KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye ametetea uamuzi wa chama hicho kuwaandikia barua watuhumiwa wa ufisadi.
Nnauye amesema, huo ni utaratibu wa kawaida wa chama hicho si lazima litolewe kama azimio kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Akizungumza na HABARILEO, Nape amesema, kama kuna jambo limejadiliwa ndani ya kikao cha chama na linamhusu mwanachama ili liwe la kiofisi ni lazima mhusika ajulishwe kwa barua.
“Suala la barua ambalo sasa linaonekana kuwa mjadala mkubwa sio big deal, hili ni jambo la kawaida kwamba kuna mambo yamejadiliwa na kufikiwa kwa maamuzi hivyo wahusika lazima wataarifiwe kwa barua,” amesema Nnauye ambaye kabla ya uteuzi wake, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi.
Ametoa mfano kuwa, hata alipoteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi licha ya kuwa alikuwemo kwenye kikao kilichotangazwa uamuzi huo, lakini aliandikiwa barua rasmi ya kutaarifiwa juu ya uteuzi huo.
“Hata Katibu Mkuu wetu pale alipo ana barua inayo mtaarifu juu ya uteuzi wake, haitoshi kumtangaza mbele ya vyombo vya habari halafu asipewe barua, hivyo hivyo maamuzi yanayohusu mwanachama mwingine ye yote awe na tuhuma kama hizo za ufisadi au mambo mengine lazima pia yawekwe kwenye maandishi na ataarifiwe,” amefafanua Nape.
Alitoa ufafanuzi huo baada ya kushutumiwa na baadhi ya makada wa CCM kuwa ndani ya NEC hakukuwa na azimio la watuhumiwa wa ufisadi kuandikiwa barua wala kupewa siku 90 za kujiondoa kwenye uongozi.
Wanaomshutumu wanadai kuwa anatoa matamshi kwa maslahi yake binafsi, lakini Nape alieleza kuwa wanachokisema majukwaani sio utashi wao, bali ni taratibu za chama hasa suala la barua na hilo la siku 90.
“Hili la barua wanalisema sana na lile la siku 90, hizo siku 90 kikatiba ni muda wa kufanyika kwa vikao vya NEC kutoka kimoja kwenda kingine, hivyo hiki tunachokisema hatukukitoa mbinguni kiko kwenye Katiba yetu. Sisi tumeziweka hivyo kwa kuwa kwenye kikao kijacho Sekeretarieti ni lazima tutoe taarifa ya yatokanayo na kikao kilichopita na mojawapo hilo suala la ufisadi,” alisema Nape.
“Hawa wamekosa hoja za kuzungumza, ni vyema wakaondoka kuliko kujadili na kupindisha mambo ambayo yako kwenye taratibu za chama,” alisema mwanasiasa huyo machachari.
No comments:
Post a Comment