Tuesday, April 12, 2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) P.O. Box 8921, Dar es Salaam, TANZANIA; Gender Resource Centre, Mabibo Road, Tel. 255 022 2443205/2443286/2443450; Mobile 255 0754 784050, 0715 784050; 0784 784050 Fax 255 022 2443244; Email info@tgnp.org ; web www.tgnp.org Aprili 11, 2011



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Uchambuzi wa madai ya wanaharakati kuhusu mchakato wa Muswada na Katiba Mpya ya Tanzania Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), tumekuwa tukifuatilia kwa karibu mchakato wa kutengeneza Katiba mpya ya Jamhuri wa Muungano Tanzania unaoendelea hapa nchini. Kwa muda mrefu sasa wananchi wamekuwa wakidai Katiba mpya ambayo itashirikisha mawazo ya walio wengi. Kwanza, tunaipongeza serikali kwa kuona kuwa wananchi wana mahitaji ya kuwa na Katiba mpya baada ya ile ya mwaka 1977 kutokukidhi haja za wakati huu na hivyo kuonekana kuwepo na mapungufu mengi. Tunasikitika kuona kwamba wakati tupo katika hatua za awali kabisa za kuujadili muswada huu, kumeibuka makundi ya wanasiasa wanaotumia mwanya huo kuvuruga utaratibu mzima wa kukusanya maoni ya wananchi. Ili Katiba iwe na uhalali wa kisiasa na mamlaka ya kusheria, wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kutunga Katiba mpya.Katika mchakato huu ni muhimu kuwemo na demokrasia na ushiriki wa wananchi wote wanawake, wanaume,vijana, watu wanaoishi na ulemavu na watu wote walioko pembezoni ili kuleta mabadiliko chanya na pia kuleta haki na usawa kwa wote. Tunajua kuwa kama wananchi watanyamazia au watashindwa kutoa maoni yao juu ya muswada huu, itakuwa mwanzo wa kuwa na Katiba isiyo ya wananchi wote. Tumesikitishwa na makundi ya wananchi wanaokubali kutumiwa vibaya kuzomea kwenye mikutano ya kujadili muswada huu na kuleta vurugu. Pia tunalaani kitendo cha wanasiasa kuwatumia vibaya watoto wadogo wasio na uelewa wa kuchangia muswada huu na kuwajaza katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es salaam Aprili 8,2011 na kusababisha wananchi wenye mapenzi mema na Taifa letu kukosa nafasi ya kuchangia kutokana na kukaa nje ya ukumbi.Tunalaani kitendo cha Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kutumia silaha na wakati mwingine kuwatishia wananchi waliojitokeza kutoa maoni yao na kuwanyima haki ya kiraia na haki ya kibinadamu, hasa matumuzi ya askari wengi waliotumika mjini Dodoma Aprili 7,2011 na kusababisha wananchi wengine kuogopa kujitokeza kutoa maoni Aprili 8,2011. Tunaitaka jamii ielewe kuwa tunatafuta Katiba ya wananchi kwa maslahi yetu sisi sote wananchi na sio ya wanasiasa au watawala kwa hiyo suala hili liachiwe wananchi walisimamie wenyewe kwa uhuru ili ipatikane Katiba itakayolinda maslahi ya wananchi wote na sio kundi dogo la wanasiasa. Tumeshuhudia katika miaka ya 90 mabadiliko mengi ya kisiasa, kiuchumi na kijamii na hasa baada ya kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi vya kisiasa. Sisi kama wanaharakati watetezi wa wanyonge, tunaamini kabisa kuwa kuna haja sasa ya kuwa na Katiba mpya ambayo itabeba maoni, mapendekezo na madai ya wananchi walio wengi. Katiba ambayo itajali makundi yote na kutoa kipaumbele cha kuwepo uwiano ulio sawa kwa wanawake na wanaume. Katiba ambayo itazingatia kutoa sheria na sera ambazo zinawanufaisha wananchi wote hasa walioko pembezoni kwa kuzingatia mahitaji yao muhimu hasa ya ajira, afya, elimu, maji, ardhi na mengineo. Sisi kama wanaharakati tumefanya uchambuzi wa kina wa muswada huu na kubaini mapungufu kadhaa. Yafuatayo ni madai na mapendekezo yanayotokana na uchambuzi tulioufanya na mjadala unavyoendelea: 1. Uwiano katika ushiriki na uwakilishi wa vyombo vya Katiba Kwa mujibu wa Ibara ya 6 (1), tunadai, Tume ya kuongoza mchakato huu lazima iwe na uwakilishi asilimia 50:50 wanawake na wanaume, uteuzi wa wajumbe usifanywe na rais peke yake, badala yake bunge au vyombo vingine vyenye mamlaka, pia uteuzi uzingatie wajumbe toka kila jimbo zikiwemo asasi za kiraia, asasi za kidini na makundi ya watu wanaoishi na ulemavu, VVU na Ukimwi. 2. Jina la muswada wenyewe liwakilishe mchakato wa wananchi walio wengi wanavyopendekeza kwa maana ya kutengeneza Katiba mpya, na sio muswada wa sheria ya marejeo ya Katiba iliyopo ( Constitutional review Act, 2011). Kwa mujibu wa kifungu cha 3 neno Katiba limetafsiriwa kumaanisha marekebisho katika Katiba ya sasa 3. Katika kifungu cha 8(1) Hadidu za rejea zisiandaliwe na Rais kama ilivyooneshwa badala yake bunge liunde kamati maalum kwa ajili ya kutoa maamuzi pia kuwepo na usawa wa kijinsia katika uwakilishi wake kwa maana ya wanawake na wanaume na viongozi toka ngazi za kijamii ambao pia watakubaliana muda husika wa kuanza mchakato wa Katiba mpya na muda wa kumaliza mchakato huo. 4. Kifungu cha 17(3) lazima kutengeneza chombo kitakachohakikisha kuwa makundi yote yanawakilishwa katika mikutano na mijadala ya kupata Katiba mpya kwa kujali zaidi wananchi walioko pembezoni hasa wanawake na wanaume, vijana, wanaoishi na VVU na Ukimwi, wanaoishi na ulemavu, wafugaji, wavuvi, wakulima, wanaofanya kazi zisizo rasmi na wengineo 5. Lugha ya muswada iwe ya kiswahili, kwa kuwa muswada huu wa kuandaa Katiba mpya si muswada kama miswada mingine ya sheria za kawaida, na kwa kuwa suala la Katiba ni nyeti na linaliwahusu na kuwagusa watanzania wote, ushiriki wa kila aina katika mchakato wote ni muhimu sana. Tumeshangazwa sana na hatua ya serikali ya kuamua kutumia lugha ya (kiingereza) ambayo watanzania walio wengi hawaielewi kabisa. 6. Katika kifungu cha 21(1) Rais asiwe na madaraka na nguvu za kuunda Baraza la Katiba, badala yake kuwepo na chombo cha kuchagua Baraza la Katiba kama ilivyopendekezwa kwenye tume ya kuongoza mchakato wa kupata Katiba mpya na lichaguliwe moja kwa moja na wananchi 7. Katika kifungu cha 26 jukumu la kusimamia kupata kura za maoni litekelezwe na chombo huru na sio Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tunapendekeza pia mchakato huu usiongozwe au kusukumwa kwa maslahi ya viongozi wachache bali tuhamasishe na kuwezesha watanzania wote wapate nafasi ya kutoa sauti na madai yao. 8. Vyama vya siasa na makundi mengine yasiyolitakia taifa hili mema waache mara moja kuwatumia wananchi masikini kwa kuwahonga ili wavuruge utaratibu wa mijadala. Matumizi ya watoto wadogo, kujadili ajenda za vyama kwenye mijadala badala ya kuchangia muswada, kuzomea na kufayanya vurugu ziachwe mara moja. 9. Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama visiingilie utaratibu kwa kuwatisha wananchi na mabomu ya machozi na silaha kwani hali hii inawatisha wananchi walio wengi kushiriki ipasavyo katika mijadala hii pia vitendo hivi ni kinyume na haki za binadamu. Imetolewa na: Usu Mallya ………………. Mkurugenzi Mtendaji

No comments: