Monday, February 1, 2010

Mtangazaji anayefichua tuhuma za rushwa mbaroni


JESHI la Polisi katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia mtangazaji wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), Jerry Muro, kwa tuhuma za kudai fedha kwa njia ya vitisho kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana jioni, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleimani Kova alisema Muro alimtishia Wage kuwa yeye ni Ofisa wa Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kumtaka atoe fedha Sh milioni 10.

“Mpaka sasa, Polisi bado inamhoji mtuhumiwa na baada ya mahojiano hayo kukamilika, taratibu za kisheria zitachukuliwa dhidi yake na maelezo zaidi kuhusu mtangazaji huyo nitayatoa kesho (leo) wakati wa mazungumzo yangu na waandishi wa habari,” alisema Kova jana saa 12:15 joni.

Gazeti hili lilimshuhudia mtangazaji huyo akiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi, akiwa ameshikilia bahasha kubwa tatu za khaki pamoja na kamera ya video.

Akizungumzia tukio hilo, Muro ambaye amejipatia umaarufu katika siku za karibuni kwa vipindi vyake vya uchunguzi, alikana tuhuma hizo na kueleza kushangazwa kuwekwa chini ya ulinzi kwa madai kuwa alipigiwa simu na mtu kupewa taarifa kuwa kuna kazi katika Hoteli ya City Garden, katikati ya Jiji.

“Nilipewa taarifa ya kazi City Garden, lakini baada ya kufika hapo nilishangaa nawekwa chini ya ulinzi na askari waliovaa kiraia ambao ndiyo walionifikisha kituoni hapa ingawa sielewi kosa langu, lakini nakana tuhuma hizo siyo kweli,” alisema Muro.

Naye mlalamikaji Wage alidai mtuhumiwa huyo anatumiwa na watu wengine ambapo juzi alimpandisha katika gari lake na kumfunga pingu kisha kumtaka atoe Sh milioni 10. Kwa kuthibitisha kuwa alikuwa ndani ya gari hilo, alidai kuacha miwani yake yenye mikanda myeusi.

Baada ya polisi kumhoji, Muro kama anazo pingu, alikiri kumiliki pingu pamoja na bastola ambapo baada upekuzi katika gari lake lenye namba za usajili T545 BEH aina ya Toyota Crester, polisi walikuta pingu hizo pamoja miwani iliyodaiwa kuwa ya mlalamikaji.

Hadi kufikia saa 12:15 jioni, gazeti hili lilipoondoka kituoni hapo, mtangazaji huyo alikuwa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano.

Muro ni mtangazaji aliyejizolea umaarufu zaidi kupitia kipindi chake cha Usiku wa Habari kinachooneshwa kila siku kupitia Kituo cha TBC1. Kabla ya kuhamia TBC, alikuwa mtangazaji wa ITV.

1 comment:

Anonymous said...

Pole sana Jerry, usivunjike moyo kwenye harakati zako za kuwafichua mafisadi, shida kama hizo hutokea mara nyingi kwa wanaharakati.

Mdau