HOTUBA
YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA VINCENT JOSEPHAT
NYERERE (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA
2012/2013 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
(Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Kwa
niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, napenda kuchukua fursa hii
kuwasilisha maoni yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara
ya Mambo ya Ndani ya nchi kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, napenda
kuwashukuru askari wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza wanaoishi
Kambi iliyoko katika Kata ya Mkendo kwa kunichagua kuwa Diwani wao. Vile
vile, nawashukuru wananchi wote wa vyama vyote na dini zote Jimbo la
Musoma Mjini kwa kunichagua kuwa Mbunge na mtetezi wao. Pia napenda
kumshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa imani yake
kubwa kwangu kwa kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi katika Wizara hii.
Kwa upekee kabisa, Mheshimiwa Spika, kwa wanaoeneza propaganda kwamba
CHADEMA inachukia au kudharau askari polisi wetu, naomba nitoe shukrani
zangu kwa mke wangu Helen V. Nyerere ambaye pia ni askari wa Jeshi la
Polisi.
UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI
Mheshimiwa Spika,
Katika
mwaka uliopita wa fedha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji
matukio mbali mbali ya mauaji ya raia yaliyowahusisha askari wa Jeshi la
Polisi pamoja na wa vyombo vingine vya dola. Aidha, tulihoji matukio
mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu za wananchi wetu hasa katika
maeneo yenye migodi mikubwa ya dhahabu kama vile Nyamongo, Arusha na
kwingineko katika nchi yetu. Vile vile, tulihoji sababu za Serikali
kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria na za kiutendaji watuhumiwa wa
makosa haya makubwa.
Mheshimiwa Spika,
Wakati
anatoa hoja yake ya kuahirisha Mkutano wa Bunge la Bajeti la mwaka
jana, Waziri Mkuu aliahidi kwamba Serikali ingefanya uchunguzi wa
matukio yote ya mauaji kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (The
Inquests Act), Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania. Kwa maneno yake
mwenyewe, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema: “vifo ... ambavyo vimetokea
katika mazingira ya kutatanisha chini ya mikono ya Vyombo vya Dola, ni
lazima vichunguzwe.” Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, hadi wakati
tunaandika maoni haya, hakuna Mahakama ya Korona hata moja ambayo
imeitishwa kwa lengo la kuchunguza vifo vilivyotokana na matumizi ya
nguvu ya vyombo vya dola. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama kauli ya
Waziri Mkuu ilitolewa kwa lengo la kuwahadaa Watanzania. Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itamke ni lini Serikali
itaunda Mahakama za Korona ili kuchunguza matukio yote ya mauaji ya
wananchi katika maeneo yote tuliyoyataja mwaka jana.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
sababu ya Serikali kutotimiza ahadi yake ya kuchunguza matukio ya
mauaji kwa mujibu wa Sheria tajwa, vitendo vya mauaji na ukiukwaji wa
haki za binadamu vimeendelea kutokea katika nchi yetu. Kwa mfano, katika
taarifa yake ya Haki za Binadamu kwa Mwaka 2011, Kituo cha Sheria na
Haki za Binadamu (LHRC) kinaripoti kwamba “mwenendo wa matukio ya
ukatili wa polisi na mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria na vyombo
vya dola umeendelea kuongezeka katika nchi yetu. Kati ya Januari na
Desemba 2011 tayari watu 25 wamekwisharipotiwa kuuawa wakiwa mikononi
mwa polisi na maafisa wengine wa usalama, wakati ambapo watu wengine 50
walijeruhiwa.” Taarifa hii inaungwa mkono na taarifa ya Hali ya Haki za
Binadamu kuhusu Tanzania iliyotolewa mwaka huu na Wizara ya Mambo ya Nje
ya Marekani (State Department) inayoonyesha kuwa bado yapo mauaji
yanayotokea mikononi mwa vyombo vya dola ikiwemo jeshi la polisi,
utesaji na wananchi wanaotuhumiwa kujikuta wakipata vipigo kinyume na
mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.
MAUAJI YENYE SURA YA KISIASA
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na Serikali kutochukua hatua kukabiliana na matukio ya mauaji
yanayohusishwa na vyombo vya dola, sasa limezuka wimbi la mauaji na
matukio ya majaribio ya mauji yenye sura ya kisiasa katika maeneo
mbalimbali nchini. Matukio hayo ni pamoja na mauji ya kada wa CHADEMA
Mbwana Masudi yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika
Jimbo la Igunga, na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Usa River,
Marehemu Msafiri Mbwambo, mara baada ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika
Jimbo la Arumeru Mashariki.
Aidha,
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na majaribio ya mauaji ambapo wabunge wa
CHADEMA Mheshimiwa Highness Kiwia wa Jimbo la Ilemela na Mheshimiwa
Salvatory Machemli wa Jimbo la Ukerewe, walioshambuliwa kwa mapanga
mbele ya maafisa polisi na watu wanaosadikiwa kutumwa na makada wa CCM
mkoani Mwanza. Vile vile, Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa
Iringa Mjini (CHADEMA) alivamiwa na wafuasi wa CCM wanaodaiwa kutumwa na
Iddi Chonanga, Diwani wa Kata ya Nduli (CCM) katika Halmashauri ya
Manispaa ya Iringa.
Mheshimiwa Spika,
Matukio
ya mauaji au majaribio ya mauaji yenye sura ya kisiasa yamewahusu pia
watu ambao sio wanachama au viongozi wa vyama vya siasa lakini
wanaonekana kupinga matakwa ya watawala. Haya yamemkuta Mwenyekiti wa
Jumuia ya Madaktari Dr. Steven Ulimboka ambaye alitekwa nyara na kuteswa
kwa kikatili na watu ambao taarifa za vyombo vya habari zimewataja kuwa
maafisa wa vyombo vya dola. Kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iamuru
kukamatwa kwa watuhumiwa wote ambao wametajwa kuhusika na utekaji nyara
na jaribio la kumuua Dr. Ulimboka ili kufuta dhana kwamba vyombo vya
dola viko juu ya sheria na vinaweza kuua au kutesa wananchi bila mkono
mrefu wa sheria kuwaangukia.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe
14 Julai 2012, mtu anayesemekana kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa
CCM katika Kata Ndago, Jimbo la Iramba Magharibi, Yohana Mpinga, ambaye
pia ni mtoto wa Mwenyekiti wa CHADEMA katika Kata ya Urughu alifariki
dunia kufuatia vurugu zilizotokea baada ya kumalizika kwa mkutano wa
hadhara uliohutubiwa na viongozi wa CHADEMA katika Kata ya Ndago. Kwa
vile, tayari baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali ndani ya Bunge
hili tukufu wanaelekea kuwa wameshapitisha hukumu kwamba CHADEMA
inahusika na kifo cha Marehemu Yohana Mpinga, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ina haya ya kueleza kuhusiana na tukio hili.
Kwanza,
mkutano wa hadhara wa CHADEMA ulihudhuriwa pia na maafisa polisi
waliokuwepo wakati wote wa mkutano huo. Pili, licha ya kuwepo kwa
maafisa polisi hao, kundi la wahuni wanaodaiwa kukodiwa na makada wa CCM
wa Jimbo la Iramba Magharibi walivuruga mkutano huo kwa kupiga mawe
watu waliohudhuria mara mbili lakini mara zote polisi waliokuwepo
hawakuchukua hatua zozote dhidi ya kundi hilo la wahuni. Aidha, mara ya
wahuni hao kuvuruga mkutano mara ya pili, viongozi wa CHADEMA walitoa
taarifa rasmi katika Kituo cha Polisi cha Ndago na kufunguliwa jalada
namba NDG/RB/190/2012.
Tatu,
mara baada ya kutoa taarifa hiyo kwa polisi, mkutano wa hadhara
uliendelea bila fujo yoyote hadi ulipomalizika na msafara wa viongozi wa
CHADEMA kuondoka eneo la Ndago na kuelekea Kinampanda ambako kulikuwa
na mkutano mwingine wa hadhara. Wakati huo, kundi la askari polisi wa
Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kutoka Kiomboi walishafika katika eneo la
mkutano na kukuta mkutano umemalizika. Nne, kwa vile mkutano wa hadhara
wa CHADEMA ulimalizika kwa amani mbali na matukio ya kihuni
yaliyoripotiwa kwa Jeshi la Polisi, na kwa vile kulikuwa na kikosi cha
FFU na askari polisi wengine katika eneo la mkutano baada ya msafara wa
CHADEMA kuondoka, ni wazi kwamba watu wanaotakiwa kutoa maelezo ya jinsi
Marehemu Yohana Mpinga alivyofikwa na mauti ni Jeshi la Polisi lenyewe.
Aidha,
Mheshimiwa Spika, ni Jeshi la Polisi pekee linaloweza kuwaeleza
Watanzania kwa nini kikundi cha wahuni waliowarushia mawe viongozi wa
CHADEMA na wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara hawakuchukuliwa
hatua zozote na polisi waliokuwepo kwa muda wote wa mkutano huo au
askari wa FFU waliofika baada ya msafara wa CHADEMA kuondoka. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa sana na mauaji ya kijana huyo na
inatuma salamu za pole na rambi rambi kwa familia, ndugu na jamaa wa
marehemu. Hata hivyo, Kambi yetu inasikitishwa na kushangazwa sana na
ushabiki wa kisiasa ambao umejitokeza humu Bungeni na kauli za kutoa
hukumu ambazo zimetolewa na baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali
bila hata kusubiri uchunguzi kamili juu ya jambo hili.
MASLAHI YA POLISI NA MAGEREZA
Mheshimiwa Spika,
Katika
maoni yake ya mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia
utamaduni wa Serikali kupuuza maslahi ya askari polisi na wale wa Jeshi
la Magereza. Utamaduni huu ni wa muda mrefu sana. Kwa mfano, katika
hotuba ya bajeti ya Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha
2006/2007, aliyekuwa Waziri wakati huo alikiri kwamba “... kutokana na
kipato kidogo cha askari polisi, inawawia vigumu kukopa katika mabenki
nchini kutokana na riba kuwa kubwa na kukosa dhamana za uhakika. Hivyo,
askari polisi hawana mahali popote wanapoweza kupata fedha za
kujiendeleza kiuchumi. Aidha, mishahara na posho wanayolipwa askari bado
haikidhi hali halisi ya mahitaji yao na familia zao.”
Mheshimiwa Spika,
Toka
wakati huo hadi sasa, maslahi ya askari polisi yamekuwa mabaya zaidi
kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumuko wa bei hasa za
vyakula kupanda wakati ambapo mishahara yao haijaongezeka sambamba na
ongezeko la gharama halisi za maisha. Aidha, katika hali inayoonyesha
kutokujali kabisa maslahi na hali za maisha za askari wetu, Serikali
imeshindwa kutekeleza ahadi yake iliyotolewa tarehe 17 Novemba, 2011 na
aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya ndani Mheshimiwa Khamis Sued
Kagasheki, aliyeliambia Bunge hili tukufu kwamba “... posho ya askari
imepandishwa na ... kwamba (inatakiwa) itoke kwenye shilingi laki moja
mpaka shilingi laki moja na hamsini.... Ni jambo ambalo tunalo na
tumelifanyia kazi na tuna uhakika kwamba, litaweza kutimia….”
Mheshimiwa Spika,
Ni
ukweli usio na mjadala kwamba askari polisi na magereza bado wanapokea
posho ya kujikimu ya shilingi laki moja badala ya shilingi laki moja na
elfu hamsini iliyoahidiwa na Serikali mbele ya Bunge hili tukufu. Aidha,
katika mazingira ya kushangaza kabisa, mara baada ya Serikali kutoa
ahadi Bungeni juu ya posho hiyo, uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi
ulituma maelekezo kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa kufanya uchunguzi ili
kubaini askari wote waliokuwa wanadai walipwe posho ya shilingi laki
moja na nusu kama ilivyoahidiwa ili askari hao wafukuzwe kazi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ilieleze Bunge lako tukufu
ni lini italipa malimbikizo ya baki ya shilingi elfu hamsini kwa mwezi
kwa kila askari polisi na magereza ambayo haijawalipa askari hao hadi
hivi sasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
ianze kuwalipa askari polisi na magereza posho ya kujikimu ya shilingi
laki moja na nusu kwa mwezi kuanzia mwaka huu wa fedha, kwa vile ahadi
ya Serikali iliyotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani
haijawahi kukanushwa, kubatilishwa au kubadilishwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika,
Sio
tu kwamba Serikali haitekelezi ahadi inazotoa Bungeni juu ya malipo ya
askari polisi na magereza. Serikali pia imekuwa inawakopa watumishi hao
bila ridhaa yao. Kwa mfano, randama ya fungu la 29 inaonyesha kuwa Jeshi
la magereza linadaiwa jumla ya shilingi bilioni 23.65. Kati ya fedha
hizo, watumishi wa Jeshi la Magereza wanaidai Serikali jumla ya shilingi
bilioni10.34 ambazo ni malipo ya stahili zao mbali mbali kama vile
fedha za likizo, uhamisho, mafunzo, n.k. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili kama, na lini, italipa
madeni haya ya askari magereza wetu wanaokesha magerezani usiku na
kushinda juani mchana wakiwalinda wafungwa na mahabusu waliojaa katika
magereza ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Kuna
hatari kwa askari wa Jeshi la Magereza kufanya kazi katika mazingira
magumu ambayo tumeyaeleza katika maoni haya. Mfano ni katika Jimbo langu
la Musoma Mjini. Mbali na makazi duni ya askari magereza, vile vile
kuna umbali mrefu kati ya kambi ya askari magereza ya Nyasho na Gereza
la Mkoa lililopo Kata ya Mkendo na askari magereza wamekuwa wakitembea
kwa miguu usiku wanapokuwa zamu gerezani. Hii inahatarisha usalama wao
kwani wanaweza kuvamiwa na kudhuriwa na wafungwa au mahabusu waliokwisha
kumaliza adhabu zao lakini wakawa na visasi na askari hao. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwapatie gari askari wa kambi ya
Nyasho na makazi mengine ya askari magereza yaliyoko mbali na magereza
wanakofanyia kazi ili kunusuru maisha ya askari magereza wetu.
Mheshimiwa Spika,
Katika
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya mwaka jana, tulipendekeza
kwamba “... utaratibu wa sasa wa polisi wa ngazi za chini kukatwa
shilingi 5,000 kila mwezi kwenye mishahara yao, kwa ajili kugharamia
mazishi yao na wategemezi wao, ufutwe mara moja, kwani unawanyonya kwa
sababu vipato vyao ni vidogo. Badala yake ... serikali ibebe jukumu
hilo.” Hata hivyo, hadi tunaandika maoni haya, Serikali imeendelea
kupuuza mapendekezo haya kwa kisingizio kwamba ‘mfuko wa kufa na
kuzikana’ ni wa hiari ilhali askari polisi wanaendelea kukatwa mishahara
yao kwa lazima. Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inatamka kwamba kukata mshahara wa mfanyakazi bila ridhaa yake wakati
hadaiwi chochote na mwajiri wake ni kinyume cha sheria husika za nchi
yetu na kitendo cha jeshi la Polisi kuendelea kukata mishahara ya askari
polisi kwa ajili ya ‘mfuko wa kufa na kuzikana’ bila ridhaa ya askari
polisi wenyewe kikome mara moja.
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba askari polisi wanaofanya
kazi za lindo katika mabenki yote ya biashara hapa nchini hulipwa posho
ya shilingi elfu kumi kwa siku. Hata hivyo, Serikali haijawahi kutamka
hadharani kiasi ambacho mabenki hayo hulipa serikalini kwa ajili ya kazi
hiyo ya kulinda mabenki binafsi. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikli kulieleza Bunge lako tukufu kiasi
ambacho mabenki ya biashara hulipa serikalini kwa ajili ya huduma ya
ulinzi inayotolewa na askari polisi ili Bunge lako lifahamu kama askari
polisi wanaofanya kazi hiyo wanalipwa inavyostahili.
VITENDEA KAZI VYA POLISI
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa, makosa ya jinai
yaliyoripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi hapa nchini yalikuwa
62,133. Ripoti inasema kwamba kwa mwaka 2011 makosa 63,703 ya jinai
yaliripotiwa katika vituo vya polisi nchini. Kwa kiasi kikubwa, ongezeko
hili la uhalifu linasababishwa na askari wa doria kushindwa kufika
kwenye maeneo ya matukio ya uhalifu kwa haraka pindi wapatapo taarifa
kwa kisingizio cha kukosa mafuta kwa ajili ya magari ya doria.
Hata
hivyo, Mheshimiwa Spika, nyaraka za Serikali zinaonyesha kwamba Bunge
lako tukufu limekuwa likiidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya mafuta ya
magari ya Jeshi la Polisi. Kwa mfano, kwa mujibu wa randama ya Fungu la
28 kwa mwaka huu wa fedha, matumizi halisi ya mafuta kwa ajili ya Jeshi
la Polisi kwa mwaka wa fedha 2010/2011 yalikuwa shilingi bilioni 2.81.
Aidha, katika mwaka wa fedha uliopita Bunge lako tukufu liliidhinisha
shilingi bilioni 2.61 kwa ajili ya mafuta, wakati ambapo kwa mwaka huu
wa fedha Serikali inaomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 2.56 kwa
ajili ya mafuta ya magari ya Jeshi la Polisi.
Wakati
Bunge limekuwa lkiidhinisha mafungu haya makubwa ya fedha kwa ajili ya
mafuta, askari polisi wamekuwa wakilalamika kwamba hawapewi fedha za
mafuta kwa ajili ya magari ya doria hivyo kusababisha askari polisi
kushindwa kufanya kazi zao hizo ipasavyo. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali ieleze zinakopelekwa fedha za mafuta kwa ajili
ya Jeshi la Polisi kama gari moja la doria linapatiwa lita 5 za mafuta
kwa kutwa na/au usiku.
IDARA YA UHAMIAJI NA PAKACHA LA MIPAKA
Mheshimiwa Spika,
Mipaka
yetu na nchi jirani zinazotuzunguka imekuwa pakacha linalovuja. Ndio
maana katika hotuba yetu ya mwaka jana tuliliambia Bunge lako tukufu
kwamba “... kumekuwa na ongezeko la wageni wengi kutoka nchi za nje ...
kiasi cha kujiuliza kama nchi hii ina utaratibu wowote wa kuratibu na
kudhibiti uingiaji wa wageni hapa nchini.” Tulionyesha jinsi ambavyo
kumekuwa na ongezeko la wageni haramu kutoka nchi za Somalia, Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Pakistan,
Nigeria, China, India na Bangladesh “ambao wanaishi Tanzania kwa mfumo
usio rasmi, bila ya kuwa na hati zinazowaruhusu kufanya hivyo.”
Tulitahadharisha kwamba “utaratibu wa kuachia kila mgeni kuingia
Tanzania na kuishi atakavyo bila ya vyombo husika kujua kuwepo kwake ni
hatari kiusalama, hasa katika zama hizi za kusambaa kwa ... ugaidi na
uharamia wa kimataifa katika masuala ya fedha, biashara za binadamu ...”
n.k.
Mheshimiwa Spika,
Maneno
na tahadhari zetu ziliangukia kwenye masikio ya Serikali kiziwi. Na
sasa yale tuliyoyasema yameanza kutimia kwani ni mwezi mmoja tu umepita
tangu wahamiaji haramu zaidi ya arobaini kutoka Ethiopia kukutwa
wamekufa ndani ya lori la mizigo ambalo kwa vyovyote vile lilitokea nchi
jirani. Watu hawa waliingiaje nchini na kusafiri hadi katikati ya nchi
yetu bila kujulikana na maafisa wa Uhamiaji, polisi wa usalama
barabarani na usalama wa taifa kama kweli nchi yetu iko salama? Ni afisa
gani wa Idara ya Uhamiaji aliyewapitisha katika mpaka wetu wa Namanga
au Horohoro au Sirari au Kogaja au Borogonja? Na ni askari polisi gani
aliyewasindikiza hadi Kongwa? Aidha, ni afisa mizani gani wa TanRoads
aliyepitisha lori walimokuwa watu hao bila kulikagua na kujua
kilichokuwamo?
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitegemea – kwa kuzingatia ukubwa na uzito
wa kashfa hii – viongozi waadilifu katika Wizara, Idara ya Uhamiaji na
Jeshi la Polisi wangewajibika kutokana na uchafu huu. Hata hivyo, hakuna
hata mmoja ambaye amefanya hivyo. Kwa vile uwajibikaji wa hiari
unaelekea kushindikana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Rais
Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuwawajibisha wale wote
waliohusika kuanzia viongozi wa Wizara walioko humu Bungeni na uongozi
wa juu wa Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi ili kuondokana na aibu
hii ya nchi yetu kuwa transit route ya biashara ya kusafirisha binadamu
katika sehemu hii ya Bara la Afrika.
Mheshimiwa Spika,
Matatizo
ya ongezeko la wahamiaji haramu katika nchi yetu linatokana na Idara ya
Uhamiaji kuendekeza vitendo vya kifisadi katika kuajiri, kupandisha
madaraja au vyeo wa maafisa wa Idara hiyo. Kwa mujibu wa taarifa tulizo
nazo, ajira katika Idara ya Uhamiaji haizingatii tena elimu, uwezo na
weledi wa maafisa husika. Bali, kwa mujibu Taarifa ya Utafiti wa Mpango
Mkakati wa Mageuzi Katika Utumishi wa Uhamiaji (Immigration Service
Reform Programme Strategic Plan Research Report) iliyochapishwa na
Wizara ya Mambo ya Ndani tarehe 27 Novemba, 2011, “mara nyingi mgawanyo
ya kazi (katika Idara) hautegemei sifa bali unategemea upendeleo,
rushwa, kujuana na urafiki vitu ambavyo viko kinyume na maana halisi ya
mgawanyo wa kazi.” (“Most of the time placement is not based on merits
but depends on nepotism, bribery and technical know-who, friendship and
favouritism that have been contrary to the whole meaning of placement.”)
Mheshimiwa Spika,
Ushahidi
wa kauli hii unapatikana katika Taarifa hiyo ya Utafiti inayoonyesha
kwamba maafisa wengi wa ngazi za juu katika Idara ya Uhamiaji ni watu
wenye uwezo mdogo kielimu kulinganisha na maafisa wa ngazi za chini wa
Idara hiyo. Kwa mfano, katika ngazi ya Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji
kwenda juu hadi kwa Kamishna Mkuu, kuna maafisa kumi wenye shahada ya
uzamili (masters degree), wawili wenye post-graduate diploma (PGD),
ishirini na nne wenye shahada ya kwanza, tisa wenye stashahada, saba
wenye diploma, kumi na moja wenye kidato cha sita na 248 wenye elimu ya
kidato cha nne. Katika maafisa hawa wa ngazi za juu, kuna Kamishna mmoja
mwenye elimu ya kidato cha nne wakati kuna Makaimu Kamishna 216 wenye
elimu hiyo ya kidato cha nne na Kamishna Wasaidizi Wakuu 31.
Kwa
upande mwingine, Mheshimiwa Spika, kuanzia ngazi ya Mrakibu Mwandamizi
(Senior Superintendent) kwenda chini mpaka koplo kuna maafisa wenye
shahada ya uzamili 36, wenye post-graduate diploma wako saba, wenye
shahada ya kwanza wako 340, wenye stashahada wako 78, diploma wako kumi
wenye cheti (certificate) wako 52, waliomaliza kidato cha sita wako 585
wakati waliohitimu kidato cha nne wako 337. Katika mazingira ambayo
maafisa wenye uwezo mkubwa wa elimu hawapewi nafasi za juu katika Idara
badala yake uongozi wa juu umejazwa na wenye elimu za mashaka kama
inavyoonyeshwa katika Taarifa ya Utafiti ya Wizara, ni wazi kwamba
matukio kama ya maafa ya wahamiaji waliokutwa wamekufa Jimboni kwa Naibu
Spika wa Bunge hili tukufu hayawezi kuepukika!
Aidha,
Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya upendeleo na rushwa katika ajira
ya Idara ya Uhamiaji ya aina hii, maafisa uhamiaji hawawezi kuacha
kutumiwa na wanasiasa wa chama tawala kuwatuhumu washindani wao kisiasa
kuwa sio raia wa Tanzania ili kuwaondoa katika kinyang’anyiro cha
chaguzi zetu. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Mheshimiwa Ali Mohamed Keissy
alipotaka kugombea Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA na kuzushiwa tuhuma kuwa
siyo raia. Hata hivyo, alipojiunga na CCM bila ridhaa yake tuhuma za
kutokuwa raia ziliyeyuka na sasa ni Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi
Kaskazini katika Mkoa anakotokea Waziri Mkuu!
Mheshimiwa Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya
Bunge hili tukufu juu ya mambo haya ambayo yamethibitishwa na Ripoti ya
Utafiti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Aidha, Kambi inaitaka Serikali itoe
kauli kama kuna haja yoyote ya kutumia mamilioni ya fedha za wananchi
kusomesha maafisa wa Idara ya Uhamiaji ambao baada ya kufuzu hawapatiwi
vyeo na majukumu yanayolingana na uwezo wao wa kielimu.
JESHI LA ZIMA MOTO NA UOKOAJI
Mheshimiwa Spika,
Ni
dhahiri kuwa umuhimu wa Jeshi hili unaonekana pale yanapotokea majanga
ya moto, mafuriko au maafa mengine kama vile tetemeko la ardhi ambapo
athari za matukio haya ni makubwa sana na mara nyingi hupelekea wananchi
kupoteza maisha. Malalamiko ya wananchi katika maeneo mbalimbali juu ya
Jeshi la Zimamoto kuchelewa kufika katika maeneo ya tukio yamekuwepo
kwa miaka mingi na yamepigiwa kelele sana hapa Bungeni. Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inarudia ushauri wake kuwa Serikali iboreshe mfumo
mzima wa zimamoto katika nchi yetu ili kukabiliana na majanga ya moto
yanayoongezeka kutokana na kupanuka na kukua kwa miji yetu.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya maelezo na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ninaomba kuwasilisha.
.....................……………………………………..
VINCENT JOSEPHAT NYERERE
MSEMAJI MKUU WA
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
17/07/2012
No comments:
Post a Comment