Monday, February 22, 2010

Mizengo Pinda ambeba Rostam Aziz


WAZIRI Mkuu Mizengo Kayanza Peter Pinda amewashauri wananchi wa Jimbo la Igunga mkoani Tabora wasimkatae Mbunge wao Rostam Aziz wakati wa uchaguzi mkuu ujao kwa kusikia maneno yanayosemwa bungeni, badala yake wazingatie kile alichowafanyia.

Wakati Pinda anampigia debe Mbunge huyo jana kwenye mkutano wa hadhara katika uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, baadhi ya wananchi wa jimbo hilo walimwomba Waziri Mkuu amshinikize Mbunge wao abaki jimboni humo, kwa madai kuwa haonekani.

Wananchi hao walitoa ombi hilo ili waweze kupata fursa ya kumweleza kero zao na awaeleze yanayosemwa bungeni kuhusu yeye (Rostam).

Mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Moka Changalawe alimweleza Pinda kuwa kukosekana kwa Mbunge jimboni kwa muda mrefu kumesababisha baadhi ya viongozi kuwanyanyasa wananchi kwa kuwabambikia kesi za uongo, zikiwemo kutishia kuua.

Hata hivyo, Pinda katika hotuba yake, alisema kama kuna manyanyaso na ubabe kwenye halmashauri hiyo, ni vitendo vya kuchochea rushwa na serikali imejipanga kuondoa tatizo hilo.

Hata hivyo hakujibu ombi la wananchi hao la kumwomba Mbunge huyo kubaki jimboni humo. Pinda juzi mara baada ya kuwasili mjini hapa alizungumza na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Igunga na kuwaomba wasimkatae Mbunge huyo.

“Tunaelekea katika uchaguzi mkuu ujao baadaye mwaka huu. Naomba mtakapokuwa mnachagua viongozi wenu mzingatie wamewafanyia nini iwe ni katika nafasi ya udiwani au ubunge.

“Iwapo mnataka kumchagua tena Rostam zingatieni amewafanyia nini katika ubunge wake. Msisikilize kile kinachosemwa bungeni juu yake. Bunge lina mambo yake, mimi kama Waziri Mkuu nafahamu mambo ya pale bungeni,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema iwapo wananchi wa Igunga wanaridhishwa na namna Mbunge wao anavyowatatulia matatizo yao ya kimsingi wana hiari ya kumchagua tena kuendelea kuwa Mbunge bila kusikiliza nini kinasemwa juu yake.

Ingawa Waziri Mkuu hakufafanua zaidi ni maneno gani ya bungeni ambayo yamekuwa yakisemwa juu ya mbunge huyo, Rostam ni miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa wakihusishwa na kampuni ya Richmond iliyoingia mkataba tata na Shirika la Umeme (Tanesco).

Wakati wa kuhitimisha mjadala bungeni juu ya suala la Richmond katika mkutano wa 18 wa Bunge ulioahirishwa hivi karibuni mjini Dodoma, Spika Samuel Sitta alisema suala hilo limekwisha isipokuwa amebakiwa na kazi ya kumsihi Rostam aachane na mawazo ya kutaka liundwe jopo la majaji kuichunguza ripoti ya kamati teule iliyochunguza na kuwasilisha bungeni taarifa ya Richmond.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alionya tabia ya viongozi kujenga uhasama baina yao kwamba hatua hiyo inawafanya kutumia muda mwingi katika kugombana badala ya kuwatumikia Watanzania masikini.

Alisema serikali haitavumilia kuona viongozi wanatumia muda mwingi katika ugomvi wakati Watanzania wanakabiliwa na matatizo mbalimbali ukiwewo umasikini.

“ Kama kweli tunataka kuwahudumia wananchi masikini hawa ni lazima tuwe na ushirikiano sisi viongozi kwanza. Idadi yetu sisi Watanzania ni kama milioni 40 hivi au na zaidi kidogo. Hata hivyo asilimia 80 ni wakulima na asilimia 20 ndio sisi viongozi.

“Iwapo sisi asilimia 20 tutajali zaidi maslahi yetu na kuwasahau hawa masikini ipo siku hawa watu watatupiga marungu,” alisema Waziri Mkuu.

Alisema viongozi wa serikali wanawajibika kutumia fedha wanazozipata katika kuwasaidia masikini wanaowaongoza badala ya kujilimbikizia fedha huku wakizungukwa na watu masikini jambo ambalo ni hatari.

1 comment:

Anonymous said...

Kwa mtaji huo hapo tusigemee suala la RICHMOND tena kuchukuliwa hatua, wanatuchezea maigizo tu hao na kutufanya sie punguani ila yana mwisho hayo tutapambana kwenye uchaguzi mkuu 2010