Geofrey Nyang’oro
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven
Ulimboka amewasili Afrika ya Kusini kuanza kupatiwa matibabu. Dk
Ulimboka alisafirishwa juzi kwa ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la
Afrika ya Kusini kwenda nchini humo, baada ya hali yake kubadilika
ghafla Alhamisi wiki iliyopita.
Jopo la madaktari lililokuwa
likimhudumia, Dk Ulimboka lilitoa taarifa kuwa figo zake zimeshindwa
kufanya kazi na juhudi zao kusafisha damu yake kutokutoa matokeo mazuri,
hivyo kushauri apelekwe nje ya nchi kwa matibabu zaidi.
Katibu wa
Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alilieleza Mwananchi jana, kuwa
Dk Ulimboka alifika salama Afrika ya Kusini na kuwa kwa sasa anaendelea
na matibabu.
“Habari nilizopata kutoka Afrika Kusini zinaeleza
kuwa amefika salama jana (juzi) na anaendelea vizuri baada ya kupata
huduma zinazohitajika,”alisema.
Dk Chitage ambaye hakuwa tayari
kutaja ni hospitali gani anatibiwa, alisisitiza kuwa huduma alizozipata
nchini humo zimenza kumsaidia.
Hata hivyo, habari zaidi
zilizopatikana jana zilieleza kuwa Dk Ulimboka wenzake wawamekataa
kutaja hospitali hiyo kwa sababu za kiusalama, na kwamba hali yake
ilikuwa bado haijabadilika sana.
“Hakuna mabadiliko yoyote,
walifika salama jana (juzi) na kwa kuwa anatibiwa katika hospitali ya
kulipia, huduma zimeanza jana (juzi) ileile,” alisema daktari mmoja
ambaye yupo karibu na Dk Ulimboka.
Mgomo
Katika
hatua nyingine, Dk Chitage alisema madaktari wanaendelea na mgomo nchi
nzima, licha ya vitisho vinavyoendelea kutolewa na Serikali.
“Kuhusu
mgomo upo palepale, sisi tunaendelea hadi madai ya msingi tuliyotoa
likiwamo la uboreshwaji wa huduma za afya pamoja na sitahili zetu
yatakaposikilizwa na Serikali,” alisema Dk Chitage.
Dk Chitage
alisema, madaktari kote nchini wanatarajia kukutana kujadili mambo
mbalimbali kati ya leo na kesho na kutoa taarifa kwa umma kueleza
matokeo yake.
Dk Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana usiku wa
kuamkia Jumatano, akapigwa, na kujeruhiwa vibaya kisha kutupwa katika
Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mkataba hospitali binafsi
Serikali
ipo katika mchakato wa kuingia mkataba na hospitali binafsi nchini kote
kuhudumia wagonjwa ambao wanakosa matibabu kutokana na mgomo wa
madaktari unaoendelea nchi nzima.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi
wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema, Serikali imechukua hatua hiyo ili
ziweze kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa.
Alisema kwa upande wa huduma za wajawazito na watoto, zitaendelea kutolewa bure katika hospitali za Serikali na binafsi.
Mganga
Mkuu wa Manispaa ya Kinondoni, Dk Gunini Kamba alisema tayari
wameshaingia mkataba na Hospitali ya TMJ kutoa huduma ya matibabu katika
kipindi cha mgomo uliopo.
Dk Kamba alisema huduma zitakazotolewa
ni za magonjwa yote na kwamba wagonjwa watachangia kiasi kidogo cha
fedha kama walivyokuwa wakichangia katika hospitali za Serikali.
Alisema
wagonjwa walioandikiwa kupimwa kipimo cha CT-Scanr na X-Ray watachangia
kiasi kidogo cha fedha kama walivyokuwa wakichangia katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa
Hospitali hiyo, Dk Tayabali Jafferji alisema wamekubaliana na Serikali
kutoa huduma ya matibabu ambapo mgonjwa atatoa gharama ndogo ya
matibabu.
KCMC
Athari za kuondolewa kwa
madaktari zaidi ya 80 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, zinatarajiwa
kuanza kuonekana leo huku hospitali hiyo ikifunga kliniki zote za
wagonjwa hospitalini hapo.
Taarifa zinadai mbali na kutimuliwa kwa
madaktari hao 80, baadhi ya madaktari wanaosomea ubingwa (resident
doctors) zaidi ya 50 nao wamelimwa barua kutokana na kujihusisha na
mgomo huo.
“Jana (juzi) jioni wanaosomea ubingwa nao walipewa
barua warudi kwa Provost (mkuu wa chuo) wa chuo kikuu cha utabibu
kilichomo chini ya Chuo Kikuu cha Tumaini,” kilidokeza chanzo chetu.
Tayari
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dk Martin Shao amewasihi madaktari katika hospitali
hiyo kuweka mbele masilahi ya wagonjwa.
Wakati huohuo, uongozi wa
Hospitali ya Serikali ya Mkoa Kilimanjaro ya Mawenzi umeamua kurudisha
huduma za upasuaji katika chumba cha zamani ambacho kilifungwa Desemba
27, 2010 na wataalamu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutokana na
kukosa sifa, hivyo kuifanya hospitali hiyo kutokuwa na huduma ya
upasuaji.
Mtikila atoa tuhuma
Mwenyekiti wa
Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amemtaka Rais
Jakaya Kikwete kujiuzulu nafasi yake hiyo kutokana na watu wa Idara ya
Usalama wa Taifa kutajwa katika tukio la kumpiga na kumjeruhi Dk
Ulimboka.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari
uliofanyika Dar es Salaam jana, Mtikila alidai kuna ushahidi wa kutosha
wa watu wa idara hiyo kuhusika na alidai kuwa, baadhi yao wamejibainisha
wenyewe, na mwingine aliyetambuliwa na Dk Ulimboka mwenyewe.
Alisema
Rais Kikwete anapaswa kujiondoa katika nafasi hiyo vinginevyo
ahakikishe watendaji wa idara hiyo ambao wanatuhumiwa kuhusika na kipigo
na mateso dhidi ya Dk Ulimboka wanatiwa mbaroni badala ya kuunda tume
kuchunguza suala hilo.
Kuhusu mmoja wa maofisa wa Jeshi la Polisi
kupigwa na watu wenye hasira siku Dk Ulimboka alipofikishwa katika
Taasisi ya Mifupa (Moi), alisema askari huyo akiwa chooni kwa kutumia
‘radio call’, alisikika akiwaeleza wenzake kuwa Dk Ulimboka hajafa hali
ambayo inaonyesha kuwa kulikuwa na mpango unaotekelezwa na jeshi hilo.
Tangazo Moi
Uongozi
wa Taasisi ya Mifupa (Moi) umebandika tangazo linalowataka madaktari
wote wanaotaka kuendelea na kazi kujisajili, na mwisho usajili huo ikiwa
ni leo.
Tangazo hilo lilitolewa baada ya kikao cha Bodi ya
Wakurugenzi wa Moi na kilichokaa Juni 29 na kutoa siku tatu za mwisho wa
wiki kwa madaktari wote kujisajili kwa Mkurugenzi wa Tiba.
Katika
hatua nyingine hali katika Hospitali za Rufaa za jijini Dar es Salaam
,Amana na Temeke na Mwananyamala huduma ziliendelea kwa kusuasua
kutokana na mgomo unaoendelea.
Arusha
Uongozi
wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mt Meru umelazimika kuitisha kikao cha
pamoja na madaktari wa hospitali hiyo kwa lengo la kuwasihi waachane na
mgomo.
Kwa mujibu wa vyanzo vya habari kikao hicho kiliitishwa na
Mganga Mkuu Mfawidhi, Dk Eliringia Mlay, siku moja tu baada ya Dk
Ulimboka kutekwa na kisha kujeruhiwa na watu wasiojulikana.
Katika
kikao hicho madaktari hao wakizungumza kwa jazba, walitishia kugoma na
kubainisha ya kwamba kamwe hawawezi kuwa na ari ya kufanya kazi, ihali
mwenzao kaumizwa, na hivyo kuonyesha hofu ya usalama wa maisha yao.
Dk,Mlay
alipoulizwa na gazeti hili alikiri uongozi wa hospitali hiyo kuitisha
kikao hicho na kubainisha ya kwamba, lengo lake lilikuwa ni kuwasihi
wasigome ili kuokoa hali za maisha za wagonjwa hospitalini hapo.
Imeandaliwa
na Pamela Chilongola, Joseph Zablon, Geofrey Nyang’oro, Aidan Mhando,
Dar; Daniel Mjema, Moshi na Moses Mashalla, Arusha
1 comment:
tunaomba mtuwekee picha za wanaharakati waliokuwepo airport kumuaga dr. ulimboka ili tuliokosa kwenda tujionee harakati hizo pevu!!
Post a Comment