ASEMA MADAKTARI WASIOKUBALI MSHAHARA WA SERIKALI WAFUNGASHE VIRAGO
Boniface Meena
WAKATI
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka
akiendelea na matibabu Afrika Kusini, Rais Jakaya Kikwete amesema
Serikali haihusiki na kilichomtokea daktari huyo kwa kuwa alikuwa kiungo
muhimu katika majadiliano baina ya pande hizo mbili.
Rais
Kikwete alisema hayo jana katika hotuba yake ya kila mwezi, ambapo mbali
na suala hilo, pia alizungumzia sababu za mgomo wa madaktari na
usafirishaji wa wahamiaji haramu.
Dk Ulimboka ambaye alikuwa
anaratibu mgomo wa madaktari unaoendelea nchi nzima kutokana na Serikali
kushindwa kutimiza madai yao mbalimbali, anatibiwa figo na majereha
aliyoyapata katika sehemu mbalimbali za mwili, baada ya kutekwa na watu
wasiojulikana, kisha kupigwa, kung'olewa kucha, meno mawili na kutupwa
katika Msitu wa Pande, usiku wa kuamkia Jumatano iliyopita.
Tangu
kutokea kwa unyama huo uliofanywa na watu wasiojulikana, baadhi ya
wananchi na wanaharakati wamekuwa wakiilaumu Serikali kuwa inahusika na
utekaji huo na wengine wakienda mbali zaidi, kuwa watekaji walikuwa
wanamlazimisha kueleza nani yuko nyuma ya mgomo wa madaktari.
Rais
Kikwete, kama awali alivyosema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, walisema
wanatambua kuwa, Serikali nayo inatajwa katika orodha ya wanaotiliwa
shaka kuhusu kilichomtokea Dk Ulimboka, lakini yeye ameshangazwa na
hisia hizo, kwani haoni sababu ya Serikali kufanya hivyo.
"Dk
Ulimboka alikuwa kiungo muhimu katika mazungumzo baina ya Serikali na
madaktari. Ni kweli kwamba yeye si mtumishi wa Serikali, hivyo
hakustahili kuwa sehemu ya majadiliano haya. Kulikuwa na rai ya kutaka
asiwepo, lakini nilisema wamuache maadam madaktari wanamwamini kuwa
anaweza kuwasemea vizuri zaidi kuliko wao wenyewe walioajiriwa na
Serikali," alisema Rais Kikwete.
Alisema Serikali haina sababu ya
kumdhuru Dk Ulimboka kwa sababu suala la mgomo, Mahakama Kuu
imekwishatoa amri ya kuusitisha, hivyo anayekaidi amri hiyo atakuwa
ananunua ugomvi na mhimili huo wa dola, ambao wenyewe una mamlaka ya
kumtia adabu.
"Hivi baada ya kufika hapo Serikali iwe na ugomvi
na Dk Steven Ulimboka kwa sababu ipi na jambo lipi hata iamue kumdhuru?"
alihoji na kuongeza:
"Kama kuna mtu wa Serikali kafanya, itakuwa
kwa sababu zake binafsi na siyo za Serikali au kwa kutumwa na
Serikali," alisema Rais Kikwete.
Alisema alichofanyiwa Dk
Ulimboka kimemsikitisha na kumhuzunisha kwa kuwa ni kitendo cha kinyama
na kinyume kabisa na mila na desturi za Tanzania.
Alisema
Watanzania hawajazoea mambo hayo na kwamba ameelekeza vyombo vya ulinzi
na usalama kufanya uchunguzi wa kina ili ukweli ujulikane.
"Nimesema
kuwa ningependa ukweli huo ujulikane mapema ili tuondoe wingu baya la
kutiliana shaka na kulaumiana kunakoendelea hivi sasa," alisema.
Alisema
anatoa mkono wa pole kwa Dk Ulimboka na kumwombea apone haraka ili
aungane na familia yake na Watanzania wenzake katika ujenzi wa taifa.
Rais
Kikwete pia alimpongeza Juma Mgaza ambaye alimsaidia Dk Ulimboka kumtoa
katika pori alikotupwa na kumpeleka kituo cha polisi kwa moyo wake wa
huruma.
Kuhusu mgomo
Kuhusu mgomo unaoendelea
Rais Kikwete alisema, kiwango cha mshahara cha Sh3.5 milioni
wanachokitaka madaktari Serikali haina uwezo wa kukitoa, hivyo daktari
anayeona kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara
huo, awe huru kuacha kazi na kwenda kwa mwajiri anayeweza kumlipa kiasi
hicho.
Rais Kikwete alisema, kwa sasa Serikali haiwezi kuwaahidi
kuwa inao uwezo wa kuwalipa mshahara wa kuanzia wa Sh3.5 milioni na
posho zote zile, kwani ikifanya hivyo malipo ya daktari anayeanza kazi
yatakuwa Sh7.7 milioni kwa mwezi, kitu ambacho haitakiweza.
"Si
vyema kutoa ahadi hewa kwa watu tunaowaheshimu na kuwathamini kama
walivyo madaktari. Kutokana na ukweli huo basi kama daktari anayeona
kuwa hawezi kufanya kazi serikalini bila ya kulipwa mshahara huo awe
huru kuacha. Nasi tutamtakia kila la heri,"alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema, madaktari hawana sababu ya kugoma ili washinikize kulipwa mshahara huo kwani uwezo haupo.
"Kwa
nini upate usumbufu wa kuachishwa kazi na kutakiwa kuondoka kwenye
nyumba ya Serikali ndani ya saa 24. Jiepushe na yote hayo kwa kujiondoa
mwenyewe," alisema.
Alisema mamlaka za ajira zimeanza kuchukua
hatua hizo kwa wale wanaokwenda kinyume na sheria za kazi na wataendelea
kufanya hivyo kwa wote wanaoendelea kugoma.
Alisema anajua
baada ya hatua hizo kuchukuliwa kuna manun’guniko ya kuonewa
yatajitokeza, lakini ni bora kufanya hivyo ili ijulikane Serikali haina
daktari.
"Mlitegemea mwajiri afanyeje? Ni bora kufanya hivyo ili
ajue hana daktari aweze kufanya utaratibu wa kuziba hilo pengo na huyo
anayekuja awe na mahali pa kuishi."
Kutokana na hali hiyo amewasihi madaktari kuacha mgomo na kurejea kazini, kwani Watanzania wanateseka na kupoteza maisha.
Sababu za mgomo
Rais
Kikwete alisema kwamba, kuna masuala matatu ambayo yamekuwa na mwafaka
kwa kiasi fulani na kutoafikiana kwa baadhi ya mambo kati ya madaktari
na Serikali.
Alisema suala la kwanza ni suala la kufanya kazi
katika mazingira hatarishi ambalo Serikali imekubali hoja ya kuchukua
hatua ya kuwalinda madaktari wanaofanya kazi katika mazingira hatarishi.
Pia alisema Serikali imeeleza dhamira ya kurudisha posho ya
mazingira hatarishi kwa watumishi wa umma wanaostahili na utekelezaji
wake utafanyika baada ya uchambuzi wa kina wa kubainisha mazingira
hatarishi ni yapi, viwango stahiki viwe vipi na nani hasa wahusike.
Rais
Kikwete alisema kuwa, madaktari wamekataa suala hilo la kufanya
uchambuzi, wanataka kiwango kiwe kama wanavyotaka wao, yaani asilimia 30
ya mshahara na kianze mara moja.
Alisema suala la pili ambalo
wamekubaliana nusu nusu ni kuhusu nyumba za kuishi ambalo Serikali
imekiri wajibu wake wa kuwapatia nyumba za kuishi.
Rais Kikwete
aliongeza kwamba, kwa maeneo ambayo madaktari wanalipwa posho ya pango,
Serikali imesema waajiri wataendelea kufanya hivyo kwa mujibu wa
taratibu zilizopo kwa watumishi wa umma wenye stahili ya kupewa nyumba.
Alisema jambo hilo limekataliwa na madaktari na kutaka lazima walipwe asilimia 30 ya mshahara kama posho ya nyumba.
Rais
Kikwete alisisitiza kwamba, Serikali kwa upande wake imeona vigumu
kufanya hivyo na kuwasihi wakubali wanayotendewa kama wafanyakazi
wengine wote wa umma.
Alisema suala lingine ambalo lilikuwa na
makubaliano ya nusu nusu ni kuhusu posho ya kufanya kazi katika
mazingira magumu na pande zote mbili ziliafikiana kuwa yapo baadhi ya
maeneo nchini yanayo mazingira magumu kwa watumishi wa umma, hivyo hatua
zichukuliwe kuwasaidia watumishi hao.
Kuhusu posho, alisema
Serikali imekubali kuwapo posho ya aina hiyo ila itatekelezwa baada ya
kufanya uchambuzi wa kuainisha mazingira husika, kutambua watumishi
waliopo na gharama zake.
Alisema madaktari hawajakubali kusubiri zoezi la uchambuzi lifanyike, wanataka Serikali ilipe posho hiyo sasa.
"Tofauti
hapa si posho hiyo kuwapo, bali ni rai ya Serikali ya kubaini maeneo
yenyewe na kupanga aina ya hatua na viwango vya posho kulingana na
mazingira halisi ya maeneo. Madaktari hawaoni haja ya kufanya hayo,"
alisema.
Alisema kuna mambo mawili ambayo hayakuwa na mwafaka
kabisa kati ya pande hizo mbili na la kwanza ni posho ya kuitwa kazini
(on call allowance).
Rais Kikwete alisema, Serikali ilishaongeza
posho hizo tangu Februari, 2012 posho iliongezwa kutoka Sh10,000 hadi
Sh25,000 kwa daktari bingwa, Sh20,000 kwa dakari mwenye usajili wa
kudumu na Sh15,000 kwa madaktari waliohitimu ambao wapo katika kipindi
cha mafunzo kazini (Interns).
Alisema hata hivyo, madaktari kwa upande wao hawakukubali uamuzi huo wa Serikali na kusisitiza walipwe asilimia 10 ya mshahara.
Rais
Kikwete alisema ugumu wa kukubali pendekezo la madakari ni kuwa sharti
la malipo haya ni mtu kuitwa kazini na kwamba ukitaka ilipwe kiwango cha
mshahara ina maana kuwa hata kama daktari hakupangwa kuitwa au
alipangwa na hakutokea aendelee kulipwa.
Alisema jambo la pili
ambalo mwafaka haukufikiwa baina ya Serikali na madaktari ni kuhusu
mshahara wa kuanzia kazi wa daktari ambao madaktari wanataka uwe Sh3.5
milioni wakati Serikali inasema kiasi hicho hatukiwezi.
Alisema
Serikali imeeleza utayari wake wa kuongeza mshahara kwa kati ya asilimia
15 mpaka 20 kama ambavyo itafanya kwa watumishi wote wa umma katika
mwaka huu wa fedha.
Rais Kikwete alisema, kwa kiwango cha sasa
cha mshahara wao, daktari ataanzia kati ya Sh1.1 milioni na Sh1.2
milioni kutegemea kiwango kipi hatimaye kitaamuliwa.
"Madaktari wamekataa katakata na wameng’ang’ania Sh3.5 milioni," alisema.
Alisema
ni muhimu madaktari wakatambua kuwa wagonjwa wanateseka na wengine
kupoteza maisha kwa mgomo usiokuwa halali kisheria ambao pia haustahili
kuwapo hata kwa mujibu wa maadili ya udaktari.
Alisema viongozi wa MAT na wenzao wanawaingiza madaktari katika mgogoro na mahakama na waajiri wao isivyostahili.
Rais
Kikwete alisema ni vyema viongozi wa madaktari na madaktari wakatambua
kuwa wanashiriki katika mgomo usiokuwa halali ambao pia kiongozi wao
mkuu amekana mahakamani kuwa hahusiki nao.
Rais Kikwete alisema
madaktari lazima watambue pia kwamba ajira zao wanaziweka hatarini kwani
mfanyakazi hana kinga ya kutofukuzwa kazi na mwajiri kwa kushiriki
mgomo unaokubalika kisheria.
"Huu siyo. Watapoteza ajira, hawana
pa kukimbilia, hawana cha kuwalinda. Kwa madaktari interns,
wanahatarisha maisha yao, kwani hawatapata cheti cha kudumu wakishiriki
mgomo usiokuwa halali. Lazima watafakari kwa hayo wafanyayo," alisema.
Hoja za madaktari
Rais
Kikwete alisema katika mambo 12 ambayo madaktari waliyawasilisha pande
zote mbili zilifikia mwafaka na kukubaliana kwa pamoja kwa mambo saba.
Alitaja la kwanza ni kuhusu usafiri wa kwenda na kurudi kazini ambalo limeshashughulikiwa.
Alisema
jambo la pili, ni madaktari kupatiwa Green Card za Bima ya Afya ambalo
Serikali na Wizara ya Afya zimechukua hatua za utekelezaji wake.
Jambo
la tatu, alilitaja Rais Kikwete kuwa ni hatua za kinidhamu kuchukuliwa
dhidi ya Watendaji Wakuu wa Wizara ya Afya ambalo tayari Serikali
imechukua hatua.
"Uongozi wa juu wa wizara umebadilishwa na sasa
kuna uongozi mpya. Lakini, jambo la kustaajabisha hata Waziri mpya wa
Afya alipowataka waonane kuzungumzia hoja walikataa kumuona. Kwanza
walisema hawaoni sababu kwa vile wameyazungumza na kamati yake kwa miezi
mitatu bila ya mafanikio," alisema.
Rais Kikwete alisema kuwa,
jambo la nne walilokubaliana ni viongozi kuwalazimisha kupewa rufaa ya
kutibiwa nje suala ambalo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewaeleza
madaktari wazingatie maadili ya kazi zao na kukataa kutoa rufaa kwa mtu
asiyestahili awe kiongozi au asiwe kiongozi.
Alisema jambo la tano ambalo pande zote mbili zilikubaliana ni kuhusu madaktari waliofukuzwa.
"Hawa
ni wale Interns waliokuwa wamerudishwa wizarani kutoka Muhimbili na
kupangiwa hospitali za Temeke, Ilala, Mwananyamala na Lugalo. Hili ni
jambo ambalo lilikuwa limemalizika kitambo na wote walikuwa wamerudi
Muhimbili," alisema.
Rais Kikwete alisema jambo la sita ni kuhusu
mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa na madaktari kuhusu kuboresha
huduma ya afya ambalo Serikali imeliafiki.
Rais Kikwete alisema jambo la saba, ambalo pande zote walilokubaliana ni kuhusu kuongeza posho ya uchunguzi wa maiti.
Alisema
jambo hilo jipya halikuwepo mwazoni, hata hivyo, Serikali imelikubali
na posho hiyo imeongezwa kutoka Sh 10,000 hadi kufikia Sh100,000 kwa
daktari na Sh50,000 kwa wasaidizi wake,” alisema.
No comments:
Post a Comment