MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Daniel ole Njoolay, yupo tayari kujiuzulu endapo mamlaka za uteuzi zitamtaka awajibike kutokana na kashfa ya ufisadi wa fedha za ruzuku ya pembejeo za kilimo inayowakabili viongozi mkoani humo.
Njoolay amewaeleza waandishi wa habari kuwa, yupo tayari kujiuzulu ikiwa hana budi kufanya hivyo.
Ametoa msimamo huo baada ya kupokea taarifa ya tume aliyoiunda kuchunguza kashfa ya matumizi mabaya fedha za ruzuku ya pembejeo za kilimo kupitia mfumo wa vocha.
Inadaiwa kuwa,viongozi mkoani humo wametumia visivyo Sh bilioni 6.8,za ruzuku.
“Uongozi wa Mkoa wa Rukwa unaiomba radhi sana serikali kwa kashfa hii iliyotokea mkoani na tutakuwa tayari kuwajibika kisiasa kama hapana budi,” imesema sehemu ya taarifa ya Njoolay aliyoitoa kwa waandishi wa habari.
Taarifa ya tume hiyo ya watu tisa iliyofanya uchunguzi kwa takribani mwezi mmoja, imebainisha kuwa waliohusika na ufisadi huo ni watendaji 43 wa vijiji, mawakala 23, watumishi wanne wa kilimo ambao wote watafikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Kwa mujibu wa Njoolay,wenye nyadhifa za kisiasa waliobainika kuhusika na kashfa hiyo wakiwemo madiwani na wakuu wa wilaya watafikishwa kwenye vyama vyao vya kisiasa ili washughulikiwe huko.
Taarifa ya Njoolay imeeleza kuwa, uchunguzi wa tume umebaini mambo mengine kadhaa ikiwa ni pamoja na mkoa, wilaya na vijiji kutokuwa makini kusimamia na kufuatilia kwa karibu usambazaji wa ruzuku ya pembejeo ya kilimo kwa wakulima.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo,'wajanja' walitumia mwanya huo wa Serikali kutofuatilia kwa makini kuiibia Serikali mabilioni hayo ya fedha.
Kazi ya kufanya hesabu haijakamilika,lakini kiasi kilichokuwa kimechukuliwa benki ni Sh bilioni 6.8 na kilichobaki ni Sh bilioni 1.6 tu.
Kati ya hizo kiasi kilichotumika vizuri, asilimia 25 zimetumika Sumbawanga, asilimia 30 Nkasi na asilimia 80 80 wilayani Mpanda.
Waliohusika kuiba fedha hizo za Serikali walitumia mbinu kadhaa ikiwa ni pamoja na kughushi sahihi za wakulima, kuandikisha wakulima hewa, wafu, watoto,na vichaa.
Mbinu zingine ni pamoja na kuwahonga wakulima fedha kidogo kati ya Sh 2,000 na 7,000 ili watie saini vocha bila kupata mbolea na pia kuwapatia wakulima idadi ndogo ya mbolea kuliko kiasi halisi walichosainishwa.
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa imeagiza hatua kadhaa zichukuliwe zikiwemo za kuipongeza Wilaya ya Mpanda kwa kusimamia kwa ufanisi suala hili na hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watumishi wa Serikali waliolegalega kufuatilia kwa ukaribu zoezi hili.
Hatua nyingine ni pamoja na mawakala wote na watendaji walioibia Serikali wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na tume iendelee na uchunguzi kuwabaini wengine, kuna uwezekano idadi ya watuhumiwa ikaongezeka.
Tume ya kuchunguza uozo huo uliokuwa ukipigiwa kelele na wakulima wengi waliolalamika kukosa pembejeo za kilimo msimu huu, iliundwa Januari 11, mwaka huu na mkuu wa mkoa huyo.
No comments:
Post a Comment