TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
LEO, FEBRUARI 17, 2010
Sisi Muungano wa Asasi za Kiraia zinazotetea Usawa wa jinsia, haki za binadamu, maendeleo na ukombozi wa wanawake kimapinduzi (FemAct) pamoja na asasi zingine za kiraia tumekuwa tukifanya kazi kwa karibu na wabunge na Bunge la Tanzania kwa muda mrefu sasa. Tunatambua jitihada za muda mrefu za baadhi ya Wabunge pamoja na Bunge kwa ujumla katika kutetea haki na maslahi ya wananchi wa Tanzania. Tulifika hatua ya kuanza kuamini kwamba ukombozi wa Mtanzania unaweza kuletwa kupitia Bungeni.
Katika mkutano wa 18, Bunge lilikuwa litekeleze majukumu kadhaa ikiwa ni pamoja na kupata taarifa ya serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio 23 ya Bunge ya kashfa ya manunuzi ya kitapeli ya mitambo ya kufua umeme wa dharura ya Richmond LLC, mkataba mbovu wa ubinafsishaji wa Mgodi wa makaa ya mawe Kiwira, ukodishaji wa bandari kwa kampuni ya TICTS na mkataba mbovu wa ukodishaji reli ya kati (TRL). Mengine ni Bunge kupokea na kujadili taarifa ya kamati ya Bunge kuhusu uchafuzi wa mazingira na ukiuakaji wa haki za Binadamu mgodi wa North Mara na ukiukwaji wa haki za binadamu eneo la Loliondo wilaya ya Ngorongoro.
Mkutano huo wa 18 wa Bunge ulimalizika Ijumaa tarehe 12 Februari 2010. Tofauti na matarajio ya wananchi, Bunge limemaliza kikao chake bila ya kuchukua hatua madhubuti juu ya kashfa za Richmond, Kiwira, TICTS, TRL, Loliondo na North Mara. Jambo hili limetushtua na kutusikitisha sana. Tulitarajia Bunge kutimiza wajibu wa mamlaka na kazi za Bunge kama inavyoelezwa katika Katiba Ibara ya 63 (2 ), inasema;
“Sehemu ya pili ya bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya mwananchi, kuisimamia na kuishauri serikali ya jamhuri ya muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa katiba hii ”.
Sisi wananchi tunaona kuwa Bunge limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kuisimamia serikali, kutokana na mfumo mbaya wa madaraka na uwajibikaji kati ya serikali na bunge ambao unaruhusu maslahi ya chama tawala chukua hatamu kuliko maslahi ya wananchi wengi na taifa kwa ujumla. Wananchi wengi kupitia taasisi mbalimbali wameshatoa hoja kuhusu umuhimu wa kubadilisha huu mfumo huu mbaya wa utawala na utamaduni wa kisiasa unaolimbikiza madaraka kwa watawala na kuvuruga mgawanyo wa madaraka na uwajibikaji. Mapendekezo kadhaa yalikwishatolewa kiwa ni pamoja na kutenga baraza la mawaziri lisitokane na wabunge. Mfumo huu umedhoofisha demokrasia shirikishi ambayo ingewezesha wananchi na makundi yao kuwa na uwezo wa kuliwajibisha bunge,wabunge na madiwani. Aidha mfumo huu unalimbikiza madaraka katika serikali kuu na kudhoofisha uwezo wa madaraka kwenye serikali za mitaa ambako ndiko kwenye wananchi walio wengi.
Katika muktadha wa mfumo unaolimbikiza madaraka kwa walio wachache na kuvuruga uwajibikaji, ni vigumu kwa bunge kuiwajibisha serikali kama inavyotegemewa na wananchi walio wengi. Ndio maana bunge limefunika kisiasa kashfa za Richmond, Kiwira, TRL, na TICTS ingawakashfa hizi zimelisababishia taifa letu hasara kubwa ya mabilioni ya fedha na madhara makubwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwafanya wawe maskini na fukara zaidi.
Mabilioni ya fedha ya wananchi zilizopotea zingeweza kutumika kuboresha hali za wananchi. Kwa mfano;
oFedha zilizopotea katika kashfa ya Richmond ni shilingi bilioni 173 Kiasi hicho kingeweza kujenga nyumba 19,211 za walimu wa shule za msingi nchi nzima kwa gharama ya shilingi milioni tisa(9) kwa kila nyumba. Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM II 2007-2011) ulipanga kutumia sh bilioni 153 kwa ujenzi wa nyumba za walimu. Kwa hiyo fedha zilizopotea katika kashfa ya Richmond zingetosha na kubaki kujenga nyumba zote za walimu wa shule ya msingi kulingana na mahitaji yaliyopangwa na MMEM II ili kuboresha elimu ya msingi katika shule za umma nchini. Mpaka sasa serikali imeweza kutoa asilimia tatu (3%) tu ya fedha za ujenzi wa nyumba za walimu kiasi ambacho hakizidi shilingi bilioni tano.
oKiasi cha fedha kilichopotea katika kashfa ya Richmond, kingeweza kuwapatia chakula cha mchana wanafunzi 5,242,424 kwa Mwaka mzima kwa kasma ya shilingi 33,000 kwa Mwaka kama ilivyokadiriwa na mpango wa chakula duniani. Taifa lingeweza kuepusha mimba za utotoni mashuleni ambazo baadhi zinachangiwa na ukosefu wa chakula kwa wanafunzi mashuleni.
oKiasi hicho kingeweza kujenga zahahati zaidi ya 1,700 kwa gharama ya shilingi millioni 100 kwa kila moja na kuboresha huduma ya afya kwa wananchi vijijini na kwa makundi ya watoto, wazee na watu wenye ulemavu na kuepusha vifo vya wanawake katika uzazi ambao kwa sasa takribani wanawake ishirini na nne hupoteza maisha kila siku kutokana na sababu za uzazi.
Ni dhahiri kuwa mfumo wa utawala uliopo haukidhi haja ya kusimamia rasilimali za nchi yetu na kuwajibisha watawala kwa wananchi. Hivyo tunatoa wito kwa wananchi kutambua kuwa Tanzania sasa inahitaji mapinduzi makubwa na ya haraka katika mfumo wa uwajibikaji na uongozi na, muundo wa sera za utawala, siasa na uchumi. Uchaguzi Mkuu wa 2010 ni fursa pekee kwa wananchi kufanya mapinduzi yanayotarajiwa; kuchagua watu waadilifu na wanaoweka mbele maslahi ya taifa na wananchi. Wabunge wetu wa sasa wameshindwa kutetea na kulinda haki na maslahi ya taifa na wananchi.
Ni kutokana na haya tunayoyabaini, FemAct na Mitandao mingine tunapendekeza na kudai yafuatayo:
1)Bunge lijisafishe na kuanza kuangalia na kuweka maslahi ya taifa kuliko maslahi ya vyama na wabunge binafsi kutokana na kuogopa kutopitishwa na vyama vyao kugombea nafasi za ubunge majimboni.
2)Serikali iharakishe kuweka mazingira ya kuruhusu wagombea binafsi katika nafasi mbali mbali za uongozi wa kisiasa katika ngazi zote za utawala;
3)Mwaka huu wa uchaguzi mkuu, kila mpiga kura awe makini na kuchagua wagombea waadilifu na wasio wabinafsi ili kupata bunge litakalokuwa na uwezo wa kusimamia serikali na kutunga sheria kwa kuzingatia maslahi ya taifa
4)Wananchi kutambua kuwa wao ndio wana wajibu wa kuchagua wabunge wenye uwezo wa kuisimamia serikali ili iweze kuwachukulia hatua kali viongozi na watumishi wote wa umma ambao wanafanya ufisadi unaosababisha taifa kupoteza mabilioni ya fedha. Hivyo ni vema wananchi wakati wa uchaguzi wakaepuka kudanganyika kwa rushwa na hongo kama fulana,kanga, kofia, na vyakula, kwani kumpa mtu kura yako kwa rushwa ni kuweka rehani maendeleo yako na taifa.
5)Wasomi na matajiri wazalendo wajitolee kuchangia mawazo na maono mapya pamoja na rasilimali za kuwezesha mapinduzi na ukombozi wa wananchi dhidi ya ujinga, maradhi, umaskini na unyonge; na
6)Vyombo vya habari na makundi ya vuguvugu la mapinduzi ya jamii, kwa pamoja, waongoze mapinduzi mapya nchini Tanzania ili kuwe na uwajibikaji utakaoweza kubadilisha maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi.
Aidha, sisi kwa pamoja kama Asasi za Kiraia tumeamua kuchukua hatua zifuatazo;
(a)Kuandaa maandamano makubwa ya kitaifa kuonyesha kutoridhishwa na utendaji usioridhisha wa Bunge la sasa na kudai mfumo mbadala wa demokrasia shirikishi ambao una uwezo zaidi katika kutetea maslahi ya wananchi
(b)Kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili waweze kutambua mamlaka walioyo nayo katika kuwachagua na kuwafanya wabunge na viongozi kujali maslahi ya taifa na wananchi.
Mungu ibariki Tanzania
Imetolewa na kusainiwa na
1. FEMINIST ACTIVIST COALITION (FemAct)
2. CHAMA CHA WALEMAVU TANZANIA (CHAWATA)
3. TANZANIA NETWORK OF LEGAL AID PROVIDERS (TANLAP)
4. SAHRINGON TANAZANIA CHAPTER
5. MEDIA COUNCIL OF TANZANIA (MCT)
6. MTANDAO WA WAFUGAJI
7. TANZANIA COALITION ON DEBT AND DEVELOPMENT (TCDD)
17 Februari 2010
1 comment:
Wanaharakati nyinyi mnajuwa sheria na matukio yalivyo, Bunge sio Mahakama wao kama wajibu wao wameshatimiza na kukabidhi jukumu kwa Serikali ndio yenye kuwajibika kwa sasa, mnataka eti wabunge wawe ving'ang'anizi mpaka kieleweke, hivi hamkuona walivyolivalia njuga mpk hapo lilipofikia? Na ni kamati hizohizo za bunge ndio waliolipuwa hayo yote, sasa kama mnataka wangewavua hata ubunge sio jukumu la bunge wale wamechaguliwa na wananchi ktk majimbo yao. Au mnataka chama kiwavuwe uanachama ili mipasuko izidi?Jambo muhimu wanaharakati mujipange muendee majimbo ya hao mnaoona hawafai ili wasichaguliwe sio kupanga maandamano yasiyo na tija, nimeamini msemo wa Raisi kuwa kuna asilimia 15 hata ukifanya mazuri vipi hawatakusifia wao ni lawama tu, Kama tuna ubavu twendeni ktk majimbo tukajichaguwe wenye uadilifu!!Tukutane huko majimboni.
Msuya
Arusha
Post a Comment