-Achunguzwa kwa mahusiano na waliotimuliwa Bagamoyo
WAZIRI Mwandamizi katika serikali ya Rais Jakaya Kikwete, anahusishwa na sakata lililomsibu Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Jerry Muro, na sasa uchunguzi dhidi yake unaendelea, Raia Mwema limefahamishwa.
Habari za ndani ya Serikali zimeeleza kwamba vyombo vya dola vimeshitushwa na taarifa za kuhusika kwa waziri huyo ambaye taarifa zake zimekutwa kwa Muro na wenzake wawili Edmud Kapama na Deogratias Mgasa.
Kwa mujibu wa habari hizo, vyombo vya dola vilipowapekua na kuwahoji Muro na wenzake vilipata ushahidi wa waziri huyo kuwa na ‘mahusiano’ na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, waliotimuliwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Waliotimuliwa madarakani na Pinda ni Mkurugenzi Mtendaji Rhoda Nsemwa; Mweka Hazina, Michael Karol Wage; Ofisa Kilimo, Mifugo na Ushirika, Naftal Rhemtullah; Ofisa Mipango, Aloyce Gabriel na Mkaguzi wa Ndani, Abdul Mwinyi.
“Jerry Muro na wenzake walikutwa na ushahidi unaoonyesha kwamba waziri (anamtaja jina) alikuwa akinufaika na fedha za ubadhirifu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo. Walikuwa na ushahidi wa gari ambalo Waziri huyo amenunuliwa na liko Morogoro katika sehemu ya biashara zake,” kinaeleza chanzo cha habari serikalini.
Raia Mwema limefahamishwa kwamba vyombo vya dola kwa pamoja sasa vinachunguza jinsi waziri huyo (jina tunalo) alivyonufaika na fedha kutoka halmashauri hiyo ya Bagamoyo na sababu za mmoja wa watumishi hao kutoa fedha kwa waziri huyo.
“Unajua wanaangalia mahusiano kati ya Waziri huyo na mmoja wa watumishi waliofukuzwa kazi na Waziri Mkuu, maana lazima Serikali ijiridhishe walitoa fedha kwake kwa maslahi gani na kama wana mahusiano ya binafsi, kibiashara ama ya kikazi kabla ya kuchukua maamuzi na pia kina Muro na wenzake walizipataje hizo taarifa na walikuwa wanazitumia kwa malengo gani,” anaeleza Ofisa Mwandamizi serikalini.
Mbele ya Hakimu Gabriel Mirumbe wa mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Jerry Muro na wenzake wawili walishtakiwa kwa pamoja, wiki iliyopita, kwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 toka kwa Mweka Hazina wa Wilaya ya Bagamoyo, Wage, aliyefukuzwa kazi hivi karibuni na Waziri Mkuu kwa ubadhirifu.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Boniface Stanslaus akiwa na Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Benny Lincoln wamedai mahakamani hapo kwamba mshitakiwa wa kwanza na wa pili pia wanakabiliwa na shitaka la kujipachika wadhifa ambao si wao.
Inasemekana January 29, 2010 katika hoteli ya Sea Cliff washtakiwa walijitambulisha mbele ya Wage kuwa wao ni maafisa wa TAKUKURU wakati si kweli.
Mapema mwaka huu, Waziri Mkuu, Pinda, aliwavua madaraka viongozi watendaji hao wakuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, kwa kutowajibika ipasavyo na kutozingatia kanuni za fedha na ameteua wapya.
Pinda alitangaza uamuzi huo mjini Bagamoyo mwanzoni mwa mwaka huu kwenye mkutano na viongozi na watendaji wa Halmashauri hiyo, akiwa Waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Aliwavua madaraka watendaji wakuu hao kwa kutumia kanuni ya 37 ya Kanuni za Utumishi wa Umma za Mwaka 2003 na kusema hatua nyingine za kinidhamu zitafuatia kadri itakavyoonekana inastahili.
Baada ya kuwavua madaraka watendaji hao, aliwateua Samuel Saiyanga kuwa Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Halmashauri hiyo, akitokea Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma na Fidelis Nenetwa kuwa Mweka Hazina, akitokea Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga.
Wengine walioteuliwa ni Fidelica Myovelo, kuwa Ofisa Kilimo, Mifugo na Ushirika akitokea Halmashauri ya Wilaya ya Iringa; Felista Masamba kuwa Mkaguzi wa Ndani akitokea Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na Prudence Mtiganzi kuwa Mhandisi wa Maji akitokea Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero.
Alisema uamuzi wa kuwapumzisha watendaji hao unatokana na mapendekezo ya ripoti ya uchunguzi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Septemba na Oktoba mwaka jana.
Uchunguzi wa Mdhibiti ulitokana na tuhuma za ukiukwaji wa kanuni za fedha, uzembe wa kufuatilia utekelezaji wa miradi na ubadhirifu katika Halmashauri hiyo.
Ripoti hiyo ilibainisha ukiukwaji mkubwa wa kanuni za fedha, uzembe na kushindwa kuwajibika na matokeo yake kuzorota kwa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Waziri Mkuu alisema pamoja na kuwa hatua hizo zimechukuliwa kwa Bagamoyo, halmashauri zingine nchini zikae chonjo na zitashughulikiwa kwa kuwa nazo zina matatizo yanayofanana na ya Bagamoyo.
No comments:
Post a Comment