Na Geofrey Nyang'oro
AFYA ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk
Steven Ulimboka imeanza kuimarika ingawa bado amelazwa katika Chumba cha
Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU).
Dk Ulimboka alipelekwa
Afrika Kusini Juni 30, mwaka huu baada ya jopo la madaktari lililokuwa
likimtibu, likiongozwa na Profesa Joseph Kahamba kutoa taarifa za
kubadilika ghafla kwa afya yake na kupendekeza apelekwa nje ya nchi kwa
ajili ya vipimo na matibabu zaidi.
Jana, Katibu wa Jumuiya ya
Madaktari, Dk Edwin Chitage alisema taarifa walizokuwa nazo zinasema:
“Afya mwenyekiti wetu imeanza kuimarikia, lakini bado yupo katika chumba
cha wagonjwa mahututi kwani alikuwa naumwa sana.”
Katika hatua
nyingine, Dk Chitage alisema madaktari na wananchi wa kawaida
wanaendelea kutoa mchango wa awamu ya pili unaolenga kukusanya Dola za
Marekani 30,000 kwa ajili ya kulipia gharama za matibabu za Dk Ulimboka.
“Sijapata
kiwango sahihi kilichokusanywa hadi sasa, lakini michango inaendelea
vizuri. Madaktari na wananchi wanaendelea kukusanya na tunawashukuru,”
alisema Dk Chitage.
Madaktari na ndugu wa Dk Ulimboka kwa pamoja,
walikataa ofa iliyokuwa itolewe na Serikali ya kulipia gharama za
matibabu za mgonjwa huyo wakiishutumu kuhusika na tukio la kutekwa,
kupigwa na kutupwa katika Msitu wa Pande kwa mwenyekiti huyo wa jumuiya
ya madaktari.
Madaktari pia wamepinga tume ya polisi iliyoundwa na
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa
Polisi, Suleman Kova wakitaka kuundwa kwa tume huru kuchunguza tukio
hilo.
Hilo ni miongoni mwa madai matano ya madaktari yaliyomo katika tamko la pamoja baina yao na viongozi wa dini na wanaharakati.
Madai
mengine ni pamoja na Serikali kurejea katika meza ya majadiliano na
madaktari, kufuta kesi iliyofungua mahakamani dhidi ya madaktari hao,
kuwarejesha kazini waliofukuzwa na Rais Jakaya Kikwete kukutana na
viongozi hao kujadili chanzo cha mgogoro huo.
No comments:
Post a Comment