MABALOZI wa amani waliounda umoja ujulikanao kama Amani Forum wamewakosoa wanaharakati wanaoandaa maandamano dhidi ya Bunge kwa kusema kitendo hicho ni choko choko zinazoashiria uvunjifu wa amani unaofanywa na watu wenye maslahi binafsi.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema ambaye ni mmoja wa wajumbe pamoja na Katibu wa Umoja huo, Risasi Mwaulanga wameliambia gazeti hili kwamba kesho watahutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, waliouandaa ambao pamoja na masuala mengine, wamesema wataufafanulia umma madhara ya tamko la wanaharakati hao dhidi ya bunge.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili, mabalozi wa Amani Forum ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Afrika Mashariki, Dk Walid Kabourou, Mrema na Mwaulanga walisema tamko hilo la wanaharakati ni miongoni mwa viashiria ambavyo vimeanza kuonekana yakiwemo maneno ya chini chini ya kuvunja amani ya nchi.
Katibu wa Amani Forum, Mwaulanga alisema katika mkutano wa hadhara wa kesho ambao ni wa kwanza kufanyika tangu umoja huo uzinduliwe rasmi mwezi uliopita, mabalozi hao wamesema watahakikisha wanaueleza umma pia athari za maneno ya chini chini ambayo yamekuwa yakijitokeza kuhusu masuala ya dini.
Mwaulanga alisema wanaharakati na vyama vya siasa, vimekuwa vikitoa mfano wa Marekani katika harakati zao lakini vikishindwa kubaini kwamba wao hufanya mambo kwa maslahi ya nchi na maendeleo.
Alisema katika kuhakikisha kuwa umma unaelewa ukweli wa mambo juu ya suala zima la kulinda amani, Amani Forum mwezi ujao itafanya mikutano mingine miwili Dar es Salaam katika maeneo ya Manzese na Buguruni kabla ya kuhamia kwenye mikoa aliyoitaja kwamba ni yenye utata.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Mara, Arusha, Mwanza, Mbeya na ya Kusini. “Uamuzi wa wanaharakati hauna chochote zaidi ya kujenga hisia za chuki na wananchi kutoiamini serikali na bunge lao,” alisema Mwaulanga na kusisitiza kwamba badala ya kuandamana, wangekwenda kujipanga wachaguliwe wabunge wanaoendana na matakwa wanayohitaji na si kuandaa maandamano nchi nzima.
Mwaulanga ambaye maoni yake yaliungwa mkono na Mwenyekiti wa TLP, Mrema, alisema kupitia wanaharakati, wanaweza kujipitisha watu wengine wenye malengo maalumu ya kiuchumi au kisiasa wakapitisha maazimio kwa wananchi yanayoweza kuiingiza nchi kwenye mgogoro.
Katibu huyo wa mabalozi wa amani ambaye alisema mkutano wa kesho utazungumzia pia mauaji mkoani Mara, alisema wanaharakati walipaswa waandamane kupinga ukatili kama uliojitokeza hivi karibuni wa watu 17 wa ukoo mmoja kuuawa katika Kijiji cha Buhare, Mara na si kujielekeza kwenye mambo ya kisiasa.
“Umeona hizi taasisi zisizo za kiserikali, zimetangaza maandamano yasiyoisha nchi nzima. Sasa yale maandamano ingawa yanaweza kudaiwa ni dhidi ya bunge, si wangeyafanyia Dodoma bunge linapokuwa pale.
Lakini unaposema ni maandamano nchi nzima, ni dalili kwamba yanapinga serikali nzima,” alisema Mrema. Mrema alisema, “ukishasema maandamano ni nchi nzima, ni dhahiri polisi itakataa. Wakishakataa si dalili ya mgogoro umeanza.
Soma zaidi
1 comment:
Ndhani hao Mabalozi wa amani sasa wanaelekea pabaya, sikutegemea figures zilizomo humo especially Mrema kusema hayo nadhani anaanza kujipendekeza kwa serikali sasa, wabunge wenyewe wameliona hili na wamekiri udhaifu.
Post a Comment