Thursday, February 4, 2010

UFAFANUZI WA SPIKA KUHUSU TAARIFA POTOFU ZILIZOTOLEWA NA BAADHI YA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU SERIKALI KUUONDOA MUSWADA WA BARAZA LA USALAMA LA TAIFA WA

Waheshimiwa Wabunge, napenda kutoa ufafanuzi kuhusu utaratibu unaotumika kuamua ni Muswada upi uende Kamati gani, na huu utaratibu siyo kwamba ni hiari ya mtu isipokuwa unatawaliwa na Sheria na Kanuni za Bunge. Kwahiyo napenda kutoa ufafanuzi kuhusiana na mwenendo wa kupeleka Miswada katika Kamati kwa mujibu wa Kanuni zilizotungwa na Bunge kama ifuatavyo;

Muswada wa Sheria hupelekwa kwenye Kamati na Spika kama isemavyo Kanuni ya 84(1) “Spika atapeleka Muswada wa Sheria kwenye kamati inayohusika na Kamati itaanza kuujadili muswada huo mapema iwezekanavyo’’

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge toleo la 2007, Kanuni ya 114(14) inasema; Kamati inayohusika ni ile iliyopelekewa Muswada kwanza kama isemavyo Kanuni hiyo nanukuu;

“Kamati yoyote ambayo Spika atapeleka kwake kwanza Muswada au jambo lingine lolote, itahesabiwa kuwa ndiyo Kamati inayohusika kushughulikia Muswada huo au jambo hilo’’

Kwa mujibu wa Kanuni hizi uamuzi wowote wa Spika kupeleka Muswada kwenye Kamati yoyote ni halali kwa kuwa amepewa mamlaka ya kufanya hivyo.

Hata hivyo, kwa kuzingatia matakwa ya Nyongeza ya Nane Kifungu cha 9(1)b ya Kanuni za Bunge Toleo la 2007, moja ya Majukumu ya Kamati za Kudumu za Sekta ni kushughulikia Miswada ya Sheria na Mikataba inayopendekezwa kuridhiwa na Bunge iliyo chini ya Wizara inayozisimamia, kwa hiyo tunazo Kamati za Kisekta ambazo zinaweza kupewa Miswada ya Sekta zake, kwa hiyo Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ndiyo inayosimamia Ofisi ya Rais – Utawala Bora kama ilivyotajwa kwenye Nyongeza ya Nane, Kifungu cha 8(2)(a) kisemacho:
“Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala itasimamia shughuli za Wizara zifuatazo:
(a) Ofisi ya Rais;
(i) Utawala Bora
(ii) Menejimenti ya Utumishi wa Umma.” na
Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, kwenye Nyongeza ya Nane, Kifungu cha 8(4) Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama inasimamia shughuli za Wizara zifuatazo:-
Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa;
Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki;
Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Hivyo waheshimiwa wabunge kwa mujibu wa Kanuni, Nyongeza ya Nane, Kifungu cha 8(2)(a) na 9(1)(b) hakukuwa na kosa wala tatizo lolote kwa maamuzi ya kupeleka muswada huo katika Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala kwa sababu sekta ama Wizara hii iko chini ya Kamati hii.
Waheshimiwa Wabunge, Kamati inayopelekewa Muswada inaweza kuwaruhusu Wabunge ambao si wajumbe wa Kamati au watu ambao si Wabunge kuhudhuria na kushiriki katika shughuli za Kamati kama ilivyo Kanuni ya 114(8) isemayo:
‘’Bila kuathiri masharti yaliyotangulia ya Kanuni hii, kila Kamati itajiwekea utaratibu wake, na Kamati inaweza kuwaruhusu wabunge ambao si wajumbe wa Kamati au watu ambao si wabunge kuhudhuria na kushiriki shughuli za Kamati lakini hawatakuwa na haki ya kupiga kura’’.
Kwa hiyo tarehe 3/11/2009 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ilifanya kikao cha pamoja na Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kujadili kwa pamoja muswada huo Dodoma Hotel.
Kamati ilikwenda mbali zaidi kwa kuwaita pia wadau mbali mbali waje kujadili muswada huo na tarehe 15 Oktoba, 2009 Kamati ilialika wadau na waliofika walikuwa ni taasisi zisizo za kiserikali za NOLA (National Organization for Legal Assistance) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (Legal and Human Rights Centre).

Hata hivyo, tangu tarehe 30 Januari, 2010 baadhi ya Vyombo vya Habari vimekuwa vikitoa taarifa potofu kuhusiana na kuondolewa na Serikali kwa Muswada wa Baraza la Usalama wa Taifa kwa kutumia kifungu 87(1) cha Kanuni za Bunge baada ya michango ya baadhi ya Wabunge kuonyesha kutokukubaliana na baadhi ya vifungu katika Muswada huo.
Habari hizo za upotoshaji zimekaziwa jana tarehe 2 Februari, 2010 katika gazeti lingine la Mtanzania Toleo namba 512 lililobeba habari yenye ujumbe usemao “Sitta aikoroga Serikali’’ likiwa na dondoo zifuatazo:
Apeleka Muswada kwenye Kamati siyo
Siri yavuja, Ofisi yake ilionywa ikakataa
Malecela, Ngwilizi, Lubeleje washangaa
Na gazeti lingine la Tazama Tanzania, toleo namba 378 nalo la tarehe 2 Februari, 2010 lililobeba habari yenye kichwa cha habari kinachosomeka `Spika Sitta achangia kumkwaza Waziri Sophia Simba’.
Waheshimiwa Wabunge, kama nilivyosema ni vizuri magazeti yakatumia kanuni zetu. Kuondolewa kwa Muswada uliowasilishwa na Mheshimiwa Waziri, Sophia Simba, ni utaratibu tu, na wala siyo mara ya kwanza kwa Muswada kuondolewa kama itafikia mahali Serikali ikaridhika na kuona kwamba inafaa kuchukua hatua kama hiyo, jambo ambalo ni utaratibu wa kawaida ambao hufanyika ndani ya Bunge, na kwa maoni yangu ni utaratibu mzuri kwa sababu Serikali inaonesha umakini na usikivu wa kile ambacho Wananchi wake wanajadili kupitia Wawakilishi wao ambao ni Waheshimiwa Wabunge.
Kwa mantiki hiyo pale itakapoonekana kwamba, maoni yale hayafai, Kanuni zinamruhusu Waziri husika kuuondoa Muswada huo ili kuufanyia marekebisho kwa lengo la kuuboresha zaidi, kwa hiyo si kosa na wala si ishara ya Wizara husika kushindwa kufanyakazi.

Kwa maoni yangu ni vyema vyombo vya habari vikazingatia Kanuni za Bunge pindi vinapokuwa vinaripoti juu ya maamuzi yanayofanywa na Bunge kuhusiana na masuala mbalimbali ili kuweza kuwatendea haki Watanzania na pia kuepusha migongano baina ya Mihimili ya Dola.

Ufafanuzi huu umetolewa jana tarehe 03 Februari 2010.

No comments: