SAKATA la wabunge kuhusishwa na rushwa limeingia sura mpya, baada ya
Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe kuhojiwa na chama chake
cha Chadema kwa saa tatu jana.
Wakati Zitto akihojiwa, kambi rasmi
ya upinzani bungeni, iliwataja wabunge saba wa CCM na kueleza kuwa ndiyo
wanaolichafua Bunge kwa kujihusisha na mambo yenye maslahi binafsi
wakiwa watumishi wa umma.
Kadhalika, Naibu Spika wa Bunge, Job
Ndugai alisema kwamba Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru)
ilikuwa ikiendelea kuwahoji baadhi ya wabunge kuhusu tuhuma za rushwa na
kwamba uchunguzi ukikamilika taarifa zitawekwa wazi.
Zitto
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya
Umma (POAC) na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, jana aliandika katika
ukurasa wake wa mtandao wa Tweeter kwamba alihojiwa na Sekretarieti ya
chama chake kutokana na tuhuma za rushwa zinazowagusa badhi ya wabunge.
Katika
maelezo yake, Zitto alisema aliiambia sekretarieti ya chama hicho
kwamba Chadema kifanye uchunguzi ili kubaini ukweli wa suala hilo na
kwamba yuko tayari kuwajibika ikiwa itathibitika kwamba alihusika kula
rushwa.
“Kwa saa tatu nimejieleza mbele ya sekretariati ya chama
kuhusu tuhuma za rushwa dhidi yangu. Niliomba kutaka kutoa maelezo kwa
Katibu Mkuu, nimekiomba chama kufanya uchunguzi na ikibainika hatua
zichukuliwe,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo kwenye Tweeter.
Lissu ataja wengine
Kwa
upande wake, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo, Tundu Lissu aliwataja wabunge
wa CCM ambao wanatuhumiwa kuwa ni Nasir Abdallah (Korogwe Mjini),
Mariam Kisangi (Viti Maalumu), Vicky Kamata (Viti Maalumu) na Charles
Mwijage (Muleba Kaskazini) ambao hata hivyo, wote wamekanusha madai
hayo.
Wabunge wengine watatu tumeshindwa kuwataja kwa kuwa hawakupatikana kuzungumzia tuhuma dhidi yao.
Katika
orodha hiyo wamo wawili wa Viti Maalumu na mmoja wa jimbo na Lissu
alidai kwamba wamekuwa wakishiriki vikao vya Kamati ya Nishati na Madini
huku wakijua kuwa wana maslahi binafsi na wengine kutumia fursa hiyo
kujinufaisha.
“Kwa takriban juma moja sasa kumekuwa na mjadala mzito
wa ufisadi hapa bungeni, sasa Kambi Rasmi ya Upinzani imejitathmini na
kuona kwamba wabunge wake hasa walioko kwenye Kamati ya Nishati na
Madini iliyovunjwa, John Mnyika, David Silinde na Mwanamrisho Abama
hawahusiki,” alisema Lissu na kuendelea:
“Ila uchunguzi wetu
umefanikiwa kupata majina ya wabunge wanaohusika moja kwa moja na
mgongano wa kimaslahi ambao tunaona tuwataje kwa maslahi ya umma.”
Lissu
alikwenda mbali zaidi na kutaja tuhuma zinazowahusu wabunge hao akisema
wawili ambao gazeti hili halikuwaja, wamejihusisha kufanya biashara na
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) hivyo wana mgongano wa kimaslahi.
Alisema
Mwijage ana mgongano wa kimaslahi katika mchakato mzima wa kuipa zabuni
ya kusambaza mafuta kampuni ya Puma Energy kwa kuwa yeye ni mtalaamu
mwelekezi wa kampuni hiyo inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 50.
“Nasir
Abdalah na Mariam Kisangi; Hawa wanamiliki vituo vya mafuta. Sasa kwa
namna yeyote ile kuwa wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini hawawezi
kutenda haki katika mchakato wowote unaohusu suala la mafuta,” alisema
na kuendelea;
"....(jina limehifadhiwa) hana mgongano wa moja kwa
moja wa maslahi, lakini kwa kadri tunavyofahamu, yeye ndiye aliyekuwa
akiyafanyia kampeni ya kupata zabuni makampuni ya mafuta ya Oryx na
Camel na ....(jina limehifadhiwa), suala lake ni complicated kidogo.
Maslahi aliyonayo katika suala hilo ni kuwa ana uhusiano wa Kimapenzi na
kigogo mmoja katika Wizara ya Nishati na Madini.”
“Hawa ndiyo
wajumbe wa Kamati ya Nishati na Madini ambao sisi Kambi ya Upinzani
tunawafahamu kuwa ndiyo waliojihusisha na mgongano wa kimaslahi.
Tumewaangalia wabunge wetu wote watatu hawamo ila kama kuna mtu ana
taarifa zinazowahusu, aseme na tutazifanyia kazi.”
Lissu alisema
kitendo cha wabunge kujihusisha na mgongano wa kimaslahi na taasisi za
umma ni kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995
na ni kinyume na maadili ya kibunge.
Katika hatua nyingine Lissu
amemshauri Spika wa Bunge Anne Makinda kuzivunja pia kamati za Bunge za
Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Mashirika ya Umma (POAC) akisema
nazo zina madudu mengi.
“Hili lisiishie tu kwa kuvunja Kamati ya
Nishati na Madini, tunataka pia kamati za POAC na LAAC zivunjwe,
uchunguzi ufanyike na wahusika waitwe kujitetea na hatimaye wenye hatia
watajwe hadharani bungeni na majina yao yachapishwe kwenye magazeti ili
haki itendeke,” alisema.
Alipoulizwa Chadema imefanya nini dhidi
ya Mbunge wake, Zitto Kabwe kutajwa katika orodha hiyo, alijibu: “Nikiri
kwamba sisi taarifa tunazo ila hatujamwita kumwuliza. Naomba ieleweke
kwamba kama chama au Kambi Rasmi ya Upinzani hatuna maslahi na mbunge
yeyote anayeonekana kujihusisha na masuala hayo.”
“Katika hili
tunaomba uchunguzi ufanyike na matokeo yake yatangazwe ili tupate msingi
wa tuhuma hizo na ninaahidi kwamba tutazifanyia kazi ipasavyo.”
Majibu ya tuhuma
Alipotakiwa
kuzungumzia tuhuma hizo, Kisangi alikiri kumiliki kituo cha mafuta
lakini akasema sheria haimzuii mtu kama mambo yake anayafanya kwa uwazi.
“Nimekuja
bungeni nikitokea kwenye ualimu, nilikuwa nafundisha Shule ya Msingi ya
Mianzini na biashara hii ni ya familia. Inaendeshwa kwa uwazi na
mwanangu wa kwanza ndiye anayeisimamia. Kutokana na uwazi katika
shughuli zangu, mwaka jana Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma
ilinipongeza. Mimi ni msafi na siko huko wanakofikiri wao (Chadema).”
Kwa
upande wake, Mwijage alikanusha kuwa mtaalamu mwelekezi wa Kampuni ya
Puma, badala yake akasema ni mtaalamu wa petroli anayefanya kazi ya
kuishauri Serikali kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu nishati hiyo.
"Siyo
kweli, hawa wanadandia hoja. Mimi ni mtaalamu wa petroli ambaye mchango
wangu kimsingi una faida kubwa bungeni na hata kwa jamii kwa ujumla.
Sijafanya maamuzi yeyote ya kulihujumu taifa hili na hata kwenye Bajeti
ya Wizara ya Nishati na Madini pekee, nilitoa mchango wa kurasa 10
kuhusu masuala hayo ya petroli,” alisema
Aliishauri kambi hiyo ya
upinzani kuvuta subira, akieleza kuwa jambo lililoko bungeni linahusu
ufisadi na uhujumu uchumi hivyo kauli zinazotolewa bila utafiti zinaweza
kuvuruga mchakato mzima uliokwishaanzwa na Kamati ya Maadili ya Bunge.
Awali,
Abdallah alipoulizwa kuhusu tuhuma za kumiliki vituo vya mafuta hivyo
kuwa na maslahi binafsi, alicheka na kuahidi kwamba angepiga simu
baadaye, lakini hakufanya hivyo na alipopigiwa baadaye alikata simu.
Hata hivyo, alizungumza na waandishi wa habari na kukanusha kumiliki
vituo vya mafuta.
Kamata kwa upande wake alisema: “Kuna kamati
maalumu imepewa kazi ya kuchunguza mambo hayo, hivyo yote yanayoulizwa
yatakuwa wazi na ukweli utajulikana tu. Nina maslahi au sina ukweli
mtaujua, haraka ya nini?.
Mjadala Bungeni
Mjadala huo wa
wabunge kuhusishwa na mgongano wa kimaslahi ulianza kulipuka bungeni
jana asubuhi baada ya wabunge watatu; Joshua Nassari (Arumeru
Mashariki), Salum Barwany (Lindi Mjini) na Mbunge wa Nkasi Kaskazni, Ali
Kessy kutaka wabunge wanaotuhumiwa kwa ufisadi watajwe bungeni ili
kuisafisha taasisi hiyo ya kutunga sheria.
"Mheshimiwa Naibu
Spika juma lililopita Mheshimwa (Vita) Kawawa alitoa hoja kutaka suala
la ufisadi lishughulikiwe kwa kuvunjwa Kamati ya Madini na Spika
akaridhia na kulipeleka suala hilo kwenye Kamati ya Maadili. Kwa nini
Kamati nyingine zilizohusishwa na ufisadi huo nazo zisivunjwe?” alihoji
Nassari na kuendelea:
“Kuna Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(LAAC) inayoongozwa na Mheshimiwa Mrema na Kamati ya Mashirika ya Umma
(POAC) inayoongozwa na Zitto. Kuna tabia ya wabunge kuzikimbia kamati
zisizokuwa na mikataba kama Kamati ya Huduma za Jamii na wanazikimbilia
kamati zenye mikataba.”
Barwany alitaka Bunge litajiwe majina ya
wabunge waliotuhumiwa kwenye kashfa hiyo mpaka wakapelekwa kwenye Kamati
ya Maadili, akieleza kuwa hili litasaidia kulisafisha... “Tumeambiwa
Kamati ya Maadili inajadili suala hilo, lakini hatujatajiwa ni wabunge
gani waliopelekwa huko, tunaomba mtutajie ili Bunge lijisafishe.”
“Mimi
naungana na wazo la Barwany na Nassari. Majina yatajwe wabunge
tunadhalilishwa na wananchi huko mitaani. tuwataje hadharani,’ alisema
Kessy.
Akitoa mwongozo wa hoja hiyo, Ndugai aliiagiza Kamati ya
Uongozi ya Bunge kutoka kwenye ukumbi wa Bunge ili wakajadili suala hilo
na baadaye apelekewe taarifa.
“Naamini wenyeviti wote wa kamati mmo
humu ndani, naomba sasa hivi mwende kwenye Ukumbi wa Spika mkajadili
suala hilo halafu nipate majibu sasa hivi,” alisema.
Baadaye jioni, Ndugai alisema kuwa Spika hawezi kuwataja kwa majina wabunge ambao wanajihusisha na rushwa kwa kuwa hawajui.
Alisema
Kamati ya Uongozi iliyokutana jana mchana ilikubaliana kuwa ufanyike
uchunguzi wa kina kwa ajili ya kuwabaini wale wanaoshukiwa na kwamba
ikibainika Bunge litawaanika hadharani.
“Kamati imerejea
kumbukumbu za hansard ya Jumamosi kuwa ufanyike uchunguzi wa kina juu ya
jambo hilo na wabunge mtaitwa kwa ajili ya kutoa ushirikiano, ikumbukwe
kuwa mbunge akiitwa siyo kwamba ndiyo amekuwa mtuhumiwa, bali pale
itakapothibitika majina yatawekwa hadharani,’’ alisema Ndugai.
Naibu
Spika alitahadharisha kuwa ndani ya Kamati hiyo utafanyika uchunguzi wa
kutosha kubaini kama kuna mjumbe mwenye maslahi kwa wale wahusika basi
ataondolewa ili kutoa nafasi kwa kamati kufanya kazi yake ipasavyo.
Aliwatahadharisha
wabunge kuwa Kamati hiyo haitaingilia utaratibu wa vyombo vya dola
ambao wamekuwa wakiufanya ikiwemo wa Takukuru wa kuwahoji baadhi ya
wabunge.
No comments:
Post a Comment