ALIYEKUWA Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu Tanzania (BoT), Emmanuel Boaz, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwamba maofisa wa BoT, Iman Mwakosya, Ester Komu na Sophia Larika, wanaokabiliwa na mashitaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), kupitia kampuni ya Mibale Farm hawakufanya kosa.
Boaz alipohojiwa na mawakili wa washitakiwa hao ambao wanashitakiwa pamoja na Farijala Hussein, Rajab Maranda na Ajey Somani, alidai kuwa kwa uelewa wake, kama ambavyo yeye alikuwa akitenda kazi zake na washitakiwa hao, walifanya hivyo pia hajui kama walikuwa na nia ovu katika kuidhinisha malipo ya zaidi ya Sh bilioni 3.8.
Akihojiwa jana na wakili Majura Magafu, alikubaliana naye kwamba waliopitia jalada la maombi ya kuhamishiwa deni kwenda Kampuni ya Mibale kutoka Kampuni ya India ya Lakshmi Textile Mills, walikuwa 10 akiwamo yeye na kuwa hajui sababu ya maofisa hao kushitakiwa na wengine kuachwa.
Aliendelea kudai, kuwa malipo ya Mibale Farm hayakuwa na shaka kwani yalikuwa halali na pia hakukuwa na shaka dhidi ya ofisa yeyote wa BoT kuhusu malipo hayo.
Mbele ya jopo la mahakimu watatu wakiongozwa na Samwel Kalua, shahidi huyo alidai kwamba yeye na watendaji wote waliokuwa wakishughulikia malipo ya kampuni hiyo, walifuata maelekezo ya aliyekuwa na kauli ya mwisho katika malipo hayo, Gavana wa BoT, Daudi Balali (marehemu).
Katika mashitaka hayo, Mibale Farm inadaiwa kuhamishiwa deni la BoT na Lakshmi Textile Mills. Hussein, Maranda, Somani na Kiza Selemani ambaye hayumo katika kesi hiyo, walisaini hati za makubaliano hayo ya kuhamisha deni ambayo inadaiwa kuwa ni ya kughushi.
Ilidaiwa kuwa Oktoba 26, 2005, BoT iliingiza fedha hizo kwenye akaunti iliyofunguliwa na watuhumiwa hao ikiwa na namba 6005274 ya Mibale Farm katika Benki ya Barclays na benki hiyo kutia shaka kwa kuwa fedha hizo ziliingizwa kwa jina la Mibale Farm na si Nibale Farm na hivyo ilitaka kufahamu uhalali wake.
1 comment:
Wizi mtupu!!!!
Post a Comment