Thursday, February 3, 2011

NSSF kufua umeme wa megawati 300 Desemba

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeanza mchakato wa kuzalisha umeme wa megawati 300 ifikapo Desemba mwaka huu, ili kusaidia kuondoa kero iliyopo nchini sasa.

Hayo yalisemwa jana mkoani hapa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Dk. Ramadhani Dau, kwenye ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa wadau wa NSSF.

Dau alisema pamoja na kuzalisha umeme huo pia wanaangalia uwezekano wa kutandaza bomba la gesi kutoka Mnazi Bay hadi Dar es Salaam na Mwanza, lengo likiwa ni kusambaza gesi inayozalishwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Alisema shirika hilo limeshateua mshauri ili kusaidia kufikia azma hiyo na kupunguza kero ya kukatika kwa umeme ambayo husababisha shughuli za jamii kusimama kwa muda.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano, shirika hilo limeongeza idadi ya wanachama kutoka 380,693 mwaka 2005/06 hadi 506,216 mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 33, na ifikapo Juni mwaka huu, wanachama wa shirika hilo wanatarajiwa kufikia 518,410.

Aliongeza kuwa kwa upande wa wanachama makusanyo yameongezeka kutoka Sh. bilioni 126,96 hadi Sh. bilioni 315.31 sawa na ongezeko la asilimia 148, matazamio yao ni kukusanya Sh bilioni 404.58 ifikapo Juni mwaka huu.

Aidha, mwaka 2005/ 6 hadi 2009/10 shirika hilo liliongeza uwekezaji kutoka Sh bilioni 424.89 hadi Sh trilioni 1.03 sawa na ongezeko la asilimia 144, pia katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kwa kushirikiana na Serikali NSSF imewekeza kwenye miradi mbalimbali ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), nyumba za Polisi na nyumba za Jeshi la Wananchi.

Alisema miradi mingine imegharimu Sh bilioni 340.5 ambazo ni mkopo kwa Serikali na uwekezaji katika maeneo mbalimbali na kuongezeka kutoka Sh bilioni 477.76 mwaka 2005/06 hadi Sh trilioni 1.136 mwaka 2009/10 na Oktoba mwaka jana, NSSF ilipandisha
pensheni kwa asilimia 52 na hivyo wastaafu kuongezwa pensheni kutoka Sh.52,000 hadi Sh.80,000 kwa mwezi.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, malipo ya wanachama yaliongezeka kutoka Sh bilioni 40.18 mwaka 2005/06 hadi Sh. bilioni 102.82 mwaka 2009/10 sawa na ongezeko la asilimia 156.

"Nawasihi waajiri kulipa michango ya wafanyakazi kwa wakati ili wanufaike na shirika letu pia tunajitahidi kukamilisha miradi ya ujenzi wa daraja la Kigamboni na kujenga upya makazi kuanzia Mchikichini, lengo likiwa ni kubomoa nyumba mbovu na kujenga mji wa kisasa unaojitegemea - Satellite City".

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alilipongeza shirika hilo kwa kujenga majengo mbalimbali likiwamo la makazi na UDOM, daraja la Kigamboni na mpango wa kuzalisha umeme nchini, ili kuondoa kero kwa
wananchi.

Alisema wananchi watafarijika kusikia daraja la Kigamboni litajengwa wakati wowote lengo ni kurahisisha shughuli za maendeleo na alitoa angalizo kwa shirika hilo kutafiti sekta isiyo rasmi ambayo mchango wake ni mkubwa kwenye uchumi wa Taifa na kutoa angalizo kwa waajiri kupeleka michango ya wafanyakazi kwa wakati, ili kuepusha usumbufu baina ya mwajiri na mwajiriwa.

Katika mkutano huo wanachama saba na wastaafu wawili waliotekeleza sheria za NSSF na kupeleka makato ya wafanyakazi kwa wakati walizawadiwa.

Wanachama hao ni Kampuni ya Madini ya Bulyanhulu, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kampuni ya simu ya Vodacom, Chuo Kikuu cha St. Augustine, Mwanza; Sekta Binafsi, Said Salum Barkhresa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), Kiwanda cha Tobacco Alliance,
Morogoro; hospitali ya Lugoda, Mufindi na wastaafu Joram Elirai na Joseph Sikira.

No comments: