Na Florence Majani, Dodoma
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, imetenga zaidi ya nusu ya bajeti yake kwa mwaka wa fedha,
2012/2013 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mji mpya
wa Kigamboni, Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam.Fedha zilizotengwa kwa
ajili ya kuendeleza mji huo ni Sh60 bilioni ambazo ni sawa na asilimia
59 ya makadirio ya matumizi ya wizara hiyo, ambayo ni Sh101.731 bilioni.
Hata
hivyo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna
Tibaijuka alisema Bungeni jana kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya
ujenzi huo ni sawa na asilimia 10 tu ya mahitaji ya kiasi cha Sh605.
“Kwa
hiyo tutatumia mbinu za kisasa kutafuta pesa nyingine Sh605 bilioni nje
ya Bajeti kutekeleza mradi huu bila kuchelewa zaidi. Mradi huu
unahitaji kiasi hicho cha fedha kwa miaka mitatu ya kwanza,” alisema
Profesa Tibaijuka alipokuwa akiwasilisha makadirio ya matumizi ya wizara
yake jana na kuongeza:
“Nitasimamia mradi huu kwa kasi, ari na
nguvu mpya. Ingawa pia sitakuwa nimetenda haki iwapo sitawashukuru
wananchi wa Kigamboni kwa uvumilivu na ushirikiano wanaotuonyesha.”
Katika
Bajeti ya wizara hiyo ya Sh101.7 bilioni, matumizi ya kawaida ni Sh30.7
bilioni na Sh71 bilioni ni za maendeleo. Katika fedha hizo za
maendeleo, Sh61 bilioni ni fedha za ndani na Sh10 bilioni ni fedha za
nje.
Kuhusu wananchi wanaoishi katika eneo hilo, Profesa
Tibaijuka alisema hakuna mkazi yeyote wa Kigamboni atakayehamishwa kwani
idadi ya wananchi waliopo ni ndogo ikilinganishwa na idadi ya makazi
mapya yanayotakiwa kujengwa katika eneo hilo.
Alisema ni ushauri wake
kwamba wakazi wote wa Kigamboni wachague kubaki katika mji huo kwani
wawekezaji wa ndani na nje watapewa maeneo kwa ajili ya kujenga makazi
ambayo yatatumika kuwahamishia wananchi watakaoamua kubaki.
“Tunashauri
wote wabaki kwa kuwa sasa hivi kuna wananchi takribani 82,000 wakati
tunajenga mji mpya wenye uwezo wa wakazi 400,000. Hakuna sababu ya
wananchi kuhama eneo hili ila makazi yao yatapangwa upya na kuboreshwa,”
alisema.
Gharama za mradi
Profesa Tibaijuka alisema ujenzi
wa Mji wa Kigamboni utafanywa kwa awamu tatu, ambazo zitatekelezwa kati
ya mwaka huu na 2032 na gharama zinazotarajiwa kutumika hadi
utakapokamilika ni Sh11.6 trilioni.
Alisema awamu ya kwanza
itakuwa kati ya mwaka 2012 na 2022, awamu ya pili kati ya 2022 na 2027
na awamu ya tatu ni kati ya 2027 na 2032.
Profesa Tibaijuka alisema
miongoni mwa kazi zitakazofanywa katika mwaka huu wa fedha ni kuundwa
kwa wakala mpya wa kusimamia mradi huo anayejulikana kama Kigamboni
Development Agency (KDA).
Kazi nyingine ni kuidhinisha mpango na
kuanza utekelezaji, kufanya uthamini wa mali zilizomo katika maeneo ya
miundombinu, huduma za maji na eneo mbadala na kulipa fidia kwa mali
zilizomo katika maeneo yaliyofanyiwa uthamini.
Kuhusu fidia, Waziri
Tibaijuka alisema wananchi ambao hawajakiuka maagizo ya mradi kwa
kufanya maendelezo haramu, wasiwe na wasiwasi kuhusu fidia kwa sababu
mradi utazingatia haki na ni endelevu... “Fidia itatolewa kwa mujibu wa
sheria kwa tathmini ya kiujumla ambayo itakokotolewa kutokana na viwango
vya soko na kuhusishwa ili iwe sahihi.”
Alisema atafanya ziara
ya mafunzo kwa wawakilishi kutoka Kigamboni kutembelea mji mpya ili
uwepo uelewa wa pamoja juu ya jinsi mji huo utakavyokuwa.
Hazina ya Ardhi
Katika
hatua nyingine, Profesa Tibaijuka alisema wizara yake inakamilisha
uanzishaji wa Hazina ya Ardhi pamoja na Mfuko wa Fidia ya Ardhi.
Alisema
vyombo hivyo vitasimamia utoaji wa ardhi kwa wawekezaji wa ndani na nje
kwa misingi ya kuingia ubia wa kumiliki pamoja hisa zitakazotolewa kwa
uwiano kati ya wananchi na wawekezaji husika.
Kuhusu kuweka na
kutunza alama za mipaka ya Tanzania na nchi jirani, Profesa Tibaijuka
alisema majadiliano ya kupima maeneo hayo yalishakamilika.
Alisema
majadiliano yalishafanyika baina ya Tanzania na nchi za Comoro na
Msumbiji na mkataba wa kwanza kati ya Tanzania, Msumbiji na Comoro
kwenye alama za utatu baharini inayotenganisha nchi hizo ulikamilika na
kutiwa saini Desemba 5, mwaka jana.
“Mkataba wa pili kati ya
Tanzania, Shelisheli na Comoro ulitiwa saini Februari 17, mwaka huu.
Hivyo basi, Tanzania imekamilisha upimaji wa mipaka katika Bahari ya
Hindi na itatangaza eneo lake la ukanda wa kiuchumi baharini bila
kipingamizi kwa nchi jirani,” alisema.
Alisema wizara yake
imewasilisha andiko la kudai nyongeza ya eneo ya ukanda wa kiuchumi
baharini Januari, mwaka huu na Tume ya Mipaka ya Baharini ya Umoja wa
Mataifa, inapitia andiko hilo.
Profesa Tibaijuka alisema
kupatikana kwa eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 61,000
kutaiwezesha Tanzania kuvuna rasilimali za chini ya bahari kwa manufaa
ya sasa na kwa vizazi vijavyo.
Kurasini kulipwa fidia
Kuhusu
mradi wa uendelezaji wa eneo la Kurasini ulioanza 2006 kwa ajili ya
upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Profesa Tibaijuka alisema wizara
imetenga fedha chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara kulipa fidia kwa
wananchi watakaopisha mradi huo katika eneo la Kurasini na Shimo la
Udongo.
“Wizara itaendelea na malipo hayo kwani hata mwaka jana
tulilipa kiasi cha Sh550 milioni kwa wakazi wa Mtaa wa Kurasini waliopo
jirani na Mabwawa ya Majitaka,” alisema.
Alisema wizara yake
itaendelea kutatua migogoro ya ardhi, urasimishaji wa makazi holela,
mikopo ya nyumba, ujenzi wa nyumba unaofanywa na Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC) na ujenzi wa nyumba za biashara na makazi.
No comments:
Post a Comment