Baraza
la Habari la Kiislamu Tanzania (BAHAKITA) limesema linakusudia
kuwafungulia mashitaka Madaktari Mabingwa wote pamoja na Madaktari
waliokuwepo kwenye Mafunzo kwa Vitendo (Interns) ambao walishiriki
katika mgomo kwenye hospitali mbalimbali nchini na kusababisha wagonjwa
kukosa huduma za matibabu huku wengine wakipoteza maisha yao.
Hatua
hiyo imefikiwa baada ya baraza hilo kukaa na Madaktari waliokua katika
mgomo na kukubaliana kuwa waiombe radhi Serikali pamoja na wananchi
kisha warudi kazini, lakini Madaktari hao wamekiuka makubaliano hayo na
kuendelea na mgomo jambo lililoonyesha kwamba hawakuwa tayari kupata
suluhu.
Katibu
wa BAHAKITA, Said Mwaipopo amesema wameshauriana na Wanasheria wao na
kuamua kuwafungulia kesi ya mauaji Madaktari hao katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam tarehe 16 Julai 2012.
Amesema,
“kwa tukio zima jinsi lilivyokwenda, limeonyesha kwamba Madaktari
hawataki wala hawana shida tena ya kurudi kazini kwa sababu ni wazi
kwamba kuna mtu yuko nyuma yao wanaemtumikia. Sisi kama Watanzania,
sehemu ya jamii tumekaa na Wataalamu wetu wa Sheria tumekubaliana kwamba
Jumatatu tunakwenda kufungua kesi Mahakamani kwa Madaktari wote
waliogoma wakati wamesomeshwa na kodi zetu na Serikali yetu
imewasomesha, tutawafungulia kesi ya kusababisha mauaji pale Muhimbili,
kwa hiyo tunachofanya hivi sasa ni kwenda pale Muhimbili kwa mganga mkuu
kuchukua orodha ya watu waliopoteza maisha.”
“Sisi
tuliingilia kati mgomo huu kwa nia njema ya kutapata suluhu kati ya
madaktari na serikali…lakini baada ya taarifa zetu kutoka kwenye vyombo
vya habari Ikulu ilitoa tamko la kukataa kukutana na sisi... ...lakini
Ikulu walieleza vizuri kwamba hawajawahi kukataa kukutana na viongozi wa
madaktari kwa maana hiyo basi serikali imeonekana dhahiri kutaka
suluhu. Baada ya taarifa hizo sisi tuliwatafuta viongozi wa MAT ambao
tuliwaeleza kwamba kutokana na taarifa hizo wao waombe msamaha kwa
serikali na umma wa watanzania kwa kuendesha mgomo ambao umesababisha
vifo. Lakini baada ya kuwaeleza hivyo hawa viongozi wa MAT
hawakukubali…sisi kama viongozi ambao lengo letu ilikuwa kutafuta suluhu
tukaona hawa vijana (madaktari) wana nia mbaya. Lakini sisi si kujitoa
tu bali tutawafungulia mashtaka ya mauaji wote walioshiriki katika mgomo
huo. Tutafanya hivyo ili fundisho kwa wengine ambao wana nia kama za
madaktari wanaoendesha migomo.
Kwa
hiyo sisi tunaunga mkono kufikishwa mahakamani kwa Rais wao ni njia
sahihi kabisa ya kurudisha nidhamu, lakini pia tunaunga mkono matamko
yote yaliyotolewa na serikali dhidi ya madaktari,”alisema Mwaipopo.
Akijibu
hoja hizo, Katibu wa MAT, Dkt. Edwin Chitage amesema hawaogopi
kufikishwa mahakamani na kwamba wao waliwapokea viongozi hao kwa nia
njema wakiamini ni viongozi wa dini.
“Kama
wamesema watatufikishwa mahakamani wao waende halafu tutakutana
nao…sisi tuliwapokea kwa nia njema kabisa kwa sababu walituomba
wenyewe..lakini baada ya kikao cha Jumamosi siku ya Jumapili wakatupigia
simu kuomba tukutane nao,sisi tulikutana nao lakini cha kushangaza
walitueleza kwamba wamepigiwa simu na mtu wa Ikulu akiwataka kutuambia
kwamba inabidi tuandike barua ya kuomba msamaha halafu tuwape wao ili
waipeleke…sisi tulishangaa jambo hili… sisi hatutafanyi kazi hiyo,”
alisema Dkt.Chitage.
Chanzo: http://www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment