema viongozi wengi waliohojiwa na Baraza hilo wametumia utetezi wa kutotumiwa barua na fomu za matamko na Sekretarieti ya Maadili, jambo ambalo si utetezi unaokubalika, kwa kuwa Sheria ya Maadili namba 13 ya mwaka 1995 inatamka wazi kuwa ni wajibu wa kiongozi kujaza yeye binafsi fomu hizo na kuziwasilisha kwa Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma.

Pia alivitaka vyombo au taasisi kama vile halmashauri za wilaya ambazo hupokea barua na fomu za viongozi wa umma, kwa jumla na kuwasambazia, kuhakikisha kuwa kila kiongozi amepata fomu yake, kujaza na kuirudisha, vinginevyo lawama za kutojaza fomu zinaweza
kuangukia vyombo au taasisi hizo.

“Tumekutana na kesi za aina hiyo katika mashauri tuliyosikiliza, ndiyo maana tunasema tutazingatia kesi kwa kesi na mazingira yake, lakini suala la kujaza hizi fomu, ieleweke kuwa ni wajibu wa viongozi wenyewe kwa kuwa wao ndio waliapa na kuahidi kuwajibika,” alisema.

Awali Mukandala akijijitea mbele ya jopo la Baraza hilo lenye majaji watatu; Lubuva, Jaji mstaafu Balozi Hamis Msumi na Katibu Mkuu mstaafu Deodatus Tibakweitira, alisema tangu ashike wadhifa huo wa Makamu Mkuu wa Chuo, hajawahi kutojaza fomu na kwamba mwaka anaodaiwa kutojaza wa 2009, ana uhakika alijaza na kuziwasilisha kunakotakiwa.

Alitoa kielelezo cha kuthibitisha kujaza na kuwasilisha fomu hizo kwa Sekretarieti ya Maadili ambacho ni barua ya sekretarieti hiyo, ya kumjulisha kupokea fomu zake ya Agosti 6, mwaka jana, na kumtaarifu kuwa watamfanyia uhakiki wa mali na madeni yake kwa mujibu wa tamko lake la mwaka 2009 ambalo anadaiwa hajawasilisha.

Mwanasheria wa Sekterieti ya Maadili, Hassan Mayunga, alidai mbele ya Baraza hilo kuwa barua aliyotumiwa Mukandala ilikosewa kimaandishi, kwa kuwa uhakiki hufanywa kwa baadhi ya viongozi na hutumiwa barua moja ambayo hubadilishwa majina na anuani tu.

Hata hivyo, timu hiyo ya mawakili pia iliendelea kudai kuwa hata tamko la mwaka 2009 alilowasilisha Mukandala baada ya kutakiwa kufanya hivyo na timu ya uhakiki kufuatia tamko lake la awali kutoonekana, nalo linaonekana kuwa na utata kutokana na tarehe ya kiapo kuwa Januari 2010 wakati tamko hilo liliwasilishwa Aprili mosi mwaka huu.

Luhwavi katika utetezi wake, alidai mbele ya jopo hilo kuwa tangu kushika kwake wadhifa wa Naibu Msaidizi wa Masuala ya Siasa wa Rais, hajawahi kupelekewa barua wala fomu za kujaza na kwamba aliwahi kufuatilia Sekretarieti ya Maadili ambao walimjibu kuwa kama yumo kwenye orodha ya viongozi wa umma, atatumiwa taarifa.

2 comments:

Anonymous said...

Huu wote ni usanii unaoendelea, ionekane serikali inafanya kazi. Hakuna chochote kitakachofuata! Uzoefu unaonesha. Sheria ya maadili haijatungwa leo hii. Kila siku ahadi kibao, hakuna kinachofanyika. Waswahili husema "maneno matupu hayavunji mfupa"! Tunataka vitendo

Anonymous said...

KWA KUHOJIWA HAO VIONGOZI NI VIZURI LAKINI MI NAJIULIZA KWA NINI WATU KAMA,MRAMBA AMBAYE ANA HOTEL DAR HAJAOJIWA,AKINA LOWASA,CHENGE NA WENGINE WENGI MBONA HIYO TUME HATUJASIKIA IKIWAOJI KWANI NI VIONGOZI WENGI TU AMBAO WANAENDA KINYUME NA KIAPO CHA AJIRA YAO,JARIBU KUANGALIA POLIS,JESHI,MAGEREZA,UHAMIAJI,MAHAKAMA,NI WAFANYAKAZI WENGI TU WENYE UTAJIRI MKUBWA HUSUSANI MAJUMBA NA MAGARI,HIVYO TUME IANGALIE KWA MAKINI.