Thursday, August 9, 2012

Wanaharakati Zimbabwe wataka kuungwa mkono

Ujumbe wa Mtandao wa Mashirika ya wanaharakati unaojulikana kama Crisis in Zimbabwe Coalition umewasili nchini kuomba ushawishi wa Tanzania katika mchakato unaoendelea nchini humo wa kabadiliko ya katiba na maandalizi ya uchaguzi wa kidemokrasia unaotarajiwa kufanyika Juni mwakani.

Zaa Twalangeti, Meneja wa Utetezi na Ushawishi wa  Muungano wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Tanzania (Tango), alisema  kuwa ujumbe huo ukiwa nchini katika ziara yake ya siku tano utakutana na mashirika yasiyo ya kiserikali, serikali, vyama vua siasa na vyama vya waandishi wa habari.

Msemaji wa Crisis in Zimbabwe Coalition, Thabani Nyomi, wakati ujumbe huo ulipokutana na watendaji wa Baraza la Habari Tanzazia (MCT) alisema kuwa ujenzi wa demokrasia nchini Zimbabwe unasuasua licha ya mwafaka uliofikiwa wa kuundwa kwa serikali ya umoja.

Alisema bado uhuru wa kujieleza unabanwa kutokana na sheria mbaya zinazovibana vyombo vya habari na kuongeza kuwa wanaamini kuwa Tanzania itasaidia kutokana na msaada wake ilioutoa kwa Zimbabwe wakati wa harakati za kudai uhuru na  ushawishi wake kama mwanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano Kusini mwa Afrika (Sadc).

Aliongeza kuwa wana matumaini kuwa Tanzania itasaidia kwa kuwa hivi karibuni itakuwa mwenyekiti wa kmati ya ulinzi na Usalama ya Sadc, ambayo pamoja na mambo mengine, jukumu lake ni kuhakikisha nchi wanachama zinafanya chaguzi za kidemokrasia.

No comments: