WABUNGE wamelalamika kuwa hawajawahi kupata fedha kwa ajili ya kuendesha ofisi zao.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameahidi kuyafanyia kazi malalamiko hayo.
Leo asubuhi wabunge walipiga kelele bungeni kupinga maelezo ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuwa kuna fedha zinatolewa kwa ajili ya kuendesha ofisi za wabunge.
Mwanri amewaeleza wabunge kuwa kuna fedha zinatolewa kwa ajili ya ofisi zao ikiwa ni pamoja na kununulia samani na kugharamia mambo mengine ikiwemo chai.
“Fedha za kuendesha ofisi za wabunge zimekuwa zikitolewa kupitia ofisi za wakuu wa mikoa (Makatibu Tawala wa mikoa) na hatimaye kupelekwa kwenye ofisi za wakuu wa wilaya (Makatibu tawala wa wilaya)” amesema Mwanri wakati anajibu swali la Mbunge wa Mkinga, Mbarouk Mwandoro.
Mbunge wa Pangani, Mohamed Rished Abdallah, amesema bungeni kuwa hafahamu kama kuna fedha zinatolewa kwa ajili ya ofisi ya Mbunge.
Mbunge wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai amesema amekuwa Mbunge kwa miaka 15 na hajawahi kupata fedha za ofisi yake.
Mbunge huyo alishauri kuwa, fedha hizo ziingizwe kwenye fungu la fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo wa Jimbo (CDCF), Waziri Mkuu Mizengo Pinda amekataa.
Waziri Mkuu amewaeleza wabunge kuwa kwa mfumo wa sasa haifahamiki fedha kiasi gani zinapelekwa kwa Mbunge yupi ili kuendesha ofisi.
Pinda amesema, Serikali itatafuta mfumo mzuri wa kuzisimamia fedha hizo hivyo wabunge wampe muda.
Mwanri amewapongeza wabunge kwa kuuliza kuhusu fedha za CDCF kwa kuwa hata yeye na Waziri Mkuu wanazihitaji kwa sababu wana majimbo.
Mwandoro alimuuliza Waziri Mkuu, ni lini Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Bunge itaanza kuzitumia fedha za CDCF kwa kuwa Bunge lilishapitisha sheria hiyo, na Rais wa Tanzania ametoa kibali iwe sheria rasmi.
Mwanri amelieleza Bunge kuwa fedha za CDCF ni za maendeleo, si za kwa ajili ya kuendesha ofisi ya Mbunge.
No comments:
Post a Comment