TAARIFA MPYA ZAELEZA YUKO UJERUMANI SI AFRIKA KUSINI, RAFIKI YAKE ATOA USHUHUDA MPYA WA JINSI ALIVYOTEKWA
Waandishi wetu
WAKATI
ikielezwa kwamba Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka
anatibiwa Afrika Kusini, kuna taarifa kwamba amelazwa katika hospitali
moja ya huko Ujerumani.Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza
kuwa Dk Ulimboka alipelekwa Afrika Kusini lakini alikaa kwa muda mfupi
tu kabla ya kupelekwa Ujerumani anakoendelea na matibabu yake sasa.
Awali,
jopo la madaktari waliokuwa wanamtibu Dk Ulimboka hapa nchini lilieleza
kuwa baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili, waliamua kumpeleka Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
“Ni
kweli alikwenda kwanza Afrika Kusini, lakini hapo alipita tu. Ndege
ilitua na akaunganisha ndege nyingine kwenda Ujerumani,” kilisema chanzo
kimoja cha habari.
Hata hivyo wakati chanzo hicho kikieleza hivyo,
mmoja wa wanafamilia yake, alisema: “Sisi katika level (ngazi) ya
familia tunajua yuko Afrika Kusini lakini hii haiwazuii madaktari
kumhamishia kwenye hospitali nyingine wanayoona inafaa.”
Mwanafamilia
huyo ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema suala la Dk Ulimboka
kuhamishiwa Ujerumani si la ajabu kwani anachotafuta ni matibabu ya
uhakika.
Alipoulizwa kuhusu habari hizo, Kiongozi wa Jopo la
Madaktari waliokuwa wakimtibu, Profesa Joseph Kahamba alisema: Mimi
ndiyo kwanza nasikia, lakini kwa nature (aina) ya tukio lake, si vyema
ikaanikwa amepelekwa wapi. Pia si vizuri ikaelezwa yuko wapi ingawa
tayari watu wanajua yuko Afrika Kusini.”
“Kama kiongozi wa jopo
la madaktari wanaomtibu Dk Ulimboka ninajua kwamba yuko Afrika Kusini
ingawa hata hiyo taarifa tusingependa watu waijue kwa jinsi tukio
lilivyokuwa.”
Mmoja wa madaktari ambaye hakutaka jina lake
litajwe gazetini alipoulizwa juu ya suala hilo alipinga na kusema;
“Habari za aina hiyo mtakuwa mnazipata nyingi, najua mtaandika, ndiyo
maana mnaandika madaktari Muhimbili wanafanya kazi wakati si kweli”.
Alisisitiza
kuwa Dk Ulimboka yupo Afrika Kusini anakopatiwa matibabu na kusisitiza
kuwa habari alizokuwa nazo tangu juzi jioni ni kwamba anaendelea
vizuri.
Katibu wa Chama cha Taifa cha Madaktari (MAT), Dk Rodrick
Kabangila alipoulizwa juu ya hali ya Dk Ulimboka alisema kwa mujibu wa
taarifa za juzi jioni alikuwa anaendelea vizuri.
Alipoulizwa juu
ya taarifa za kupelekwa Ujerumani aliguna kisha akasema: “Naomba
ieleweke kuwa yupo Afrika ya Kusini kwa matibabu.
Rafiki asimulia mkasa
Rafiki
wa karibu wa Dk Ulimboka aliyekuwa naye wakati mkasa wa kutekwa
ukitokea, Dk. Deogratius Michael ameelezea tukio zima lilivyotokea na
kusema ulikuwa wa kitaalamu na ulifanywa na watu wenye ujuzi na mambo
hayo.
Dk Deogratius alisema jana kwamba siku ya tukio walikuwa
wametokea kwenye msiba wa ndugu wa mwalimu wao Profesa Yongolo na baada
ya msiba walikwenda Viwanja vya Leaders saa moja usiku kuangalia taarifa
ya habari na mambo mengine.
Huko walikutana na madaktari wengine
na ilipofika saa 4:00 usiku, Dk Ulimboka aliwaambia kwamba kuna jamaa
alikuwa akimtafuta hivyo angependa kwenda kukutana naye.
“Tukamwuliza
anamtafutia nini? Akatueleza kuwa kwa siku tatu huyo jamaa anamtafuta.
Wenzangu wakasema asiende mwenyewe na mimi ndiyo nikamsindikiza. Mara ya
kwanza huyo jamaa alisema anaitwa Abeid na alisema yuko Sterio,
tukaenda huko hatukumkuta tukaenda Hugo hatukumkuta lakini baadaye
tukakutana naye maeneo ya Barabara ya Tunis karibu na Ofisi za Ultimate
Security.”
Dk Deogratius alisema wakati wakiendelea na
mazungumzo, Abeid alikuwa akitaka kujua nini kinachotakiwa ili kutatua
mgogoro uliopo wa madaktari.
“Wakati tunamalizia mazungumzo
nilikwenda msalani, niliporudi Abeid alikuwa akizungumza na simu kila
wakati, tuliendelea na mazungumzo hadi tukamaliza na kuanza kuagana,”
alisema.
Alisema wakati wakiagana bado walikuwa wamekaa katika
viti pamoja na Abeid... “Ghafla kuna watu walifika na kusema kuwa
wanamtaka Dk Ulimboka. Walimchukua na kwenda naye katika gari. Walikuwa
watano, walikuwa ‘giant’ (miili mikubwa) na ‘very skilled’ ( wenye
uzoefu) wakamchukua Dk Ulimboka wakaenda naye kwenye gari,” alisema Dk
Deogratius.
Alisema wakati huo Abeid alikuwa anakimbia hivyo akamkimbilia ili ampe namba yake ya simu ambayo ingemsaidia kwa mawasiliano.
“Alinipa namba yake nikampigia muda huohuo lakini nilipokuja kumpigia tena sikumpata na mpaka leo hapatikani,” alisema.
Alisema baada ya tukio hilo alimpigia mke wa Dk Ulimboka na kumweleza na pia alipiga simu polisi kuwaeleza.
“Nilikwenda
polisi kutoa maelezo na nikawapa namba zangu za simu zote ili wanipigie
kama watapata chochote, lakini mtu wa kwanza kunipigia asubuhi (kesho
yake) alikuwa Juma Mgaza (aliyemwokota Dk Ulimboka) ambaye alinieleza
kuwa kuna rafiki yangu amempa hiyo namba na kwamba yuko hoi amepigwa.”
Alisema
baada ya kupata simu hiyo aliwasiliana na watetezi wa haki za binadamu
ambao walimtaka waende pamoja na kwamba walipokuwa njiani kuelekea Kituo
cha Polisi Bunju alipigiwa simu na polisi wa kituo hicho.
Kutokana na hali hiyo aliomba iundwe tume huru ikijumuisha wanasheria, madaktari na watu wengine ili ukweli ujulikane.
Upelelezi wa Polisi
Kamanda
wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema jopo la
upelelezi aliloteua hivi karibuni kushughulikia tukio zima la kutekwa
kwa Dk Ulimboka litaendelea na kazi yake hadi mwisho na hatasikiliza
kelele za wanaodai kutokuwa na imani nalo.
Alisema madai
yanayotolewa na watu mbalimbali akiwemo Dk Ulimboka mwenyewe kuwa hana
imani na jopo hilo hazitabadili chochote kwani kinachofanyika hivi sasa
ni kazi ya kawaida ya upelelezi ya jeshi hilo... “Hao wanaosema hawana
imani na jopo hilo hawana hoja isipokuwa waliache jeshi la polisi
lifanye kazi yake.
Kiongozi huyo wa mgomo wa madaktari alitekwa na kisha kujeruhiwa vibaya na baadaye kutelekezwa katika Msitu wa Pande.
Habari hii imeandikwa na Geofrey Nyang’oro, Boniface Meena na Joseph Zablon.
No comments:
Post a Comment