WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda ameshtushwa na swali lililomtaka kutoa maelezo ya kwa nini Serikali inahofu kukubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyobariki mgombea binafsi.
Swali hilo liliulizwa jana na mkazi wa kijiji cha Ibushi, Joseph Mazwazwa, mara baada ya Pinda kukagua bwawa linalotumika kwa shughuli mbalimbali za binadamu, wanyama na kilimo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kwa nini Serikali inahofia kuwapo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu ingawa Mahakama Kuu ilishabariki kuwapo kwa mfumo huo katika uchaguzi?,” aliuliza.
Waziri Mkuu alimjibu kwa kusema, ni kweli Mahakama Kuu ilibariki mgombea binafsi baada ya kesi ya suala hilo kuwasilishwa mahakamani hapo.
Alisema hata hivyo suala hilo linaleta utatanishi kutokana na tafsiri ya kikatiba, kwa kuwa Katiba inasema mgombea katika nafasi za kisiasa, kama diwani, Mbunge na Rais, ni lazima atokane na chama cha siasa kilichosajiliwa.
Alisema, hatua hiyo ndiyo inayoleta utata kwa Serikali kukubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuruhusu kuwapo kwa mgombea binafsi.
“Ni sababu hizi hasa ndizo ambazo zimetufanya kupinga uamuzi huu wa Mahakama. Hata hivyo wenzetu bado wanataka mfumo huu uwepo na ndiyo maana wamekata rufaa katika chombo cha juu ambacho ni Mahakama ya Rufaa ili mfumo huu uruhusiwe.
“Hata hivyo kesi hii kwa ngazi ya Mahakama ya Rufaa bado haijatolewa uamuzi, kwa hiyo ni vigumu kueleza. Mahakama ya Rufaa ikibariki uamuzi huu basi hatutakuwa na la kufanya itabidi tukubaliane na matokeo katika suala hili,” alisema Waziri Mkuu.
Kesi ya kutaka Mahakama kukubaliana na kuwapo kwa mfumo wa mgombea binafsi, ilifunguliwa katika Mahakama Kuu na Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila na Mahakama hiyo iliamuru mfumo huo kuanza kutumika, lakini Serikali ilikataa kutekeleza amri hiyo ya Mahakama.
Hata hivyo katika siku za karibuni wanaharakati wamekuwa wakishinikiza Serikali ikubali mfumo huo kwani tayari kuna uamuzi wa Mahakama wa kuuruhusu, hata kama Mahakama ya Rufaa itakuwa bado haijatoa uamuzi kwa suala hilo.
1 comment:
Hata mimi sioni sababu ya serikali kuogopa mgombea binafisi, mahakama ilishatoaga hukumu nashangaa serikali inasubiri nini kutekeleza, sioni utawala wa sheria hapa hata kidogo!!!
Post a Comment