Thursday, February 18, 2010

Mkapa: Kuna mtu kanizomea?

RAIS mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amesema, hakuna Mtanzania anayeweza kudiriki kumzomea kwa kuwa rekodi ya utendaji wake kitaifa na kimataifa inaendelea kumlinda.

Mkapa amelakiwa kwa kishindo katika ziara ya siku moja wilayani Kilolo mkoani Iringa.

“Mmeona mapokezi yangu, kuna mtu yeyote amenizomea? Sijifichi na wala sikimbii kuzomewa, mimi niko ‘busy’ sana na shughuli za kimataifa baada ya kumaliza utumishi wangu serikalini,” amesema Mkapa.

Ameyasema hayo jana alipozungumza na wadau wanaonufaika na taasisi yake ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS Foundation wilayani hapa.

Alizungumza wakati wa majadiliano kuhusu hali ya Ukimwi nchini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Hospitali Teule ya Wilaya hiyo iliyopo Ilula.

Mkapa amesema, baada ya kumaliza urais wake amekuwa akijihusisha na shughuli mbalimbali za kimataifa zinazomfanya awe safarini muda mwingi akishughulikia uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine; mambo yanayohusu kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kuimarisha taasisi yake ili ishiriki vizuri zaidi katika mapambano ya Ukimwi unaotishia ustawi wa watu na taifa.

Amesema, wanaoishi na Virusi Vinavyosababisha Ukimwi (VVU) ni sehemu ya mapambano ya Ukimwi na hivyo wasiwe na hofu,wajiamini na waape kuishi maisha kama wengine.

Mkapa amesema, nchi inayoendelea ambayo nguvu kazi yake inapungua siku hadi siku kutokana na janga hilo, itakuwa ndoto kwake kupiga hatua za maendeleo.

“Ili tupambane vizuri na janga hili ni lazima tuwe tayari sasa kama nchi kubeba sehemu ya mzigo wa mapambano unaobebwa na wafadhili mbalimbali duniani kwasababu itafika siku watachoka,” amesema Mkapa.

1 comment:

Anonymous said...

FISADI MKUBWA HUYO HANA LOLOTE NA AKIJA DAR HUKU KWA WAJANJA TUNAMZOMEA, MBONA ANAKIMBILIA MIKOANI TU!