Na Masoud Sanani, Zanzibar
BAADHI ya wakazi wa Zanzibar wametaka Katiba
Mpya iweke kipindi cha ubunge na uwakilishi kiwe miaka 10 kama ilivyo
kwa Rais ili kuimarisha demokrasia nchini.Wakitoa maoni kwenye Mkutano
wa kusaka maoni ulioandaliwa na Tume ya Katiba mjini hapa walisema
lazima wabunge wawe na miaka 10 kama ilivyo kwa Rais badala ya kutaka
wawe wabunge milele.
Abdallah Khamis Abdallah (54) na Bakar
Mwinyi Mussa (63) wa Mitakawani walitaka wabunge wa wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi wawe na muda maalumu wa uongozi wa miaka 10 kama ilivyo kwa
Urais.
Abdallah pia alitaka Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na
vyeo vingine vya juu wakistaafu wawe kama wananchi wa kawaida wasienziwe
kama ilivyo sasa kwani ni gharama kubwa kwa uchumi wa Taifa.
“Rais
ana pensheni kubwa na marupurupu mengi kwa hiyo alipwe akawe kama
mwananchi wa kawaida asiendelee kutunzwa ma Serikali,” alitoa maoni yake
kwa Tume inayochukua maoni juu ya kuandikwa kwa Katiba Mpya.Alitaka pia
rasilimali za Taifa ziwe za Muungano na zimilikiwe na dola.
Katika
hatua nyingine wakazi wengi waliotoa maoni yao juu ya kuandikwa Katiba
Mpya nchini walitaka mfumo wa sasa uendelee, lakini Rais wa Zanzibar awe
Makamu wa Rais wa Muungano.
Wakitoa maoni yao katika maeneo ya
Mgeni Haji, Mitakawani na Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja
jana walipendekeza mfumo wa Serikali ya Muungano na Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar uendelee.
Lakini wananchi hao walitaka Rais wa
Zanzibar awe Makamu wa Rais wa Muungano badala ya kuwa waziri katika
Muungano kama ilivyo sasa.Pia wananchi hao walitaka kero zote za
Muungano ziondolewe ili Muungano uimarike na misaada kutoka nje igawiwe
kwa pande zote mbili za Muungano yaani Bara na Zanzibar.
Awali
mkazi Zanzibar, alishauri Katiba Mpya iwe na kipengere kitakachowatoa
Ikulu Marais wanaomaliza muda wao na kutaka kugombea awamu nyingine ili
wanapogombea wawe wanatoka nyumbani kwao badala ya kutoka Ikulu.
Akitoa
maoni yake mbele ya Tume ya Katiba iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja,
Hassan Pandu Ibada (40) mkazi wa Mpapa, Wilaya ya Kati alieleza kuwa
Rais anapaswa kutoka Ikulu wakati wa uchaguzi.
Alitaka Katiba Mpya
itoe nafasi ya kuwapo kwa Rais wa muda ambaye baada ya uchaguzi
atamkabidhi madaraka aliyeshinda katika uchaguzi mkuu.
“Rais
akiwa wa Muungano au wa Zanzibar asitoke Ikulu na kwenda kwenye viwanja
vya kampeni kuwania urais, aondoke Ikulu ili awe sawa na wagombea
wengine,” alieleza mwananchi huyo .
No comments:
Post a Comment