Wednesday, February 3, 2010

Miswada muhimu yasogezwa mbele

MISWADA miwili ya Uchaguzi ambayo imekuwa ikisubiriwa kwa hamu kuwasilishwa jana bungeni, sasa itawasilishwa rasmi Jumatatu ijayo, huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Sera, Uratibu na Bunge, Philip Marmo akisema imesogezwa mbele ili kuiboresha zaidi.

Akizungumza na HabariLeo juzi mjini hapa, Marmo alisema miswada hiyo ambayo ni wa Gharama ya Uchaguzi na wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi yote ya mwaka 2009, imekuwa ikivutia hisia za watu wengi hivyo kuonekana bora kushirikisha wadau zaidi ili iweze kueleweka.

“Tunachofanya ni kuhakikisha tunawaelewesha wabunge na wananchi kuwa miswada hii si ya kuwaadhibu bali kuhakikisha kuwa makosa yanayofanyika katika uchaguzi yanadhibitiwa,” alisema Marmo.

Alisema sheria iliyopo ya uchaguzi imekuwa na makosa mengi hasa katika upande wa rushwa, hivyo sheria ya sasa inajaribu kufafanua zaidi kipi halali na kipi si halali kwa kuzingatia maoni ya wadau.

Alisema katika mkutano uliofanyika hivi karibuni chini ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kila mbunge aliyezungumza hakupinga moja kwa moja muswada huo, bali alitaka ufanyiwe maboresho zaidi hasa katika kipengele cha taratibu za kuwa wazi wakati wa uchaguzi, mwenendo usiofaa katika kampeni na kumchangia mtu fedha nyingi kupita kiasi.

Alisema lengo la sheria hiyo ni kuwa wazi kwa matumizi ya fedha wakati wa kampeni, hali ambayo haikudhibitiwa katika sheria ya uchaguzi iliyopo ambayo inatakiwa kufanyiwa marekebisho.

wali akiahirisha Bunge katika Kikao cha Sita cha Mkutano wa 18 unaoendelea mjini hapa, Mwenyekiti wa Bunge, Zubeir Ali Maulid, alitangaza mabadiliko ya ratiba ikionesha kuwa miswada hiyo miwili ingewasilishwa mmoja jana na mwingine kesho na kila mmoja ukijadiliwa kwa siku mbili.

Kwa mujibu wa ratiba ya sasa muswada wa gharama za uchaguzi utawasilishwa siku ya Jumatatu na muswada wa Marekebisho ya Sheria utawasilishwa Jumatano.

Ratiba hiyo inaonesha badala ya muswada wa gharama kutakuwa na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa kuhusu Kahawa wa mwaka 2007 na Azimio la Bunge kuridhia Mkataba wa Kimataifa kuhusu Hakimiliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mimea na Azimio la Bunge la kuridhia Itifaki ya Jinsia na Maendeleo ya Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

No comments: