Thursday, July 5, 2012

BoT yavunja ukimya mabilioni ya Uswisi

Na Ramadhan Semtawa
WAKATI Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina akiibua tuhuma nzito za kuwapo wanasiasa na wafanyabiashara walioficha kiasi cha Sh 11.9 trilioni nchini Uswisi, Benki Kuu (BoT) imesema haijapata ripoti hiyo.

Juzi, Mpina wakati akichangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi, Mipango na Utawala bora), alitoa taarifa hizo akinukuu kilichomo katika Ripoti ya ‘Global Financial Integrity (GFI)’ ya mwaka 2008, ambayo ilionyesha kiasi hicho cha fedha kufichwa nje na kuituhumu BoT kwamba inayo ripoti hiyo lakini imeshindwa kuueleza umma na kuwataja watuhumiwa.

Jana, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema benki hiyo haikuwa imepata ripoti hiyo na kusema ni vyema mbunge huyo akasaidiana na vyombo vya dola ili viifanyie uchunguzi.

“Sisi hatuna hiyo ripoti. Siyo kila kitu ambacho mwingine anaweza kukisoma basi na sisi tunacho. Lakini, kama anayo (Mpina), basi asaidiane na vyombo vya dola kwani tayari vimeanza uchunguzi wa kiasi kingine kilichoelezwa awali,” alisema Profesa Ndulu.

Alisema Uswisi siku zote imekuwa ikificha taarifa za wateja wao hivyo kuiwia vigumu BoT na wakati mwingine hata vyombo vya dola kusaka fedha zinazotuhumiwa kufichwa nje kinyume na taratibu husika za nchi.

Profesa Ndulu alisema hata uchunguzi wa vyombo vya dola unaofanywa sasa utafanikiwa endapo tu wenzao wa Uswisi watatoa ushirikiano, lakini kinyume chake unaweza kuwa mgumu na kutofikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alisema kwa sasa BoT haiwezi kuhusika na uchunguzi huo kwani vipo vyombo vya dola huku akitaja Kitengo cha Kuzuia Fedha Chafu (Financial Intelligence Unit- FIU), ambacho ndicho chenye dhamana ya kushughulikia tatizo hilo.

Mpina ashangaa
Jana, Mpina alipoelezwa kwamba BoT imesema haina taarifa hiyo, alionyesha kushangaa na kusema ni kitu ambacho ni vigumu kukielewa kwani ripoti imetajwa katika Bajeti ya Mipango ingawa ilionyesha kiasi cha fedha kinachotoroshwa kutoka Afrika na si Tanzania.

Alishikilia msimamo wake kwamba BoT lazima ifahamu ripoti hiyo kwani ndicho chombo cha nchi kinachofahamu kila mtu mwenye akaunti za fedha za kigeni nje ya nchi.

“Haiwezekani BoT iseme haina taarifa. Wao ndiyo wanahusika na kujua nani ana akaunti nje ya nchi. BoT ndiyo inajua akaunti zote za Watanzania zilizopo nje ya nchi, sasa wakisema hawajui inamaanisha nini? Hili jambo limetajwa katika Bajeti ya Mipango iweje BoT isijue?” alihoji Mpina.

Mpina alisema kiasi hicho kimetoroshwa nchini taratibu hivyo, BoT na mamlaka nyingine za dola haziwezi kukwepa kufahamu kiasi hicho cha fedha.

Alisema hivi karibuni Benki ya Dunia (WB) ilianzisha mpango wa Stolen Asset Recovery Initiative StAR (Juhudi za  Kurejesha Mali na Fedha Zilizoibwa) na kuongeza kwamba juhudi hizo zinafanya kila nchi na taasisi kama BoT kufahamu fedha za watu wake zilizofichwa nje.

“Benki ya Dunia ni chombo kikubwa cha fedha, sasa iweje BoT waseme hili hawalifahamu? Wao wanafanyaje kazi kuhakikisha wanabaini fedha zilizopo katika akaunti za nje za Watanzania? Kuna Mtanzania anaweza kuweka fedha ng’ambo bila wao kujua? Wanapataje pia taarifa za fedha kama mipango kama hii au ripoti Financial Integrity hawaifahamu?"

Sehemu ya ripoti hiyo ya Global Financial Integrity inaonyesha kwamba kumekuwa na ongezeko la kiasi cha fedha kinachotoroshwa katika nchi mbalimbali duniani kutoka Dola za Marekani 1.06 trilioni za mwaka 2006 hadi kukaribia Dola 1.26 trilioni za mwaka 2008.

Katika kiasi hicho cha fedha, wastani wa Dola 725 bilioni hadi 810 bilioni zilitoroshwa kwa mwaka tangu mwaka 2000 hadi 2008 kutoka katika nchi zinazoendelea.

Ripoti hiyo inaonyesha pia kwamba, Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini, zinaongoza kwa asilimia 24.3, nchi zinazoendelea za Ulaya asilimia 23.1, Afrika asilimia 21.9 na Asia asilimia 7.85.

Katika ripoti hiyo, nchi 10 zinazoongoza duniani kwa kuwa na kiwango kikubwa cha fedha kilichotoroshwa kati ya mwaka huo 2000 hadi 2008 na kiasi katika mabano ni China (Dola 2.18trilioni), Russia (Dola 427bilioni), Mexico (Dola 416 bilioni), Saudi Arabia (Dola 302bilioni), Malaysia (Dola 291bilioni), Umoja wa Falme za Kiarabu (Emirates, Dola 276 bilioni), Kuwait (Dola 242bilioni), Venezuela (Dola 157bilioni), Qatar (Dola 138bilioni) na Nigeria (Dola 130bilioni).

No comments: