Friday, April 1, 2011
Kashfa ya mabilioni kufikishwa Bungeni
WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanataka Bunge liingilie kati na lichunguze sababu za kupotea kwa mamilioni ya shilingi na hatimaye kufungwa kwa kiwanda cha matairi cha General Tyre East Africa Ltd cha Arusha, imefahamika. Wabunge hao, Zitto Kabwe wa Kigoma Kaskazini na Godbless Lema wa Arusha Mjini wanataka Bunge liunde Kamati Teule ya Bunge kufanikisha zoezi hilo. Katika nyakati tofauti wameiambia Raia Mwema ya kuwa ni hatua ya Bunge tu inayoweza kupata ukweli wa nini kilichokisibu kiwanda hicho kilichokuwa maarufu kwa utengenezaji matairi imara katika eneo lote la Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika. Zitto anasema ataitumia Kamati anayoingoza ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Lema anasema amepeleka hoja binafasi kwa Spika ili uchunguzi uanze. Zitto kupitia POAC amezuia Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kupiga mnada kiwanda hicho pekee kilichowahi kujipatia sifa Afrika kwa kuzalisha matairi bora na kilichokuwa kikiajiri mamia ya wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani. Kabla ya POAC kuingilia kati, NSSF ilipanga kuuza kiwanda hicho kufidia deni la dola za Marekani milioni 10 (15bn/-) huku kukiwa na taarifa kwamba tayari Halmashauri ya Manispaa ya Arusha ilikwishakupanga kugawa viwanja na sehemu ya eneo la kiwanda hicho kujengwa majengo ya kibiashara (shopping malls). Katika mahojiano na Raia Mwema wiki hii, Zitto alisema waliwaambia NSSF kwamba wakiamua kuuza kiwanda hicho, nchi haitakuwa na kiwanda cha matairi na hivyo kuendelea kuagiza kutoka nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na nchi jirani, na pia wananchi kupoteza ajira. “Tuliwambia NSSF ni shirika la umma na katika General Tyre Serikali ina hisa asilimia 76, tukawapiga ‘stop’. Hakuna kuuza na wala wasithubutu! Kamati yangu itaunda kamati ndogo kuchunguza mkopo uliotolewa ulifanya shughuli gani na kuona hatua za kuchukua,” anasema Zitto akizungumzia mpango ambao pia umo katika hoja ya Lema. “Pia tunataka kiwanda kifufuke. Tunaweza kuelekeza deni la NSSF ligeuzwe kuwa ‘equity’ (mtaji), apatikane mwekezaji na kiwanda kifufuliwe upya. Wakianza kupata faida NSSF watauza hisa zao na kutoka kwenye kampuni kama hawana ‘interest’. Ila kuuza mali ili kupata fedha zao tumewapiga marufuku,”aliongeza Zitto. Habari zaidi zinaeleza kwamba POAC jana Jumanne ilikuwa imepanga kupokea taarifa kutoka serikalini kuhusu General Tyre, huku kukiwa na taarifa kwamba msimamo wa serikali ni kutaka kuuzwa kwa kiwanda hicho. Zitto mwenyewe amethibitisha kuwapo kwa kikao hicho na kusema: “Ndiyo, tunakutana nao na wameleta taarifa kuhusu General Tyre na leo ndiyo tunaamua kuhusu kuunda kamati ndogo ya POAC. Msimamo wa Serikali pia ni kuifilisi kampuni hiyo na hivyo kuuza mali zake na kufunga kiwanda. Tutatengua msimamo huu leo na kuunda kamati ndogo ya kamati ya Bunge kuchunguza matumizi ya mkopo wa NSSF pale na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukua.” Uamuzi huo wa kamati ya Zitto ulikuja kufuatia maelezo ya Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Ramadhani Dau kuwa shirika lake limedai fedha hizo kwa muda mrefu lakini hakukuwa na juhudi zilizofanyika za kuhakikisha kuwa deni hilo linalipwa. Mkopo huo wa fedha ulitolewa kwa kiwanda hicho baada ya uzalishaji kudorora kati ya mwaka 1997-2005 na ulidhaminiwa na serikali ambayo ilikuwa na hisa nyingi katika kiwanda hicho. Serikali ilikuwa na asilimia 76 za hisa na kampuni ya Continental yenye makao makuu yake Hannover, Ujerumani ilikuwa asilimia 24 ya hisa na pamoja na wingi wa hisa zake hizo, Serikali haikuwa na madaraka yoyote katika timu ya menejimenti ya Genefral Tyre. Mkopo huo wa fedha uliidhinishwa na aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Zakia Meghji, baada ya mawasiliano ya kiserikali baina yake na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, na Waziri wa Viwanda na Biashara, Basil Mramba. Mawaziri hao wa zamani wanadaiwa kwa wakati huo walipuuza ushauri wa wataalamu wazalendo waliotaka kwanza pafanyike ukaguzi wa mahesabu kabla ya kuidhinisha mkopo. Raia Mwema imefanikiwa kuona sehemu ya mawasiliano ya kiserikali kati ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara za Fedha na Viwanda na Biashara, yote yakihimiza kutolewa kwa mkopo huo. Katika sehemu ya mawasiliano hayo ofisa katika Ofisi ya Waziri Mkuu anaandika kwenda Hazina kwenye barua yenye kumbukumbu namba PM/P/1/567/40 yenye kichwa cha habari “General Tyre East Africa Ltd,” kuwa ilikwishakuamuliwa kwamba kiwanda kipewe ‘government guarantee’ ili kulinda kiwanda na ajira za Watanzania na kama Waziri wa Fedha alikuwa na maoni tofauti basi ayapeleke mbele ya vikao, au vinginevyo atekeleze agizo hilo kabla ya tarehe 15/7/2007. Habari zinadai kuwa fedha hizo zilitolewa kutokana na kinachodaiwa kuwa “shinikizo” kubwa kutoka kwa viongozi hao ambao kwa wakati huo walikuwa wenye nguvu kimamlaka katika serikali ya awamu ya nne. Hata hivyo, katika mazingira yasiyoeleweka fedha hizo zinadaiwa kuyeyuka baada ya manejimenti iliyokuwa chini ya uongozi wa Devendra Lohani, raia wa Nepal kuzitumia vibaya na ndani ya miezi sita tu tangu kutolewa kwa mkopo huo kiwanda kilikwishakuwa taabani kikishindwa kujiendesha na kuzalisha matairi. Kwa upande wake hoja ya Lema imejikita zaidi juu ya madai hayo ya ufisadi, na anamtaka Spika wa Bunge Anne Makinda kuunda kamati teule kuchunguza ufisadi huo ili kuweka hadharani yaliyojiri nyuma ya pazia katika sakata hilo. Lema katika barua yake anataka Bunge liazimie kuunda kamati teule kwa ajili ya kuchunguza mchakato wa uendeshaji, ubinafsishaji na ufilisi wa kiwanda hicho chini ya kanuni ya 54 ya kanuni za Bunge toleo la mwaka 2007. Raia Mwema imefanikiwa kuona sehemu ya nyaraka za Lema akibainisha sababu za msingi za kuundwa kwa kamati teule kuwa ni pamoja na kupata taarifa kamili kuhusu mchakato mzima wa usimamizi na uendeshaji wa kiwanda hicho. Anataka pia ufanywe uchunguzi wa mali za kiwanda hicho ambazo mpaka sasa mustakabali wake haufahamiki na hauko wazi, kuchuguza kampuni iliyotoa ushauri wa kitaalamu na utaratibu uliofuatwa katika kuileta na hatua ya ushauri ya kampuni husika. Mbunge huyo pia anataka kamati teule itakayoundwa ichunguze ili kujua kampuni ya Continental ya Ujerumani ambayo ilikuwa mwanahisa mshirika wa Serikali iliwekeza mtaji wa kiasi gani tangu mwaka 1988 na pia ihakiki kama matumizi husika yalizingatia makubaliano. Lema pia anataka Kamati ya Bunge ichunguze ni jinsi gani kiasi cha dola za Marekani milioni 10 (shilingi Bilioni 15), fedha za mkopo, zilizotolewa na NSSF zilitumika kwa ajili ya kulipa madeni ya Benki ya Citi Bank na uendeshaji wa kiwanda na wachunguze pia kampuni au wataalamu waliohusika kupata mkopo wa NSSF. “Taarifa zinadai kuwa fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni 10 (wakati huo) zilitumika kulipa madeni ya benki ya Citi, ambayo hayafahamiki, badala ya kufufua kiwanda kama ilivyokuwa imeazimiwa awali….mpaka leo kiwanda hakifanyi kazi, kuna wafanyakazi wengi hawajaweza kulipwa mafao yao na kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi hao,” inaeleza sehemu ya maelezo ya Lema. Anaongeza Lema katika maelezo yake: “Nyaraka zinaonyehsa kuwa katika mkopo huo pia kiasi cha shilingi bilioni moja zilitumika kuilipa kampuni ya ukaguzi ya DAI Consulting ya Afrika ya Kusini. Kampuni hiyo ililipwa na NSSF kama malipo ya gharama za ushauri kwa General Tyre, malipo hayo ni fedha nyingi sana zikilinganishwa na kazi iliyofanyika.” Katika maoni yake, Lema anasema ya kuwa taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa kampuni ya matairi ya General Tyre haikuwa na njia nyingine kupinga malipo hayo kwa kuwa ilikuwa sehemu ya mkataba wa kupewa fedha hizo na NSSF na katika mazingira ya kushangaza DAI Consulting ilipewa kazi na NSSF wenyewe. Anaongeza Mbunge huyo: “Katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) ya mwaka 2007 kiwanda hicho kilikuwa kinadaiwa kiasi cha shilingi 13,817,191,814 mpaka Agusti 2005; hivyo ufafanuzi wa kina unahitajika kufahamu fedha zilizotolewa na Serikali kupitia NSSF zimekwenda wapi? Na kama zilitumika zilitumikaje?” Habari za kufa kwa General Tyre ni za muda mrefu; katika moja ya habari hizo Raia Mwema ilipata kuandika katika toleo lake la Agosti 5, mwaka 2009 (toleo namba 93) juu ya ufisadi uliofanywa na menejimenti ya kiwanda hicho na hasa meneja wake Devendra Lohani aliyekuwa anatuhumiwa kufuja fedha za mkopo wa NSSF badala ya kufufua kiwanda ili uzalishaji uanze. Baada ya kiwanda kupata fedha hizo menejimenti ililipa madeni katika benki kadhaa na kiasi cha shilingi bilioni 3.5 zilitumika bila idhini ya Bodi, nyingi zikiwa ni matumizi binafsi ya meneja huyo. Baadhi ya matumizi hayo ni pamoja na kuwaleta ndugu zake kutoka Nepal na mmoja wa wana wa mfalme wa nchi hiyo nchini kutembelea mbuga za wanyama za Serengeti, Ngorongoro na Manyara kwa gharama za kiwanda hicho. Mbunge Lema anahitimisha kuwa kuna manung’uniko mengi juu ya ufisadi mkubwa uliokuwa ukifanyika katika kiwanda hicho cha matairi, hivyo Serikali inapaswa kufuatilia kwa makini ili kuupata ukweli kwani watu wengi waliofanya kazi katika kiwanda hicho bado wako hai na wanaweza kuisadia kutoa taarifa kuhusu uhalifu huo. Lema anaeleza kuwa kiwanda hicho kilikuwa ni moja ya nguzo muhimu za uchumi wa mji wa Arusha na Serikali kwa ujumla, na kwamba pamoja na kuzalisha matairi kiwanda hicho kilikuwa chanzo cha ajira kwa wananchi zaidi ya 500 lakini pia mzunguko huo wa ajira haukuishia kiwandani tu bali hata katika mashamba ya zao la mpira katika Mikoa ya Tanga na Morogoro. Anasema kufungwa kwa kiwanda hicho kumekuwa ni chanzo cha matatizo mengi kwa wananchi wa kawaida wengi kuendelea kuwa masikini kutokana na ukosefu wa ajira na pia ajali nyingi za barabarani kutokana na viwango hafifu vya matiri ya kutoka nje ya nchi. Lema alipoulizwa mwishoni mwa wiki na Raia Mwema kwa njia simu alithibitisha kuwa ni kweli ameandaa nyaraka hizo na tayari alikuwa ameziwasilisha katika Ofisi ya Spika ili hoja hiyo ijadiliwe katika kikao cha Bunge cha mwezi ujao. “Ni kweli nimewasilisha hoja binafsi ya kumwomba Spika akubali kuundwa kwa kamati teule kuchunguza mchakato mzima wa uendeshaji, ubinafsishaji na ufisili wa kiwanda hicho…..nikikana jambo hilo nitakuwa mnafiki, na kawaida yangu siogopi kusema ukweli,” alisema Mbunge huyo. Aliongeza: “Ni matumaini yangu Spika atalichukulia jambo hilo kwa umakini mkubwa kutokana na suala hilo kugusa maslahi ya Watanzania wote na ni matumaini yangu pia kuwa kamati itakayoundwa itafichua mambo mengi ambayo kwa sasa yanahitaji majibu kwa wananchi”. Kufungwa kwa kiwanda cha General Tyre East Africa Ltd ni hitimisho la kuwapo kwa viwanda vya umma vilivyoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere kati ya miaka ya 1970 na 1980 na vingi vilibinafsishwa wakati wa uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu kwa bei ya kutupa kwa wawekezaji mbalimbali. Vingine vimetelekezwa, vikibakia kuwa magofu. Viwanda vilivyoufanya Mkoa wa Arusha kuwa moja ya mikoa iliyokuwa inaoongoza nchini kwa kuwa na uchumi mzuri ni pamoja na Kiwanda cha Bia ambacho kilinunuliwa na wawekezaji kutoka Afrika ya Kusini, Kiwanda cha madawa cha TPA, kiwanda cha kusindika nafaka cha NMC, kiwanda cha nguo cha Kiltex, kiwanda cha sabuni cha EMCO na kiwanda cha mbao cha Fibreboard. Ukiondoa Kiwanda cha Bia, vingine vyote vimeshindwa kufanya kazi kwa ufanisi unaotakiwa kutokana na wawekezaji waliopewa kutokuwa na uwezo na mitaji ya kutosha, huku vingine kama kiwanda cha nguo cha Kiltex kikiwa kimetelekezwa kabisa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment