Friday, February 26, 2010

Aliyemshushua Mkapa sasa kutuzwa

-Ni Clare Short aliyeshupalia Tanzania kutoinunua

NYOTA ya Waziri wa zamani wa Uingereza wa ushirikiano wa kimaendeleo, Clare Short, aliyekuwa mstari wa mbele kupinga ununuzi wa rada ya Tanzania kiasi cha kutofautiana na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa inazidi kung’ara nchini na Raia Mwema imebaini kuwapo kwa maandalizi ya kumpatia tuzo mahsusi kama sehemu ya kutambua juhudi zake hizo ambazo zimebainika kuwa na maslahi kwa Watanzania.

Kama tuzo hiyo itatolewa, basi, itakuwa ya kwanza kutolewa kwa Waziri kutoka Ulaya. Claire Short alifikia hatua ya kutishia kujiuzulu wadhifa wake katika Bunge la nchini kwake ili kuonyesha msimamo wa kutetea wananchi wa nchi masikini kama Tanzania.

Mama huyo ndiye Waziri aliyeanzisha mzozo wa kupinga ununuzi wa rada hiyo katika Bunge la Uingereza, nchi ambayo ni mfadhili wa maendeleo ya Tanzania, na hasa bajeti ya Taifa ambayo zaidi ya asilimia 30 hutegemea wafadhili.

Hoja zilizokuwa zikitumiwa na Short katika kupinga ununuzi huo ni pamoja na rada hiyo kuuzwa bei ghali tofauti na thamani halisi lakini pia ubora wake kuwa ulikuwa ni wa kutia shaka. Rada hiyo ilinunuliwa kutoka Kampuni ya utengenezaji na uuzaji vifaa vya kijeshi ya Serikali ya Uingereza ya BAE Systems.

Uchunguzi wa Raia Mwema kwa wiki kadhaa sasa umebaini kuwa maandalizi ya utoaji tuzo hiyo yanafanywa na Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu Tanzania (LHRC), cha jijini Dar es Salaam kwa kushirikisha wadau wengine kadhaa wakiwamo wasomi mashuhuri nchini.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa maandalizi hayo, Mkurugenzi wa LHRC Francis Kiwanga hakuwa tayari kuthibitisha wala kukanusha lakini akiweka bayana msimamo wa kituo hicho kwamba hakiridhishwi na kusuasua kwa Serikali katika kuwachukulia hatua wahusika wa kashfa hiyo ya rada, ambayo kwa maneno yake ni kuwa “chenji iliyorejeshwa ni ushahidi wa kutosha” kuwashughulikia wahusika.

“Kuhusu kutoa tuzo kwa Clare Short siwezi kuzungumzia hilo kwa sasa lakini nikwambie tu kwamba tumekuwa na mtandao rasmi wa kushughulikia masuala kama hayo ya rushwa. Sasa hilo la rada ni sehemu ya hayo, ni suala mahsusi ambalo linafanyiwa kazi ya uchambuzi wa kina ili baadaye tuamue kwa pamoja tunafanya nini…kama suala la tuzo litajitokeza sawa au mengine,” alisema Kiwanga.

Lakini Raia Mwema limebaini, mapema wiki hii, kwamba mazungumzo ya NGOs kadhaa kuhusu suala la kumtuza Claire Short yameshaanza na yanatarajiwa kuhitimishwa karibuni.

Katika hatua nyingine Kiwanga alisema; “unajua kwenye hii nchi kuna tatizo la impunity yaani watuhumiwa waliofanya hata makosa ya wazi ya ufisadi wanalindwa na system licha ya kuwapo kwa ushahidi wa wazi.”

Lakini alipoulizwa kama anaweza kuwa na mifano ya kuthibitisha hilo hakusita kutaja kashfa za Richmond, akihoji kuwa kwa nini Mramba (Basil, waziri wa zamani wa fedha) afikishwe mahakamani kwa kuitia hasara nchi lakini wengine katika Richmond na rada waachwe.

Soma Zaidi

No comments: