Friday, July 6, 2012

Afya ya Ulimboka ni ya utata mtupu

  Yaelezwa anapumulia mashine
  Hofu yatanda kwa wazazi wake
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania , Dk. Stephen Ulimboka

Hali ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania , Dk. Stephen Ulimboka, aliyelazwa nchini Afrika Kusini bado ni ya utata hasa kutokana na kuwepo kwa taarifa zinazokinzana kwamba hali yake siyo nzuri huku familia yake ikikataa kueleza chochote kuhusu suala hilo.

Wakati Katibu wa Jumuiya hiyo, Dk. Edwin Chitage, akieleza juzi kuwa Dk. Ulimboka anaendelea vizuri, vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii vimesema kuwa hali yake ni mbaya na kwamba amelazwa kwenye chumba cha wagojwa wenye uangalizi maalum (ICU).

Kutokana na taarifa hizo kutofautiana, NIPASHE ilikwenda nyumba kwa wazazi wa Dk.Ulimboka eneo la Ubungo Kibangu kwa ajili ya kupata taarifa za hali yake.

Hata hivyo, mama mzazi wa Dk. Ulimboka pamoja na kuonana na gazeti hili alipoulizwa kuhusu hali ya mwanaye aliyepelekwa Afrika Kusini kwa matibabu hakutaka kusema lolote na alionekana mwenye majonzi makubwa.

Mama huyo ambaye alikataa hata kutaja jina lake, alikuwa na hali ya hofu hasa pale alipofika mtu yeyote ambaye familia haimfahamu.

“Kwa kweli kwa sasa hivi naomba wanangu mniache, nina wageni ambao wamekuja hapa kwangu nina mazungumzo nao,”alisema mama huyo na kuingia ndani.

Kulikuwa na idadi kubwa ya watu nyumbani kwa wazazi wa Dk. Ulimboka hali inyoonyesha kuwa walikuwa wametoka mbali kwenda kuwajulia hali.

Majirani wa familia ya Dk.Ulimboka waliozungumza na NIPASHE walisema tangu tukio hilo lilipotokea, familia hiyo imekuwa ikiishi katika hali ya hofu hasa kutokana na kitendo cha kinyama alichofanyiwa mtoto wao na watu wasiojulikana ambao hadi sasa hawajajulikana.

Tangu Dk. Ulimboka apelekwe Afrika Kusini, wakazi wa  jiji la Dar es Salaam na mikoani wamekuwa wakipiga simu katika vyombo vya habari wakitaka kujua hali yake inaendeleaje.

Hata hivyo, Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), jana asubuhi liliripoti katika kipindi cha amka na BBC kuwa Dk. Ulimboka yuko ICU na kwamba amewekewa mashine za kumsaidia kupumua.

Kufuatia taarifa hizo, NIPASHE ilimtafuta Katibu wa Chama cha Madaktari Nchini (MAT), Dk. Rodrick Kabangila ambaye alieleza kuwa hajapata taarifa zozote juu ya hali ya Dk Ulimboka kwa siku ya jana ila hadi juzi usiku alikuwa anaendelea vizuri.

Wakati baadhi ya wananchi wakiwa na hisia kwamba huenda vyombo vya dola vilihusika katika tukio la kumteka na kumpiga Dk. Ulimboka, makundi mbalimbali ya kijamii, vikiwamo vyama vya upinzani vimesema sifa ya taifa ipo shakani kufuatia kitendo hicho.

Jana Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni, alisema kuwa sifa ya taifa katika jamii ya kimataifa inachafuka kutokana na vitendo vya kuteshwa kwa raia na kuuawa ovyo, huku Jeshi la Polisi likihusishwa na tuhuma hizo.

Mbowe alisema ni kweli kwamba hisia za vyombo vya dola kuhusika katika mateso na mauaji ya raia, limeendelea kuwepo.

Alisema sifa ya taifa sasa hivi iko shakani katika ngazi ya kimataifa, kutokana na tukio la mateso yenye lengo la kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka.

Alitoa mfano pia wa tukio la kushambulia wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), la kupigwa na kuumizwa kule Mwanza kuwa ni miongoni mwa mfululizo wa matukio hayo.

Alihoji kama Serikali iko tayari kuunda tume huru ya uchunguzi kuchunguza suala hilo badala ya kuachia jeshi la polisi ambalo ni sehemu ya tatizo.

Akijibu swali kuhusu kuchafuka kwa sifa ya Tanzania, Pinda, alisema hakubaliani na maneno hayo kwamba sifa ya taifa imechafuka sana na kuhoji kwamba inachafuka sana kwa lipi.

Alisema kwa kusema sifa ya taifa imechafuka lazima kuwepo kwa ushahidi wa kutosha kuhusiana na jambo hilo.

Alisema mfano wa Dk. Ulimboka siyo mzuri na kutaka sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata, kutumika ili kuondokana na hisia hizo.

Pinda aliendelea na msimamo kwamba haingii akilini mwake kwamba serikali inahusika je na kadhia ya kutekwa na kuumizwa kwa Dk. Ulimboka kwa kuwa alikuwa kwenye mazungumzo na hata wakati mkasa huo unatokea kulikuwa na amri ya mahakama ambayo ilikuwa inaisaidia serikali.

Kimsingi Pinda alikataa pendekezo la kuundwa kwa tume huru ya Bunge kuchunguza suala la Dk. Ulimboka na mauaji mengine yanaotiliwa shaka kuwa yanahusisha vyombo vya dola.

Katika swali la msingi, Mbowe alisema kumekuwepo na mauaji mengi nchini na baadhi ya vifo hivyo vimekuwa vya utata mwingi huku baadhi vikihusisha vyombo vya dola likiwemo jeshi la polisi.

Alisema kuwa Pinda, katika bajeti ya mwaka jana alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na kuahidi sheria ya uchunguzi wa vifo vyenye utata itafanyiwa kazi na serikali na kwamba vitakuwa vinafanyiwa uchunguzi.

Alihoji ni kwanini ahadi yake hiyo muhimu kwa taifa haijatekelezwa na kwamba  kutofanya hivyo haoni kama anakuza hisia kuwa viongozi wa serikali wanahusika kuagiza mauji hayo.

Akijibu swali hilo, Pinda alikiri kwamba mwaka jana alitoa kauli hiyo ili sheria uchunguzi wa vifo vyenye utata izingatiwe kikamilifu.

Mkanganyiko wa hali ya Dk. Ulimboka umezidi kushika kasi hasa kutokana na kutolewa kwa habari zinazochanganya kutoka vyanzo mbalimbali, juzi  Dk. Chitage,alipoulizwa na NIPASHE hali yake inaendeleaje na amelazwa  hospitali gani alisema anaendelea vizuri, lakini alikataa kutaja hospitali hiyo.

“Ndugu mwandishi nadhani unafahamu tukio zima lililompata Dk. Ulimboka, hivyo kutaja hospitali anayotibiwa kwa sasa ni sawa na kumtangazia kifo,” alisema Chitage.

Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 25 mwaka huu na watu wasiojulikana waliokuwa na silaha za moto ambao walimjeruhi vibaya ikiwemo kumng’oa meno na kucha.

Kufuatia tukio hilo madaktari wenzake walichangishana fedha na Jumamosi ya wiki iliyopita waliamua kumpeleka Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.


CHANZO: NIPASHE

No comments: