Thursday, February 11, 2010

Sakata la Richmond lazikwa Dodoma

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imejivua suala la utata wa mkataba baina ya Tanesco na kampuni ya Richmond Development Company LLC, baada ya kueleza kuridhishwa na utekelezaji wa Serikali wa maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo huku ikielekeza kwamba masuala yaliyobaki, badala ya kubaki kama maazimio ya Bunge, yapelekwe kwenye kamati za kisekta zinazohusika.

Kamati hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake, Mbunge wa Bumbuli, William Shelukindo (CCM), imeliomba Bunge azimio lililotaka Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na maofisa wa taasisi hiyo walioshiriki katika uchunguzi wa kuandaa taarifa ya Richmond wawajibishwe, kwa sasa liachwe kwenye mamlaka ya juu ya nchi.

Katika taarifa ya Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo, hususan kuhusu watumishi hao wa Takukuru, Shelukindo alisema kamati imeona kuwa haitakuwa haki kutolea maelezo au majibu kwa Serikali kuhusu azimio hilo, kwa sababu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru anawachunguza wabunge.

“Kwa mantiki hii, kamati inaona Bunge likubali kwamba suala hili liachwe kwenye Mamlaka ya Juu ya Nchi,” alisema Shelukindo na kusisitiza kwamba hata kwenye kamati, azimio hilo Namba 9 halikujadiliwa. Kikatiba, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru huteuliwa na Rais.

Wakati katika maazimio mengi kamati ilieleza kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali, kwenye maazimio namba 5,7,9 na 14 yaliyotaka Serikali kuwawajibisha watumishi wote wa umma waliohusika katika suala hilo la Richmond, imeshauri Bunge likubaliane na maelezo yaliyotolewa na Serikali juu ya hatua ya Waziri Mkuu na mawaziri wawili waliowahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini kuwajibika kwa kujiuzulu.

“Kamati imezingatia maoni yaliyotolewa katika ripoti hii. Tofauti na ripoti iliyowasilishwa Agosti 2009, kwa kuwa haikutoa maelezo yoyote juu ya suala hili. Kwa kuwa Serikali sasa imejiridhisha kwenye kifungu 36(d)..., kamati inashauri Bunge likubaliane na maelezo hayo kwa kuzingatia msingi huo wa uwajibikaji,” alisema Shelukindo.

Alinukuu kifungu hicho cha 36(d) kwa kusema: “hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu pamoja na mawaziri wawili waliowahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini kwa kutekeleza dhana nzima ya uwajibikaji katika suala hili linalohusu zabuni kati ya Tanesco na Richmond”.

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Edward Lowassa, alipoulizwa na waandishi wa habari kuhusu taarifa hiyo ya kamati alisema baada ya kutoka katika ukumbi wa Bunge jana mchana kabla ya suala hilo kuhitimishwa jioni, hakuwa na maoni zaidi ya kusema anawaachia wabunge wachangie.

Hata hivyo, taarifa ya Serikali ya utekelezaji wa maazimio namba 8 na 14 yaliyoitaka Serikali kuwawajibisha viongozi wenye dhamana ya kisiasa waliokuwa mawaziri hao wa Nishati na Madini ambao ni Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi, inaonesha suala la mawaziri hao halijaisha.

Taarifa hiyo inasema kwa sasa vyombo vya Dola vimekamilisha uchunguzi wa ndani ya nchi, lakini uchunguzi wa nje kwa kushirikiana na vyombo vya Dola vya kimataifa unaendelea na Serikali imehimiza vyombo hivyo vihitimishe suala hilo.

Katika maoni ya Kamati juu ya utekelezaji huo, Shelukindo aliliambia Bunge kwamba wamezingatia maelezo hayo ya Serikali kwa kupendekeza kuwa hatua hiyo iendelee chini ya usimamizi wa Serikali yenyewe, na utakapokuwa tayari, taarifa itolewe kwenye Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Maazimio mengine ambayo kamati imeridhishwa nayo, ni namba moja na mbili yaliyoielekeza Serikali kufanya mapitio upya ya Sheria ya Ununuzi ya Umma ya mwaka 2004 kwa malengo ya kuiboresha na kuipa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA). Maazimio hayo pia yaliitaka Mamlaka hiyo isiwajibike kwa Wizara ya Fedha.

Serikali katika ufafanuzi wake, ilisema muswada husika utawasilishwa bungeni katika mkutano wa Aprili mwaka huu, hali ambayo kamati pamoja na kuridhishwa na hatua hiyo, imeshauri Serikali iendelee kushughulikia suala hilo na kuwasilisha taarifa kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi.

Kuhusu Azimio namba 3 ambayo pamoja na mambo mengine, ilitaka mikataba ya madini ipitiwe upya, kamati ilipongeza Serikali kwa hatua iliyofikiwa katika kurekebisha mkataba wa Songas na kuhimiza utaratibu huo ufanyike kwenye mikataba mingine iliyobaki.

Eneo lingine ambalo Serikali imeikonga kamati, ni kwenye azimio namba 11 lililotaka kudhibiti utaratibu wa viongozi waandamizi wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi wakiwa madarakani.

Serikali katika maelezo kuhusu utekelezaji wake, imesema kipo kikundikazi kilichoundwa kushughulikia azimio hili kwa kuandaa waraka wenye Mapendekezo ya Kurekebisha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Sura 398) ulio katika ngazi ya kujadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC).

Hata hivyo, kamati ilieleza kukubaliana na maelezo hayo ya Serikali lakini kwa kushauri iwasilishe Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 ili ufanyiwe marekebisho na kupelekwa kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, kabla ya Bunge hili kumaliza muda wake.

Katika Azimio namba 10, kamati ilimpongeza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kuchunguza kwa umakini na kugundua kuwa malipo ya usafirishaji wa mitambo yalifanyika mara mbili; yaani kwa kutumia ndege na meli. Lakini ilishauri Serikali iendelee kufuatilia suala hilo, ili fedha hizo zirejeshwe serikalini.

Kuhusu azimio la kutaka wamiliki wa Richmond wafunguliwe kesi ya jinai, kamati ilieleza kuzingatia hatua zilizofikiwa na Serikali kwa kumfikisha mwakilishi wake, Naeem Gire mahakamani. Hata hivyo ilisisitiza wamiliki wafikishwe mahakamani na Serikali itoe taarifa kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Miongoni mwa wabunge waliochangia, ni wa Viti Maalumu, Stella Manyanya (CCM) ambaye licha ya kuwa mjumbe wa kamati hiyo, vile vile alihusika katika kamati maalumu iliyoundwa kuchunguza sakata hilo la Richmond.

Manyanya alisema watu wanaweza kujiuliza kwamba kwenye maazimio mbona Bunge linakubaliana na kuyapitisha; lakini alifafanua kwamba, “Bunge lilikuwa halibishani wala kushindana, bali lilichukua wajibu kutekeleza majukumu yake.

“Kwa upande wa Serikali, maazimio mengi yametekelezwa. Hilo ndo suala la msingi. Lakini sivyo tu, vilevle yale ambayo yanahitaji uchunguzi wa kina, ndiyo maana tumesema badala ya kubaki kwenye Bunge kama maazimio, yarudi kwenye sekta zinazohusika.”

Taarifa ya Serikali iliyopitiwa na kamati hiyo na kuiwasilisha jana bungeni, ilitanguliwa na taarifa mbili zilizowasilishwa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Agosti 28, mwaka juzi, nyingine Februari 11, mwaka jana na taarifa moja iliyokabidhiwa na kujadiliwa na kamati, ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na Bunge ambayo katika uwasilishwaji wake uliofanyika Februari mwaka jana, utekelezaji wake ulikuwa haujakamilika.

Wakati huo huo, taarifa kuhusu namna Serikali ilivyoshughulikia suala la mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira, Kamati hiyo ya Nishati na Madini kupitia kwa Makamu Mwenyekiti wake, Dk Harrison Mwakyembe, iliipongeza Serikali kwa hatua ilizochukua kwa kusema hiyo ni ishara tosha ya Serikali kujali wananchi wake.

Hata hivyo, pamoja na kueleza kuridhishwa, kamati iliainisha baadhi ya maeneo yanayohitaji kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuikumbusha Serikali kufuatilia uchunguzi uliofanywa na Takukuru wa Sh milioni 50 zilizotolewa kutoka Consolidated Holdings Corporation kwenye mfuko wa mafao ya wafanyakazi wa mgodi huo.

Iliitaka Serikali ikamilishe haraka makabidhiano ya mgodi huo kutoka kampuni ya TANPOWER ili wafanyakazi ambao wanaendelea na shughuli za kutunza mgodi huo, sasa wafahamu wanaripoti kwa nani pindi watakapohitaji huduma.

Kwa upande mwingine, Kamati ilishangazwa na kitendo cha viongozi waandamizi wa Tanpower kulipwa malimbikizo ya mshahara hadi Sh milioni 80 kwa mwezi, wakati wafanyakazi wa kati walilipwa Sh milioni nane na ngazi ya chini Sh milioni 1.5.

1 comment:

Anonymous said...

Tatizo kubwa la nchi yetu ni kulindana, viongozi wetu wa serikali wanalindana kwa maovu yao na matokeo yake sie walipa kodi tunaumia kwa makosa yao na waliokosea hawachukuliwi hatua yoyote ya kisheria.
Hii inavunja moyo sana na ndio inachochea rushwa kwa ngazi za chini za uongozi maana wataona kumbe ni sawa tu kufanya ufisadi maana hakuna hatua zozote zinazochukuliwa kwa matumizi mabaya ya madaraka.

Mwana GDSS