CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake (TAMWA),
kimewataka viongozi wote ngazi ya wilaya kwa kushirikiana na wabunge
kukemea vitendo vya unyanyasaji wa vipigo kwa wanawake nchini.
Kauli hiyo imetolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji
wa TAMWA, Ananilea Nkya alipokuwa akizindua na kutoa ufafanuzi juu ya
utafiti uliofanyika hivi karibuni mikoa mbalimbali nchini, ambao
umebaini ongezeko la vipigo kwa wanawake.
Alisema katika ripoti ya utafiti huo mbali na kuibua masuala anuai ya
vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia imeonesha kuwepo kwa idadi kubwa ya
vipigo kwa wanawake vinavyofanywa na wanaume jambo ambalo linakwamisha
juhudi za maendeleo ngazi ya familia.
Alisema idadi kubwa ya wanawake vijijini ni wazalishaji mali wazuri,
hivyo endapo suala la vipigo litafumbiwa macho na Serikali kupitia
viongozi wake juhudu za maendeleo katika jamii zitakwamishwa.
“Ukatili wa vipigo ni tatizo kubwa…na wote tunajua mtu anayepata
kipigo kira mara hawezi kuwa mzalishaji mali mzuri, suala hili
likifumbiwa macho umasikini mkubwa utaendelea kuzigubika familia zetu,
hasa maeneo ya vijijini,” alisema Nkya katika ufafanuzi wake.
Aidha alisema katika utafiti huo uliofanywa kwa ushirikiano na waandishi
kutoka vyombo anuai vya habari Tanzania, ukiwemo Mtandao wa
Thehabari.com baadhi ya viongozi ngazi za Wilaya wameonekana kuwa
vikwanzo katika utoaji wa taarifa hasa katika Wilaya za Tarime, Mvomero
pamoja na Wilaya ya Kinondoni.
Ameongeza kuwa utafiti umebaini kuwepo kwa baadhi ya watendaji hasa
wa vijiji kutofanya kazi zao ofisini jambo ambalo limekuwa kero kwa
wananchi na kushindwa kutimiza wajibu wao.
Utafiti huo wa kihabari (journalistic survey) uliofanyika kuanzia
mwezi Aprili 2012, TAMWA ulifanyika katika katika mikoa 20 ikiwepo 15 ya
Tanzania Bara na mitano ya Zanzibar, ambapo pamoja na mambo mengine
uliangalia vitendo vya ukatili nchini. Vitendo vilivyolengwa ni ubakaji,
vipigo kwa wanawake, kutelekeza wanawake na watoto, ukeketaji na
kulazimisha watoto wa kike kulazimishwa kukatisha masomo na kuolewa.
No comments:
Post a Comment