MLOLONGO mrefu zaidi wa majina ya vigogo umebainika kugawiwa viwanja
katika eneo la Gezaulole, jijini Dar es Salaam, ambapo safari hii imo
familia ya Rais mstaafu wa Awamu ya Pili Ali Hassani Mwinyi.
Jana,
gazeti hili lilichapisha katika ukurasa wa mbele habari iliyoonyesha
baadhi ya majina ya vigogo waliogawiwa viwanja na kufanya wananchi wa
kawaida kulalamika.
Katika uchunguzi zaidi, imebainika kuna
orodha ndefu ya majina ya vigogo waliopewa viwanja katika mradi huo wa
Gezaulole ambayo inahusisha mawaziri, wabunge, wakuu wa taasisi za
Serikali na familia za baadhi ya watu maarufu.
Kwa upande wa
familia maarufu, imo ya mzee Mwinyi ambaye pia amegawiwa eneo, wengine
wana majina ya ukoo yanayofana na ya kwake ambao ni, Asina Mwinyi,
Maimuna Mwinyi, Salama Mwinyi na Steven Ali Mwinyi, huku kutoka katika
familia yenye jina la Kikwete yumo Ali J. Kikwete.
Viongozi
wengine maarufu waliogawiwa viwanja hivyo ni Jaji Mkuu Mohamed Chande
Othman na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Semistocles Kaijage, Waziri wa
Mambo ya Ndani, Dk Emanuel Nchimbi, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia
Kabaka, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Manejimenti ya Utumishi wa Umma),
Celina Kombani na Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam
Malima.
Kwa upande wa watendaji wa taasisi za dola, yumo Katibu
wa Bunge, Dk Thomas Kashilila, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said
Mwema, Kamishna wa Utawala na Fedha wa Jeshi la Polisi, Clodwig Mtweve,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, David Misime, Balozi wa Tanzani nchini
Afrika Kusini, Radhia Msuya, SACP Hamdan Makame, ACP John Gudaba, ACP
Saada Juma Haji na ACP Mohamed Usi.
Mlolongo huo pia unaonyesha
majina ya baadhi ya wabunge ambao ni Murtaza Mangungu wa Kilwa Kaskazini
(CCM), Mohamed Misanga, (Singida Kusini CCM), Jenister Mhagama
(Peramiho CCM), Kheri Ameir (Matemwe, CCM), Kaika Telele (Ngorongoro,
CCM), Amina Clement (Koani, CCM) na Ali Hamis Seif (Mkoani, CUF)
Pia
kuna orodha ya wabunge wa Viti Maalum CCM ambao ni Subira Mgalu,
Alshaiymaa Kweygir, Elizabeth Batenga, Josephine Genzabuke, Betty
Machangu, Lediana Mng’ong’o na Mwanakhamis Kassim Said.
Wabunge
wengine wa Viti Maalum CCM ni Mariam Mfaki, Mariam Kasembe, Agnes
Hokororo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa pamoja na Suzan
Kiwanga ambaye ni mbunge wa Viti Maalum, Chadema na Ania Said Chaurembo
ambaye ni mbunge mstaafu.
Majina mengine ambayo koo zake ni za
watu maarufu ni pamoja na Ahmed Dau, David Kandoro, Asila Ditopile,
Alice Koka, Gemini Suchak, Fidelis Owenya, Filoteus Msigwa, Evelyne
Manumba, Fatma Ismail Rage, Jamhuri Kihwelo, Issack Mwang’onda, Hijjal
Makamba, Joseph Nyambibo, Mbwana Samata, Mohamed Mzimba na Mohamed
Mtonga.
Wengine ni pamoja na Masanja Manumba, Mariam Mkama,
Mansour Al-Maamry, Onesmo Mtasiwa, Musa Chagonja, Omary Shein, Shimbo
Shimbo, Sikitu Kijazi, Solomon Kivuyo, Thomas Nyalile na Aisha Sululu
(diwani Jangwani, CCM).
Pia wamo maofisa watatu wa Bunge ambao
ni Herman Berege, Anslem Mrema na Theonest Ruhilabake pamoja na mmoja wa
maofisa waandamizi ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
Boniface Njombe.
Wananchi waja juu
Baadhi ya maofisa wa
Manispaa ya Temeke walisema fomu zilizochukuliwa ni zaidi ya 20,000 na
kwamba kila fomu ilikuwa ikiuzwa Sh30,000, hivyo kufanya fedha
zilizokusanywa kuwa zaidi ya Sh600 milioni.
Tayari mlolongo huo
wa majina ya vigogo umesababisha baadhi ya wananchi waliokuwa wakisoma
majina hayo kulalamikia mchakato wa utoaji viwanja hivyo, huku wengine
wakidai kuwa, warejeshewe fedha zao.
“Tumelipa Sh20,000 kila fomu
ya kuombea kiwanja na wananchi tuliojitokeza ni karibu 30,000, lakini
majina yanaonyesha kuwa asilimia kubwa ya waliopata ni vigogo ambao
tunaamini wana viwanja mahali pengine,” alisema mwananchi mmoja(jina
limehifadhiwa).
Mwananchi huyo alisema kuwa, hakukuwa na umuhimu
wa kutangaza zabuni hiyo kwa sababu tayari walikuwa na majina yao,
hivyo walitakiwa kuwakabidhi viwanja vyao badala ya kuwasumbua na
kuwatoza fedha.
“Hali hii inaonyesha kuwa Serikali ipo kwa ajili ya watu wachache, wenye fedha na si wananchi wa kawaida,” aliongeza.
Mwananchi mwingine (jina tunalo), alisema idadi kubwa ya watu waliokabidhiwa viwanja hivyo ni watoto wa vigogo na wabunge.
Aliongeza
kuwa hali hiyo inaonyesha wazi kuwa, hakuna kiongozi atakayewatetea
wananchi, kwa vile kila mmoja wao yupo kwa ajili ya kupigania maslahi
yake.
“Wabunge ambao tuliwategemea kutetea maslahi ya wananchi
ndio wanaoongoza kwenye orodha ya kujichukulia viwanja, hii inaonyesha
wazi kuwa hakuna kiongozi atakayeacha shughuli zake ili kutetea maslahi
ya wananchi,” alisema.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya Manispaa
hiyo vinaonyesha kuwa, halmashauri hiyo imeingiza zaidi ya Sh600
milioni kutokana na uuzaji wa viwanja hivyo.
No comments:
Post a Comment