HIVI karibuni Tanzania iliungana na nchi nyingi duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.
Tanzania iliadhimisha wiki hiyo, kwa kwa kufanya matukio mbalimbali kama vile midahalo, kongamano na maandamano.
Moja ya matukio yaliyofanyika siku hiyo ni utoaji wa Tuzo kwa wanawake waliofanya vema katika tasnia mbalimbali.
Tuzo hizo zinalenga kuwahamasisha akinamama hao kufanya mambo makubwa zaidi ili waweze kuisaidia jamii inayowazunguka.
Pia tuzo hiyo inaonesha ni kwa jinsi gani wanajamii wanatambua mchango wa akina mama katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Tuzo hizo zilianzishwa na Kampuni ya Uhusiano ya Fornt Line Management, ambapo Mkurugenzi Mtendaji, Hellen Kiwia, anasema kuwa mwaka huu tuzo hiyo imeshirikisha vipengele 10.
Akifafanua zaidi Hellen anasema huu ni mwaka wa pili mfululizo, kwa kampuni yake kutoa tuzo hizo na imeweza kuwanufaisha wanawake wengi zaidi.
Hellen anasema tuzo hiyo ilianzishwa, kutokana na nia yake ya muda mrefu ya kuwasaidia wanawake pindi atakapokuwa mwanasiasa.
Anasema ndoto hizo za kuwa mwanasiasa, zilififia baada ya kupata kazi ya utangazaji katika kituo cha East African TV kwa mwaka mmoja kuanzia 2002 hadi 2003.
Akiwa huko alipata mwanga kuwa kupitia vyombo vya habari, vinaweza kuwafikia wanawake nchi nzima.
Hellen baada ya kuacha kazi katika kituo hicho na kuhitimu shahada ya uhusiano wa kimataifa katika Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, alianzisha Kampuni ya Front Line Management na alijikuta akiwa tena karibu zaidi na vyombo vya habari kiutendaji.
Alitimiza ndoto hiyo ya kuwasaidia wanawake mwaka 2010 ambapo ndipo alitoa tuzo ya kwanza ya kutambua mchango wa mwanamke.
Mwaka huu amefanikisha ndoto hiyo kwa mara ya pili, ambapo kupitia kampuni hiyo ametoa tuzo kwa wanawake wengine katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Akizungumzia uamuzi wake wa kuwafikia wanawake kwa njia ya utoaji Tuzo, anasema Tuzo hizo zinawapa mwanga wanawake hao kujiinua zaidi katika shughuli wanazofanya.
Anasema kuwa Tuzo hizo, zina nia ya kutambua mchango wa mwanamke katika jamii, kulingana na nia na malengo ya shughuli yake.
Anasema kuwa wanawake walipata tuzo hizo, wanaweza kuzitumia kama njia ya kupata mafanikio zaidi, kwa kuwa wanadhihirisha ni kwa jinsi gani mchango wao unatambulika.
“ Mimi niliamua kuwafikia wanawake wengi kwa njia hii, ikiwa ni mkakati wangu wa kuhakikisha kuwa nawafikia na kuwainua wanawake nchini. Tuzo ni moja kati ya njia pekee ya kuwasaidia akina mama hawa”, anasema Hellen.
Anasema kuwa ili mwanamke kutunukiwa Tuzo hiyo, anatakiwa awe ana mchango katika jamii inayomzunguka. Mchango huo sio lazima uwe wa mamilioni ya fedha, lakini hata kwa kutoa chochote kile chenye manufaa kwa jamii inayomzunguka.
“Binafsi naamini kuwa msaada kwa mtu yeyote katika jamii, huwa sio lazima fedha peke yake, ila hata ujuzi wa kitu fulani unaweza kuwa msaada tosha”, anasema Hellen.
Anaongeza kuwa wapo watu wanaoweza kusaidia jamii inayowazunguka kwa kuwapatia elimu au hata mazingira bora ya kujifunzia kitu fulani, nao huu ni msaada pia.
Wanawake waliopata tuzo mwaka huu ni pamoja na Oliver Lyamuya, aliyepewa Tuzo ya Multichoice Arts and Culture.
Pia kulikuwa na Tuzo ya Kilimo ya RBP, ambayo alishinda Asia Kipande Tuzo ya mwanamke chipukizi mwenye mafanikio, iliyotolewa na American People ilienda kwa Modesta Mahiga huku Mwamvita Makamba, akipata tuzo ya taaluma kutoka kwa kinywaji cha Bailey.
Tuzo ya mwanamke mwenye mchango katika michezo, ilienda kwa Rahma Al Kharoos, huku tuzo ya Sayansi na Teknolojia iliyotolewa na Kampuni ya Songas, ilienda kwa Mary Mwanukuzi.
Hellen anasema akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayotoa tuzo hizo, hahusiki kwa namna yoyote ile na uchaguzi wa wanaozipata, kwa kuwa zinaratibiwa na Kampuni ya Delloite, ambayo ina wajumbe maalumu wa kufuatilia tuzo hizo.
Kwa mwaka huu, mwanamke wa mwaka ambaye amepata tuzo bora kuliko wengine ni – Marina Njelekela, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Madaktari Wanawake Nchini (Mewata). Yeye alishinda kupitia Tuzo ya Afya, iliyotolewa na Deloitte.
Mwanaharakati na mwanahabari wa muda mrefu nchini, Ananilea Nkya, alipata Tuzo ya Teknolojia na Mawasiliano, iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Pia, kulikuwa na tuzo nyingi kama utumishi wa umma, aliyopata Margareta Chacha, Tuzo ya Biashara aliyopata Zainab Ansell, Tuzo ya Home Shopping Center aliyopata Khadija Mwanamboka na Tuzo ya Kutambua Mchango wa Mwanamke wa Muda Mrefu, aliyotunukiwa Dk. Maria Kamm.
No comments:
Post a Comment