WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameagiza uchunguzi kuhusu sakata la mwandishi wa habari, Jerry Muro, anayetuhumiwa kwa rushwa na kukutwa na pingu, ufanyike kwa kina na haraka ili ukweli ubainike, badala ya suala hilo kuendelea kuibua hisia mbaya miongoni mwa wananchi.
Pinda alisema jana bungeni kwamba binafsi hapendi suala hilo liendelee kwa muda mrefu, kwa kuwa linaweza kuanza kuleta hisia zisizo nzuri kwa wananchi.
Aliliambia Bunge kwamba amezungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mkuu wa Jeshi la Polisi na amehakikishiwa kwamba suala hilo halitachukua muda mrefu kumalizika.
Waziri Mkuu alitoa ufafanuzi huo bungeni baada ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohamed, kulifikisha jana katika chombo hicho cha kutunga sheria wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo.
“Kwa kauli nilizozipata tayari, nimezungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani, nimezungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi, nimehakikishiwa kwamba jambo hili wataliharakisha sana, vile vile kwa sababu linaweza kuleta hisia zisizo nzuri sana kwa wananchi, na tutajitahidi tuweze kulimaliza haraka,” alisema Pinda.
Pinda alisema mkanganyiko uliojitokeza ndani ya suala hilo ni namna ambavyo polisi walivyoanza kulishughulikia, hususan kuanzia kwenye vyombo vya habari na wakati huo huo Muro mwenyewe kutumia vyombo hivyo pia.
“Tatizo ninalolipata Mheshimiwa Hamad ni pengine namna jambo hili lilivyoanza kushughulikiwa, sababu tumekimbilia kwenye vyombo vya habari sisi tunaochunguza na yeye kama mtuhumiwa ametafuta vyombo vya habari na kuvitumia, kwa hiyo sasa ujumbe tunaowapa wananchi kwa ujumla unaweza ukatuchanganya sana,” alisema Pinda.
Alisema kutokana na mazingira hayo, ndiyo maana inabidi uchunguzi ufanyike na uwe wa kina, ili kubaini ukweli wa yale wanayomtuhumu ni kiasi gani na kiasi gani si kweli.
Katika swali lake la msingi Hamad ambaye pia ni Mbunge wa Wawi (CUF) alitaka kufahamu iwapo misukosuko anayopata Muro ambaye ni mwandishi wa kituo cha Televisheni ya Shirika la Habari Tanzania (TBC1), kama ni sehemu ya misukosuko wanayopata waandishi wa habari wanaofuatilia mambo mazito duniani hasa barani Afrika.
Hamad alisema kwa muda mrefu waandishi wengi wa habari wanaofuatilia mambo mazito ya nchi, hupata misukosuko sehemu mbalimbali duniani hasa katika Bara la Afrika.
Naibu Spika wa Bunge, Anne Makinda kabla ya kumpa nafasi Waziri Mkuu kujibu swali hilo la kwanza kuulizwa katika mfululizo wa maswali yaliyokuwa yamepangwa, alimwambia Hamad, “Bahati yako, halijaenda mahakamani.”
Pia Waziri Mkuu katika kujibu alianza kusema, “hili suala lingekwenda mahakamani jibu lingekuwa rahisi kweli.”
Katika majibu yake, alisema, “Labda niseme kwanza kwamba, binadamu alivyoumbwa ni kiumbe mwenye upungufu, hata kama angekuwa ana sifa nyingine zote, lakini tukubali tu kwamba atakuwa na upungufu.
Waziri Mkuu anao, Hamad anao, kwa hiyo na waandishi wa habari vile vile wanao upungufu wao kama binadamu.” Alisema ndiyo sababu zikawekwa sheria, kanuni.
“Sasa yaliyompata Jerry, kama binadamu na kama mtumishi mwingine yeyote, ni jambo ambalo linawezekana kabisa, yale anayotuhumiwa yanawezekana yakawapo, vile vile yasiwepo,” alisema Pinda.
Alisema kutokana na suala hilo kukimbiziwa kwanza kwenye vyombo vya habari na kujenga picha tofauti kwa wananchi, ndiyo maana upo umuhimu wa kufanya uchunguzi wa kina.
“Kwa hiyo mimi rai yangu ni kuwa uchunguzi fanyeni kama mnavyofanya uchunguzi mwingine wowote, utakapofikia mwisho itajulikana kama ni kesi ya kwenda mahakamani au hapana,” alisema Pinda.
Wakati huo huo, kwenye swali la nyongeza, Mbunge huyo wa Wawi alitaka kufahamu ni namna gani Waziri Mkuu anaweza kutumia nafasi yake kuhakikisha suala hilo linakwenda na kumalizika haraka kuepuka linavyoandikwa.
4 comments:
Mwandishi wa habari na pingu wapi na wapi? Anazitumiaje?Tuwe wakweli katika mambo mengine jamani japo ni mwandishi mwezetu.Tujaribu ku balance story zetu na si ushabiki.Tunaweza kujikuta tunaishi na mawakala wa majambazi katika nchi hii waliojificha kwenye migongo ya kazi zao au utendaji wao wa kazi.kwanini Tanzania tatizo la ujambazi halipungui japo kuwa serikali inatumia kila mbinu kukabili? Chombo cha habari ni silaha yenye uwezo mkubwa na ya hatari huhitaji bastola kiunoni wala pingu mfukoni, vya nini?
napenda kutoa rai kwa watanzania wenzangu kwamba maranyingi jambo lolote ambalo linaigusa jamii mara nyingi mtizamo wa waliowengi huwa ni mmoja.na radiamali zao pia huwa ni za kufanana maana kama mtu huwa akiamin kwamba yeye yu sahihi basi ni vigum sana kuweza kumbadilisha msimamo wake.na si vyema kuhukumu wakat huna vithibitisho ila wakat mtu mwenye mamlaka anapotoa rai juu ya jambo fulani ni vyema kutoegemea upande wowote ili kutoa taswira chanya kwa wananchi.si vyema kukurupuka na kusema eti fulan anahatia lakin huyu mwenzie hana hatia wakati haujatoa vigezo vya kumfanya umtie mtu hatian.tukumbuke kwamba watanzania tunautashi na tukielezwa jambo kwa ufafanuz tunaelewa bali sio kukurupuka tu na kusema watanzania wanauelewa mdogo hii ni dhihaka kubwa sana.
Mdau
Naunga mkono kwamba swala la Jerry lifanyiwe uchunguzi kuliko kulumbana kwenye vyombo vya habari.
Tunasubiri mchawi ni nani?
what goes around comes around
Hao jamaa wanambambikia kesi huyo jamaa,kwani polisi tushawazoea kuwabambikia kesi wananchi hususani wanapoona maslahi yao yanapoguswa,na hilo sakata limeundwa pia na wakubwa wa jeshi hilo,kwani polisi huwa hawali peke yao.
Chris
Post a Comment