TAARIFA ambazo zimetufikia kutoka katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili ni kwamba madaktari ambao walikuwa wakiendesha mgomo
wamerejea kazini na wagonjwa wameanza kupata huduma kama kawaida.
Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Ofisa
Uhusiano Mwandamizi wa hospitali hiyo, Aminiel Buberwa Aligaesha
inaeleza kuwa tathimini iliyofanyika kuanzia asubuhi saa mbili hadi saa
11 jioni Julai 2, inaonesha kuwa madaktari wamerejea kazini.
Akitoa ufafanuzi zaidi, Aligaesha alisema katika Idara ya Tiba,
madaktari bingwa 19 kati ya 21 wamefika kazini huku akibainisha watatu
ambao hawakufika wapo likizo.
“…Registrars wote 12 walikuja kazini. Kliniki zote za tiba
zimefanyika kama kawaida. Katika Idara ya watoto, yenye Madakatari
Bingwa 16, kati yao 14 walikuja kazini wengine wawili wako likizo na
Registrar watatu kati ya sita walikuja kazini ambapo watatu wako
likizo,” alisema katika taarifa yake ofisa huyo.
Aidha aliongeza kuwa upande wa OPD yenye Registrars saba, sita kati
yao walikuja kazini na mmoja yuko likizo. Aidha Madaktari Bingwa wote
walikuja kazini.
“Idara ya Magonjwa ya Afya ya Akili yenye Madakatri Bingwa 10, tisa
walikuja kazini na mmoja wao yuko masomoni. Upande wa Emergency
Medicine, Registrars wote 10 walikuja kazini.”
Akizungumzia kuhusu huduma za upasuaji, wagonjwa wote waliolazwa
wodini wameonwa, na baadhi ya kliniki za huduma ya upasuaji zilifanyika.
Hata hivyo, upasuaji haukufanyika kwani hakukuwa na orodha ya wagonjwa
waliopangwa kufanyiwa upasuaji.
“Kwa ujumla naweza kusema madaktari wote wamerejea kazini,” alisema Aminiel Aligaesha.
Juzi Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete akihutubia taifa alisema
Serikali hainauwezo wa kuwalipa madaktari sh. milioni 3.5 kwa daktari
anayeanza kazi kama wanavyotaka wao, hivyo kama kuna daktari ambaye
haridhiki na kiasi cha sh. 957,700 wanazolipwa sasa kwa daktari
anayeanza kazi ni vema aache kazi kiustarabu tofauti na kufanya mgomo.
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo katika hotuba yake ya mwezi Juni, huku
akisisitiza kwamba kiasi cha mshahara anaolipwa daktari anayeanza kazi
kwa sasa ni kikubwa ukilingannisha na watumishi wengine wa Serikali.
Alisema Serikali imekuwa ikipandisha maslahi ya madaktari kwa upendeleo
kulingana na umuhimu wao, kwani mwaka 2004/2005, mshahara wa kuanzia wa
daktari ulikuwa sh. 178,700, kiasi ambacho mwaka 2005/2006 kilipandishwa
na kufikia sh. 403,120.
No comments:
Post a Comment