Wednesday, April 13, 2011
Maaskofu wapinga muswada wa Katiba
MAPENDEKEZO ya Muswada wa Sheria ya Kuongoza Mchakato wa kukusanya maoni kuhusu Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, yameendelea kupingwa na sasa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) limeungana na Jumuiya ya Wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA). Katika mdahalo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, UDASA waliendesha kongamano kuhusu Katiba mpya wazungumzaji wakuu wakiwa Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samata na Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Francis Kiwanga. Katika madahalo huo sehemu kubwa ya wazungumzaji walipinga mapendekezo ya muswada huo na hasa vipengele vinavyozuia mijadala ya Katiba mpya kutohoji au kujadili mamlaka Rais, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kwamba atakayefanya hivyo atahukumiwa kifungo cha miaka miwili jela. Kwa mujibu wa wazungumzaji hao kipengele hicho kinapingana na fursa ya sasa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayotoa uhuru wa mijadala bila kuweka mipaka kwa kuegemea mipaka fulani na hasa madaraka. Vuguvugu hilo la wasomi kupinga muswada huo sasa linaungwa mkono na Baraza la Maaskofu Tanzania ambalo kupitia kwa Mwenyekiti wake wa Tume ya Haki, Askofu Paul Ruzoka, wamemuandikia barua Waziri wa Katiba na Sheria wakipendekeza hekima itumike kuimarisha utulivu wakati wote wa mchakato wa Katiba mpya. Barua hiyo iliyoandikwa Aprili 5, mwaka huu inaeleza; “Muswada wa Mabadiliko ya Katiba ya Nchi wa mwaka 2011 Namba 1 wa tarehe 11 Machi, 2011 umetangazwa katika siku chache zilizopita. Baada ya kuusoma muswada huu tulishangazwa kuona kwamba mchakato wote unaanzia na kuishia kwa Rais na kwamba Chombo Kikuu cha kuratibu mchakato wote ni Tume itakayoteuliwa na Rais ambaye ni Mwenyekiti wa Chama tawala. Tunatambua kwamba kilio cha kutaka Katiba mpya kilitokana na utashi mwema na pia hasira njema ya jamii ya Watanzania wakitaka mabadiliko yaliyo na hekima na utu. Tunahofia kwamba maudhui na mwelekeo wa muswada wa marekebisho ya Katiba unaopelekwa Bungeni havitakidhi mahitaji mazito ya watu na huenda ukachochea hasira ambayo imekwisha jidhihirisha katika jamii yetu. Tunakuomba ulisimamie zoezi la marekebisho ya katiba kwa hekima sana ukiongoza tafakari jadidi na elimu angavu itakayo wezesha zoezi lote kuwa la mazungumzo ya kitaifa kweli kweli huku amani, maelewano na makubaliano vikilindwa sana katika wakati mgumu huu. Tafadhali lipatie taifa muda wa kufaa na chombo huru kinachoaminika kuongoza wananchi kufikia makubaliano yatakayojenga msingi imara wa taifa letu kwa wakati ujao,” inaeleza barua hiyo iliyosainiwa na Askofu Ruzoka.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment