- Ni Mzanzibari aliyetorokea Uarabuni
- Ana mahekalu jirani na vigogo Zanzibar
- Kuna utata kuhusu deni la Bil.100/- na rehani ya mitambo
WAKATI Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) likielezwa kuanza kuwasha mitambo ya Dowans, mmiliki wa kampuni hiyo aliyezua utata, Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi, ni Mzanzibari aliyeukana uraia wake baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Raia Mwema limeelezwa.
Habari kutoka Zanzibar alikozaliwa Al Adawi ambaye ni brigedia jenerali mstaafu wa jeshi la Oman, zinaeleza kwamba mfanyabiashara huyo alikuwa askari polisi wa Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964 na alikimbia kama walivyofanya baadhi ya Wazanzibari katika kipindi hicho.
Mtu anayemfahamu kwa karibu Al Adawi, ameliambia Raia Mwema : “Brigedia kimsingi ni Mtanzania maana aliondoka nchini kama Wazanzibari wengi walivyoondoka na wakaukana uraia wao walipofika nje ya nchi ili kupata hifadhi ya kisiasa na kiuchumi.”
Akizungumza kutoka Zanzibar, mtoa habari huyo anasema kwamba baada ya kufika Oman alijiunga na jeshi la nchi hiyo na kubahatika kuwa mmoja wa walinzi wa karibu wa Sultani Qaboos bin Said al Said wa nchi hiyo, ambako alipata wasaa wa kujijenga kabla ya kustaafu na kuamua kuwa mfanyabiashara.
Miongoni mwa watu aliowahi kusoma nao kabla ya kuondoka nchini ni aliyekuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk. Salmin Amour ambaye ndiye anatajwa kumpokea tena Visiwani humo.
“Aliporudi nchini, Dk. Salmin alimsaidia kufanikisha kuuziwa nyumba ya Serikali eneo la Mazizini ambako wanaishi viongozi na watu mashuhuri kisiwani na nyumba yake inapakana na kiongozi mmoja wa juu wa sasa wa SMZ. Ana nyumba mbili pwani ya Mashariki na Pwani ya Magharibi ambazo anafikia anapokuja Tanzania,” anasema.
Taarifa zisizo rasmi zimeeleza kwamba, jana Jumanne, Al Adawi alitarajiwa kukagua mitambo ya Dowans eneo la Ubungo, ambako imeelezwa kuanza kuwashwa kwa majaribio wakati mazungumzo kati yake na Serikali na TANESCO yakiendelea kwa ajili ya kuzalisha umeme kuingiza kwenye gridi ya taifa.
Ilielezwa kwamba mtambo mmoja wa Dowans aina ya LM6000 PD 40MW uliopo viwanja vya TANESCO uliwashwa na kwamba ulikuwa ukizalisha megawati 37 kuchukua nafasi ya mitambo ya Songas iliyokuwa ikizalisha megawati 60 ambayo ilielezwa kupata hitilafu Jumapili.
Ofisa mmoja wa serikali aliliambia Raia Mwema jana kwamba kuna mchezo mchafu unaoendelea kuhusiana na Dowans na akahoji :“Imekuaje tatizo la umeme kuwa kubwa wakati Songas ikizalisha Megawati 60 za umeme na tatizo hilo likaja kupungua ilipowashwa mitambo ya Dowans inayozalisha umeme mdogo wa Megawati 37 tu ? Hii ni kuonyesha kwamba hawa jamaa wamepambana kufa na kupona Dowans iendelee kuvuna fedha zetu.”
Habari zinaeleza kwamba kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka kwa wanasiasa kutaka Dowans iwashe mitambo yake na kwamba hivi sasa kumekuwa na vikao vya mara kwa mara kuanzia mwishoni mwa wiki hii kutafuta njia za kutekeleza maelekezo hayo kutoka kwa wanasiasa.
Mitambo ya Dowans ambayo iliwashwa juzi Jumatatu ilizimwa jana asubuhi na ilitarajiwa kuwashwa jana jioni wakati vikao vikiendelea kuhusiana na jinsi ya kuitumia mitambo hiyo kuzalisha umeme na kuuingiza kwenye gridi ya Taifa.
Habari zimeelezwa kwamba mitambo hiyo itawashwa kwa kile kinachoitwa ‘best practice’ kwa shinikizo la Serikali na kwamba zitatumika njia za ‘kuwaziba mdomo’ watu wanaopinga mpango huo wakiwamo wanasiasa na waandishi wa habari.
Kuwashwa kwa mitambo hiyo kumekuja huku Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, January Makamba, akiendelea kupigia debe kuwashwa kwa mitambo hiyo.
Mitambo hiyo imewashwa siku moja baada ya Al Adawi anayedai kuwa ndiye mmiliki wa kampuni ya Dowans, kuwasili nchini na kuzungumzia sakata la fidia ambayo kampuni yake hiyo inaidai TANESCO kutokana na kukatisha mkataba wake kinyume cha sheria.
Al Adawi aliingia nchini na kukutana na baadhi ya wahariri wa vyombo vya habari, lakini kikao chake hicho kimeibua utata mwingi kutokana na kukataa kupigwa picha, lakini pia kutojibu maswali mengi ya msingi ambayo yanamhusu yeye binafsi na kampuni yake hiyo. Dowans sasa inaidai TANESCO Shilingi bilioni 94 zilizotolewa kama tozo kwa kile kilichoelezwa kukiuka mkataba.
Kwa mara ya kwanza Al Adawi alipozungumza na mwandishi wa habari mmoja nchini Marekani, alikana kuifahamu Dowans kabla ya kukiri baadaye alipozungumza na mwandishi huyo kwa mara ya pili, hali iliyozidi kutia shaka uadilifu wa mwekezaji huyo.
Al Adawi ambaye ni mmmoja wa waanzilishi wa kampuni ya Services and Trade ya Usultani wa Oman alimtaka mwandishi huyo kutembelea tovuti ya makampuni yake ya (http://www.stcgroups.com) kuona kama kuna kampuni ya Dowans na kwamba wao hawafanyi biashara ya nishati.
Alipoelezwa kwamba mwandishi alikwisha kuitembelea, Al-Adawi alisema, “hatuna kampuni yenye jina hilo. Kama ungetembelea tovuti yetu ungeona kuwa sisi hatujishughulishi na mambo ya nishati; tuko kwenye mambo ya ujenzi”
Katika mahojiano hayo, yaliyofanyika mwaka 2009 na ambayo sauti yake iliwekwa katika mtandao, Al-Adawi, alimpa changamoto mwandishi kwamba kama kuna kampuni ambayo inatajwa kuwa ni yake, na ambayo hajawekeza fedha zake ndani yake, angefurahi sana kama angeweza kupewa kwa bure kampuni ya namna hiyo.
Baada ya Al-Adawi kuelezwa na mwandishi huyo kwamba jina lake limo katika fomu namba 201c za BRELA akitajwa kuwa ni mkurugenzi wa kampuni ya Dowans Tanzania Limited akiwa ameweka sahihi yake Januari 26, 2007, alibadili msimamo na kukiri kuifahamu kampuni hiyo.
Anuani yake aliyoitumia katika fomu hiyo ni P.O.Box 823, PC 112, Sultanate of Oman, anuani ambayo inatumika pia na kampuni ya Services and Trade ya Oman ambayo aliianzisha na mshirika wake mwingine mwaka 1977 na hivyo kuondoa utata wowote wa kuhusika kwake kwenye kampuni ya Dowans Tanzania Limited.
Baada ya kuelezwa kuhusiana na nyaraka za BRELA, Al-Adawi alikiri kuwa kampuni hiyo ni yake na kwamba pekee ndiye mhusika wake na kwamba “aliombwa” kwenda kuleta majenereta nchini wakati ule wa dharura baada ya kampuni ya Richmond kushindwa kufanya hivyo.
“Nimewaletea majenereta mapya kabisa ; sasa kama hawataki mimi nitayaondoa” alisema Bw. Al-Awadi. Alipoulizwa kuhusu kampuni ya Dowans Holding (siyo Dowans Tanzania Limited) imeandikishwa wapi, Al-Adawi hakuwa tayari kujibu na badala yake alianza kutoa vitisho.
Kwa muda mrefu kumekuwa kukitajwa karibu kampuni nne za Dowans ambazo zote zinahusiana na Dowans Tanzania Limited.
Mwanzoni kuna kampuni iliyotajwa kuwa ni Dowans Holdings ya “Falme za Kiarabu” lakini imethibitika kwamba hakuna kampuni yenye jina hilo baada ya Taasisi ya Uwekezaji ya Dubai na Wizara ya Uchumi na Biashara ya Falme za Kiarabu ambayo inatoa leseni za biashara kutokuwa na rekodi za kampuni hiyo wala Idara ya Kanda Huru za Falme za Kiarabu.
Kampuni pekee ya Dowans ambayo inaonekana kuhusiana na Dowans Tanzania Limited ni ile ya Costa Rica ambayo imeonekana ni kampuni hewa huku wamiliki wake nao wakijificha.
Costa Rica ni mojawapo ya nchi ambazo sheria zake za uwekezaji na fedha zinakaribisha sana watu kufungua makampuni feki na zinalinda wawekezaji hao kutokujulikana na ni rahisi kufungua biashara yoyote huko hata kwa mtu mgeni.
Uhalali wa Dowans kisheria nao una utata baada ya usajili wake kuhusisha kampuni ya Portek International kupitia kampuni yake tanzu ya Portek Systems and Equipment Ltd kama mojawapo ya makampuni yenye hisa ya asilimia 39 kwenye kampuni ya Dowans Tanzania Limited.
Imethibitika kwamba kampuni hiyo ya Portek kwa mwaka 2007 na 2008 haikuwa na hisa yoyote kwenye kampuni ya Dowans Tanzania Limited wala kuonesha kuwa wanaitambua kwa namna yoyote ile kampuni hiyo tata ambayo imekuwa gumzo kwa sasa.
Kwa upande wa Afrika kampuni hiyo ya Portek Systems and Equipment ilikuwa inafanya kazi nchini Algeria kupitia kampuni ya Bejaia Mediterranean Terminals S.p.a. Portek ina hisa za asilimia 15 kwenye kampuni moja tu ya kigeni, nayo iko Phillipines, lakini ni jambo la kushangaza kuona kwamba wameshindwa kuikumbuka kampuni “yao” ambayo wana hisa 39 ndani yake.
Katika mahojiano ya awali ya Al-Adawi inaonekana hakuwa anafahamu kuwa majenereta “yake” yalitumika kuchukulia mkopo wa karibu shilingi bilioni 100 kutoka kwenye mabenki kadhaa nchini. Kwa kadiri alivyokuwa anazungumza inaonekana yeye alikuwa anajua anachodaiwa ni Shilingi bilioni nane tu na habari kuwa kuna mikopo mingine ilichukuliwa huku majenereta yakiwekwa rehani zilikuwa ni habari ngeni kwake.
Alipoulizwa kama yuko tayari kuingia hasara endapo serikali itaamua kuyataifisha majenereta hayo, Al-Adawi alisema : “Unajua kwenye biashara kuna kupata na kukosa; sasa wakiyachukua niko tayari kuyakosa”.
Kati ya Aprili 30 na Novemba 9, 2007, ikiwa ni miezi kadhaa baada ya kuhaulishiwa mkataba kutoka Richmond, Dowans Tanzania Limited ilikopa fedha katika benki mbili tofauti, Barclays na Stanbic, zinazofikia bilioni 97.5/- na kuiweka dhamana mitambo hiyo ya kuzalishia umeme iliyoko Ubungo na mali zote za kampuni hiyo walizonazo sasa na zote ambazo zitapatikana baadaye.
Nyaraka zinaonyesha kuwa Dowans walikopa jumla ya dola za Marekani milioni 55 kutoka Barclays na dola nyingine milioni 20 za Marekani kutoka Stanbic tawi la Tanzania, fedha ambazo zinapaswa kulipwa kwa riba na gharama nyinginezo.
Dowans walipokopa dola za Marekani milioni 20 kutoka Stanbic tawi la Tanzania, dhamana iliyotajwa ni mitambo ya kuzalisha umeme, akaunti yao, mikataba, bima, na amana zote za kampuni hiyo tata.
Katika mawasiliano na kampuni hiyo benki ya Stanbic yenye makao yake makutano ya Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kinondoni, Dar es Salaam, iliwakilishwa na Helen Makanza na Jeff Daly wakati Dowans haionyeshi ni nani aliyewakilisha kampuni hiyo zaidi ya Wakili Samson Russumo, ambaye alikuwa Kamishna wa Kiapo.
Baadaye Juni, 2007, Dowans ilichukua mkopo mwingine wa dola za Marekani milioni 20 kutoka benki ya Barclays ya Mauritius, makubaliano yaliyoelezwa kufuata sheria za Uingereza.
Miezi minne baadaye, Dowans imebainika walichukua tena kiasi cha dola za Marekani milioni tano kutoka Barclays tawi la Tanzania, dhamana ikiwa ni mali zile zile zilizotumika kuchukua mkopo kutoka Stanbic na Barclays ya Mauritius.
Kampuni hiyo inaonekana katika nyaraka nyingine kuweka rehani mali zake na kuchukua dola za Marekani milioni 30, Novemba 9, 2007.
Wakati serikali ikiendelea kufanya mazungumzo na kampuni hiyo, haijafahamika kama mitambo hiyo imekwisha kuondoka mikononi mwa taasisi za fedha kutokana na kuchukua fedha hizo.
No comments:
Post a Comment