Wednesday, February 3, 2010
Polisi: Muro alishirikiana na watuhumiwa sugu
POLISI Dar es Salaam imesema mtangazaji wa TBC, Jerry Muro ameshirikiana na watuhumiwa sugu wa utapeli kumdai rushwa ya Sh milioni 10 aliyekuwa Mhazini wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, jana aliwaonesha waandishi wa habari watuhumiwa hao ambao wanadaiwa pia kuwa na kesi mbalimbali za utapeli na kujifanya kuwa ni maofisa Usalama wa Taifa.
Watuhumiwa hao Edmund Kapama (52) mkazi wa Mwananyamala amebainika kwamba mwaka jana alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, akikabiliwa na tuhuma za udanganyifu akijifanya ofisa usalama wa Taifa aliyetumwa kuchunguza mwenendo mbaya wa kazi wa Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana na kutaka apewe rushwa.
Mwingine aliyehusishwa na Jerry ni Deogratias Mgasa (35), mkazi wa Mbezi Beach ambaye pia alikamatwa mwaka jana akidaiwa kuwa kiongozi wa mtandao wa matapeli nchini akituhumiwa kutapeli Sh bilioni 4 kutoka kwa watu zaidi ya 40.
Mtuhumiwa huyo akiwa na wenzake, inadaiwa alijifanya mtumishi wa taasisi nyeti, ikiwamo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru), Usalama wa Taifa na Jeshi la Polisi na wote wanadaiwa kuibia wafanyabiashara, watumishi wa sekta mbalimbali na taasisi za fedha.
“Katika kuendelea na upelelezi wa kesi ya Michael anayedaiwa kupata vitisho na kutakiwa atoe Sh milioni 10 na watuhumiwa watatu, polisi waliwatia mbaroni watuhumiwa wengine wawili baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema,” alisema Kamanda.
Alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi katika mgahawa maarufu wa PR Camp, Kinondoni na kabla ya kukamatwa polisi wapelelezi walipata kumbukumbu za watuhumiwa hao wakidaiwa kushirikiana na Muro kupitia picha zilizoonekana kwenye CCTV.
“Katika tukio hili watuhumiwa watatu walionekana wakiwa katika meza ya mazungumzo na mlalamikaji. Pia kumbukumbu zingine zinaendelea kufuatiliwa kwa kutumia mtindo huu wa vifaa vya teknolojia ya kisasa, ili kuondoa ubishi au utata kwa lengo la kupata ufanisi na uwazi,” alisema.
Aidha, alisema walipata kumbukumbu za hoteli walizokaa kati ya Januari 28 na 29 mwaka huu na walifanya upelelezi na kukutana na wahusika wa hoteli na wahudumu na kukubali kuwatambua, ingawa hawakutambua walichokuwa wakijadili na kwamba yataelezwa zaidi mahakamani.
Pia Kova alisema watu hao walifanyiwa gwaride la utambulisho na mlalamikaji aliwatambua. Hata hivyo, alisema kwamba watuhumiwa hao wawili watafikishwa mahakamani wakati wowote huku Muro akisubiri jalada lake lifikishwe kwa wakili wa Serikali Kanda ili kujiridhisha.
Alipoulizwa iweje watuhumiwa wote wafunguliwe jalada moja halafu mmoja atengwe na wengine wapandishwe kizimbani, Kova alijibu kwamba Polisi ina mamlaka ya kuamua mshitakiwa afikishwe mahakamani kwa wakati gani endapo yuko nje kwa dhamana.
“Mtuhumiwa anapokuwa nje ni uamuzi wa Polisi kumpeleka mahakamani kwa wakati wowote, labda kama angekuwa yuko mahabusu ndipo kungekuwa na muda maalumu wa kumpeleka mahakamani.
Muro ni mwaminifu na tunaamini hawezi kutoroka maana ni mwajiriwa ila hawa ni matapeli nikiwaachia hapa siwapati tena,” alisema.
Akizungumzia utata uliopo na tetesi kwamba tuhuma hizo za Muro zimepikwa, alisema yeye hawezi kujidhalilisha kwa kesi kama hiyo, isipokuwa anatimiza wajibu wake kama polisi na asingeweza kukwepa jukumu hilo, maana limepitia mikononi mwake.
“Katika kesi hii hakuna mipango yoyote na sidhani kama kuna kitu cha tofauti zaidi ya tuhuma zilizopo na kama kipo cha tofauti, mimi sikijui … hapa natimiza wajibu wangu na siwezi kubambika kesi kama hii na kamwe siwezi kujidhalilisha kwa kupanga kakesi kama haka,” alisema Kamanda.
Kuhusu risiti ya pingu ambayo Muro alitakiwa kuiwasilisha alisema kuwa hadi jana mchana alikuwa bado hajaiwasilisha.
Muro, ambaye mwaka jana alipata tuzo ya mwandishi bora, alikamatwa na Polisi Januari 31 mwaka huu mchana, katika hoteli ya City Garden katikati ya Jiji akidaiwa kutaka kupokea rushwa ya Sh milioni 10 ingawa hakukutwa na udhibiti.
Hata hivyo baadaye polisi walimfikisha katika kituo kikuu na kumhoji kwa saa kadhaa na hatimaye kumwachia huru akisubiri jalada lifikishwe kwa Mwanasheria wa Serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment