WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amesema hana mawazo ya kuwania urais kwa kuwa ni kazi kubwa, ngumu, na yenye lawama.
Waziri Mkuu ametoa msimamo huo jana mjini Tabora, baada ya mshairi Ramadhan Katwila ‘ Mv Liemba’, kusoma shairi akimwomba Mungu kumjaalia awe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya Rais Jakaya Kikwete kumaliza ngwe yake mwaka 2015.
Pinda amesema hana hamu ya kuwa Rais, kwa sababu ni kazi ngumu tofauti na watu wanavyofikiri.
“Baba wa Taifa (Mwalimu Nyerere) alisema Ikulu si mahali pa kukimbilia, msifikiri kauli ile ni ya uongo.“Urais ni kazi ngumu. Hata hii kazi ya uwaziri mkuu ni ngumu sana, sema kwa vile tu ni lazima mzigo mzito akabidhiwe ‘Mnyamwezi’.
“Ni kazi ambayo kila mtu anakutupia lawama hata ambazo hustahili. Utasikia mwingine anasema kwanza liangalie lilivyo, kila siku utaandamwa na magazeti na kila mara utajikuta kwenye ‘The Komedi’,” alisema Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema atakuwa tayari kumuunga mkono mtu yeyote atakayejitokeza kuwania urais baada ya kipindi cha Rais Kikwete kumalizika.
Awali Mwenyekiti mstaafu wa CCM wa Mkoa wa Tabora, Juma Nkumba, alimwomba Mungu ampe rehema Rais Kikwete aweze kumteua tena Pinda kuwa Waziri Mkuu mara baada ya kushinda uchaguzi mkuu ujao.
Jana Waziri Mkuu alikagua bwawa na lambo la Imalamihayo ambalo linatumika kama kuogesha mifugo ya wafugaji wa eneo hilo.
Akihutubia wafugaji hao, Pinda aliwataka wapunguze idadi ya mifugo ili kufuga kisasa na kuongeza tija na faida.
Alisema wilaya ya Tabora ina ng’ombe 54,000 ambao ni wengi kulingana na eneo hilo na hivyo kuathiri malisho ya mifugo hao hatua ambayo inawafanya kukosa afya inayotakiwa.
Baadaye Waziri Mkuu alifungua sekondari ya Nkumba ambayo ni kwa ajili ya wakazi wa kata ya Uyui na ambayo inakabiliwa na uchache wa walimu, ukosefu wa maabara, umeme na maji.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Tabora Mjini, Siraju Kaboyonga, aliwachangia wafugaji wa Imalamihayo Sh 100,000 na kutangaza kujenga kisima cha maji shuleni Nkumba, hatua ambayo wananchi katika jimbo hilo walisema angeifanya mapema bila kusubiri ujio wa Waziri Mkuu.
2 comments:
Mizengo Pinda umesema ukweli, Urais wewe huuwezi. Tunashuhudia kila mara ukilalamika kuhusu adha mbalimbali kama serikali kumiliki magari ya kifahari bila kutoa suluhisho ukiwa kama Waziri Mkuu. Hakuna mahali ulishatueleza kuwa unawasiliana au kujadiliana na Raisi juu ys kuchukua uamuzi mzito wa kuyaondoa magari hayo kama walivyofanya Rwanda na hata Kenya.
Ni haki yako kuukata uraisi kwani uwezo wa kutoa maamuzi mazito bado huna.
Umeshindwa hata kusimamia utekelezaji wa maazimio karibu yote ya Bunge kuhusu Richmondi, Ikulu hapakufai. Haua uwazriri mkuu kwako bado naona ni shubiri, maana umekuwa mtu wa siasa zaidi kuliko utendaji. Labda uwanie Ukatibu Mkuu wa Chama au Makamu Mwenyekiti huko ndo kwenye porojo.
Wewe mtoa maoni unatafakari kabla hujasema? MH kaeleza toka moyoni ya nini kuanza kulalamika?Pinda ni waziri mkuu ambaye hajali kitu kinachoitwa fedha hata kidogo na kama angezitaka angekuwa tajiri kuliko mnavyoweza kufikiria
unasema ikulu hapawezi unajua kwa zaidi ya miaka 30 amekuwa pale kama kiongozi mwandamizi wa serikali?kama angekuwa hawezi kusimamia maamuzi yake angemaliza hata miaka mitatu?unajua alikuwa private secretary wa baba wa Taifa for how long? huyu jamaa ni moja ya vichwa hazina vichache sana vilivyobaki hapa Tanzania.
Post a Comment