Tuesday, February 23, 2010

Kikwete apewa nafasi kubwa kushinda uchaguzi 2010

RAIS Jakaya Kikwete amepewa nafasi kubwa ya kushinda Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu kwa kuwa wananchi wanampa nafasi kubwa ya kuwashinda wapinzani wake watakaojitokeza kuwania kwenda Ikulu.

Utafiti uliofanywa na kampuni ya Synovate umebainisha kuwa, utendaji wa Kikwete unawaridhisha wananchi kwa asilimia 75.

Wananchi pia wamesema, chama cha siasa ambacho kipo karibu zaidi na wananchi ni Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Kwa mujibu wa wananchi hao, CCM ipo karibu na wananchi kwa asilimia 70, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa asilimia 17, Chama Cha Wananchi(CUF) kwa asilimia 9, NCCR Mageuzi kwa asilimia 2,Tanzania Labour(TLP) na UDP asilimia 1.

Kwa mujibu wa taarifa ya utafiti ya kura ya maoni ya robo ya mwisho Oktoba- Desemba mwaka jana iliyofanywa na kampuni hiyo, lengo lilikuwa ni kupata kura ya maoni ya watanzania katika mambo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi katika vipindi tofauti ndani ya mwaka.

Meneja wa Utafiti wa Vyombo vya Habari na Umma wa kampuni hiyo, Abdallah Gunda, amewaeleza waandishi wa habari kuwa, kampuni hiyo ambayo zamani ilijulikana kwa jina la Steadman Group ilikusanya maoni kwa kuwahoji watu 2000.

Amesema, watu hao waligawanywa sawasawa na uwiano wa idadi ya wananchi wa Tanzania na ilikusanya mahojiano ya uso kwa uso katika maeneo tofauti yaliyochaguliwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo,watu hao walipoulizwa ni Rais yupi wangependa awe kwa mwaka 2010, walimchagua Kikwete kwa asilimia 75.

Kikwete alifuatiwa na Freeman Mbowe kwa asilimia 10, Profesa Ibrahim Lipumba alipata kura kwa asilimia 9, John Cheyo, Salim Ahmed Salim na Zitto Kabwe ambao walipata asilimia 1.

Mbunge aliyefanya vema kwa kipindi hicho cha mwisho wa mwaka 2009 ni Zitto Kabwe kwa asilimia 31, Anne Kilango Malecela asilimia 13, Dr. Wilbroad Slaa asilimia 7, Dr. Harrison Mwakyembe asilimia 6, John Magufuli asilimia 3, Lawrence Masha asilimia 2.

Wabunge wengine ni Mizengo Pinda, Mohamed Dewji, Lucas Selelii, Samuel Sitta, John Cheyo, John Nchimbi, Halima Mdee, Jenista Mhagama, Philemon Ndesamburo, Hamad Rashid Mohamed, David Mathayo, Mark Mwandosya na Hamis Kagasheki ambao wote wamepata kura za maoni kwa asilimia 1.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo,zaidi ya robo tatu ya watanzania wanaamini kwamba Tanzania ni nchi yenye demokrasia, asilimia 57 kati yao wanaamini kwamba yapo matatizo madogo madogo.

Asilimia 21 ya waliohojiwa wamesema, Tanzania ipo demokrasia kamili, demokrasia yenye matatizo makubwa asilimia 15 wakati asilimia 3 ya wananchi walidai kwamba nchi haina demokrasia.

Wananchi walipoulizwa endapo uchaguzi ungeitishwa kesho ni wangapi wangepiga kura asilimia 94 walidai wangepiga kura, na asilimia 5 walisema wasingepiga kura.

Asilimia 69 walidai wamechoshwa na siasa, asilimia 9 walisema hawajajiandikisha, asilimia 7 ya wananchi walisema wagombea hawawasaidii.

Gunda amesema, katika utafiti huo walipita mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mbeya,Kagera, Dar es Salaam, Kigoma, Zanzibar, Tanga, Morogoro, Tabora, Iringa, Dodoma, Kilimanjaro, Arusha, Mtwara, Mara, Singida, Rukwa, Manyara, Ruvuma, Pwani, Lindi na Pemba.

Aidha alisema kuwa waliwahoji wanaume kwa asilimia 54 na wanawake asilimia 46,waliwagawa katika matabaka manne kuanzia umri wa mika 18-27 asilimia 39 walihojiwa, 28-37 asilimia 32, 38-47 asilimia 16 na miaka 48 na kuendelea walihojiwa asilimia 14.

Pia alisema kuwa watu 100 walishiriki kufanya mahojiano na kwamba,walikuwa wamepatiwa mafunzo.

1 comment:

Anonymous said...

Huo utafiti sidhani kama ni kweli, itakuwa wanampigia debe tu, hata kama ni sampling haiwezi kutoa majibu ya ukweli.